Simiyu. Fisi 16 wameuliwa katika operesheni maalumu mkoani Simiyu iliyoanza Januari 25, 2025 ili kuhakikisha usalama wa wananchi katika maeneo ambayo wanyama hao walikuwa wanaleta madhara.
Hayo yemesemwa jana Jumatano Februari 19, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya operesheni hiyo iliyofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (Tawa), Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Jeshi la Polisi.

Askari wa Tawa wakiwa katika oparesheni maalumu ya kuvuna fisi
“Desemba 20, 2024 baada ya fisi kuvamia wananchi Serikali ilichukua hatua kubwa ya kushirikisha vyombo vyake (Tawa na Jeshi la Polisi) na kuanza oparesheni, lakini ilipofika tarehe 25/01/2025 oparesheni ya mkoa mzima ilifanyika kwa ukubwa kuhakikisha inakabiliana na fisi wote waliokuwa wanasumbua wananchi.
“Na Kwa taarifa njema ni kwamba tangu kuanza Kwa oparesheni hii vyombo vyetu vimeweza kudhibiti na kuua fisi 16 na ndio maana kwa sasa mnaweza kuona hali imetulia,” amesema Kihongosi.
Ofisa Habari wa Tawa, Beatus Maganja amewataka wananchi kuonyesha ushirikiano kwa maofisa wa uhifadhi ili kuongeza ufanisi wa zoezi hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi
Maganja pia amewataka wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kutembea nyakati za usiku na alfajiri kwani ni nyakati ambazo fisi huwa katika mawindo yao.
“Wananchi endeleeni kutoa ushirikiano kwa maofisa wa Jeshi la Uhifadhi waliopo uwandani ili kuongeza ufanisi wa zoezi hili, pia tambueni kuwa Serikali imedhamiria kulinda wananchi wake na askari wapo uwandani wanafanya Kazi usiku na mchana kuwahakikishia usalama wenu,”amesema Maganja.
Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Itilima wameshukuru kwa juhudi hizo za kuwapunguza fisi.

Ofisa Habari wa Tawa, Beatus Maganja
“Kwa kweli tulikuwa tunasumbuliwa sana na fisi ambao walikuwa wanajeruhi watu, baada ya Serikali kusikia ikaweka ulinzi, kwakweli imetufanyia vizuri sana mpaka leo hatujawasikia tena tangu askari waanze kuwapunguza fisi,” amesema Mozo Mabula mkazi wa Kijiji cha Mwamunhu kilichopo Wilaya ya Itilima.