
TABORA United imeshaanza maisha mapya na kocha wao mpya, Genesis Mangombe na jamaa ameshashtukia mambo fasta ndani ya kikosi chake.
Mangombe ambaye ni raia wa Zimbabwe, ametua katika timu hiyo akichukua nafasi ya Mkongomani, Anicet Kiazayidi.
Mangombe ameliambia Mwanaspoti kuwa, ameridhishwa na ubora wa wachezaji wake baada ya kuwaona kwenye vipindi vitatu tofauti vya mazoezi.
Hata hivyo, kocha huyo alisema kitu cha kwanza ambacho anaanza nacho, ni kupandisha ufiti wa wachezaji akifichua kwamba kikosi chake kikienda hivyo kilivyo sasa kwenye mechi yoyote, wanaweza kupata shida.
“Ukiniuliza tutaanzia wapi nitakujibu tunatakiwa kupandisha ufiti wa wachezaji, tunatakiwa kuwa na kikosi chenye pumzi, stamina iliyo kwenye kiwango cha juu sana.
“Tumeshaanza kulifanyia kazi hilo kuanzia leo (jana Jumatatu) tulikuwa gym asubuhi na jioni tunarudi uwanjani kwa kuwa muda sio rafiki sana. “Tutakuwa na mchezo wa FA dhidi ya Kagera Sugar, ni lazima tutumie siku hizi chache kwa hesabu nzuri ili tuendelee kupata matokeo mazuri,” alisema kocha huyo.