Flyover Morocco, Mwenge jijini Dar es Salaam zipo palepale

Flyover Morocco, Mwenge jijini Dar es Salaam zipo palepale

Dodoma. Fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za juu  katika maeneo ya Morocco na Mwenge, jijini Dar es Salaam, zinatarajiwa kupatikana kupitia mkopo kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica), ambapo mkataba wa mkopo huo unatarajiwa kusainiwa kabla ya Julai 2025.

Ujenzi wa barabara hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020–2025, inayolenga kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza makandarasi watakaochelewesha kukamilisha miradi ambayo Serikali tayari ina fedha zake kuwajibishwa kwa kutozwa fidia.

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega akizungumza baada ya kutembelea ujenzi wa barabara za mzunguko na Uwanja wa Kimataifa wa
Ndege wa Msalato jijini Dodoma. Picha na Sharon Sauwa

Wakati huohuo, majaribio ya ndege katika Uwanja wa Kimataifa wa Msalato, jijini Dodoma, yanatarajiwa kufanyika kabla ya Juni 30, 2025.

Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatano Mei 21, 2025 na Ulega, alipofanya ukaguzi wa ujenzi wa barabara za mzunguko pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, jijini Dodoma.

Ulega amesema amekuwa akipokea maswali kutoka kwa wananchi kuhusu maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo, ambazo ni miongoni mwa ahadi zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025.

“Tunakwenda kukamilisha hatua za kitaalamu kufikia mwezi wa saba tutakwenda kutafuta mkandarasi tukimpata Watanzania watashuhudia tukimkabidhi zile kazi,”amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Jephaison Nnko amesema mipango hiyo ipo na wanatarajia kupata mkopo kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA).

“Na tumeshapitia hadi katika ngazi ya wizara na sasa tupo kwenye ‘ku-finalise design’ (kukamilisha michoro) na tukishamaliza tutaingia katika taratibu zote za kuhakikisha tunaanza vizuri,”amesema.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo akizungumzia majaribio ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma. Picha na Sharon Sauwa

Naye Mkurugenzi wa Barabara wa Wizara ya Ujenzi, Aloyce Matei amesema walikuwa na kikao na Wizara ya Fedha kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo miwili.

“Tunataka hadi kufika Julai, 2025, fedha za mkopo ziwe zimeshasainiwa,”amesema.

Majaribio ya ndege

 Ulega ametoa onyo kwa mkandarasi kuhakikisha wanaongeza idadi wafanyakazi na kufanya kazi mchana na usiku ili ujenzi huo ukamilike kwa muda uliopangwa katika mkataba ambao ni Novemba 30 mwaka huu.

“Nimeagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Tanroads kufanya kazi kwa pamoja katika kumsimamia mkandarasi huyu kwa sababu tusiache upande mmoja. Tunachotaka kuona kama Watanzania mradi huu ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa,” amesema.

Amesema kuwa hawataongeza muda katika ujenzi huo ikiwa mkandarasi huyo atafanya uzembe watamdai fidia ya kuuchelewesha.

“Na natoa maelekezo kwa miradi yote wanapochelewa hasa katika ile miradi ambayo tuna uhakika kuwa tunazo fedha lazima tuwadai fidia wanapochelewa ni kama wale wa Dar es Salaam wa BRT (Mradi wa Mabasi yaendayo kwa Kazi), wote nimewaambia wawadai fidia hatuna kesi ya masuala ya fedha pale,”amesema.

Katika hatua nyingine Ulega amesema kuwa wamebaini wizi katika eneo hilo ikiwemo wa nyaya za uzio na kuwachukulia hatua waliohusika.

“Kwa maendeleo ya mbele huu uwanja utakuwa na fance (uzio) wa kilomita 41 ili kuufanya kuwa salama. Hakuna wanyama kuingia kwenye njia za kurukia na kutua ndege  na udokozi. Na hiyo fance itakuwa ya umeme,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu TAA, Abdul Mombokaleo amesema wanatarajia kuanza kufanya majaribio ya ndege kwenye uwanja huo kabla ya Juni 30, 2025.

Kuhusu madai ya wafanyakazi wanaojenga kufanya kazi kwa muda mrefu na kulipwa saa chache, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aliahidi kumwelekeza ofisa kazi kutoka ofisini kwake kwenda Jumatatu uwanjani hapo kwa ajili ya kuzungumza na wafanyakazi.

“Akija ofisa kazi huyo apewe nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi. Kuna mambo mengine kweli unaweza kukuta hayaendi sawasawa na utaratibu na mambo mengine pia wanatakiwa kuelimishwa,” amesema.

Februari 2020 Serikali na Benki ya Afrika (AfDB), walitiliana saini mkataba wa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo wenye thamani ya Dola za Marekani 329.29 milioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *