Ukiongelea historia ya Tanzania, siyo rahisi kuacha kuutaja mji wa Bagamoyo ambayo imekuwa ikitokea katika maeneo mengi ya hasa biashara ya utumwa.
Miaka hiyo wakazi wa mji wa Bagamoyo ambao hadi leo hii umekuwa ukitembelewa na wageni mbalimbali kwa shughuli za kitalii, kazi yao ukubwa ilikuwa uvuvi na kilimo kwa mujibu wa historia.
Lakini Bagamoyo ya sasa imekuwa ya tofauti hasa katika upande wa mchezo wa ngumi kutokana na vijana wake kuweka rekodi tofauti katika mchezo huo ambao kwa sasa ni wa pili kwa ukubwa nchini.
Nuru na rekodi ya mapema ilianza kuonekana kwa bondia Maono Ally kwa kuwa Mtanzania wa kwanza na bondia wa kwanza nchini kushinda mkanda wa Ubingwa wa Baraza la Ngumi Duniani upande wa vijana ‘WBC Youth’ kwa kumchapa Technical Knockout ya raundi ya pili katika pambano la raundi Luka Pupek wa Croatia ambalo lilifanyika Afrika Kusini, mwaka 2018.
Bahati iliendelea kuwa upande wa Bagamoyo chini ya kijana Bruno Tarimo ambaye kwa sasa amepata nafasi ya kuishi nchi Australia kwa mara ya kwanza kushinda mkanda wa ubingwa wa WBA Asia Pasific mwaka 2018 kwa kumchapa kwa pointi Billel Dib wa Australia.
Lakini sasa ukiongelea Bagamoyo katika mchezo wa ngumi basi jina la kijana Firiki Salum huwezi kuliacha kwani ndiye bondia pekee kutokea ukanda huo wenye ufukwe wa bahari ya Hindi kuendelea kuwepo kwenye orodha ya mabondia kumi bora 2024/2025 akiwa kwenye nafasi ya tisa mwaka jana na mwaka huu ameshuka hadi nafasi ya kumi.
Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 14 akiwa ameshinda mapambano 12 kati ya hayo 11 kwa Knockout, amepoteza pambano mwaka jana ambalo ilikuwa ni Pakistan huku ndani akitoka sare moja.

Fikiri kwenye uzani wake wa super light, ndiye bondia namba moja katika mabondia 81 wa uzani huo nchi nzima, duniani akiwa wa 132 katika mabondia 2555.
Kwa mujibu wa mtandao boxrec, Fikiri aliyeanza ngumi mwaka 2019, amepewa asilimia 91 za kushinda kwa Knockout akitumia mtindo wa southpaw katika mapambano yake ulingoni.
Gazeti la Mwananchi limefanya mahojiano maalum na bondia huyo ambaye amekuwa na ndoto kubwa ya kushinda mikanda mikubwa ya ubingwa duniani kama ilivyokuwa kwa mabondia wengine wenye majina.
Fikiri anasilimulia kuwa kabla ya kuingia kwenye mchezo wa ngumi kazi yake kubwa ilikuwa ni shughuli za uvuvi katika pwani ya fukwe za Bagamoyo ambayo vijana wengi wazawa wamekuwa wakiifanya.
“Kabla ya kuwa bondia, nilikuwa mvuvi lakini mwenyewe ndiyo niliamua kuacha na kuanza kufanya mazoezi ya ngumi ufukweni.
“Kazi yangu ilikuwa ni kutoka nyumbani asubuhi hadi ufukweni kufanya mazoezi ya ngumi mwenyewe, hali hiyo ikaja kupelekea nionekane chizi kutokana na muda mwingi kuwepo ufukweni.
“Kiukweli watu wengi walijua kwamba nimekuwa kichaa, kukaa kwangu ilikuwa kwenye vichaka vya ufukweni nikiwa vifaa vyangu nilivyotengeneza mwenyewe kwa ajili ya kupigania.
Uliwezaje kwenda kuwa bondia rasmi?
“Binafsi namshukuru kocha wangu, Sharif Muhusini wa Sharifu Boxing Gym yeye akiwa na bondia mwengine Rehema Abdallah ndiyo waliokuja kunichukua na kunupeleka kwenye gym yao.
“Unajua ile stori ya kuwa kuna bondia chizi anafanya mazoezi ya ufukweni iliwafikia ndiyo sababu yakuja kuniona, walivyofika waliniuliza kama najua kupigana, nikawaambia naweza, Rehema akatolea kunijaribu, akanipiga.
“Lakini haikuzuia wao kunichukua,nikaenda kujiunga kwenye gym yao, nilifanya nao mazoezi, tatizo ilikuwa kuelewa lakini baadaye nikaanza kupewa mapambano, mwaka 2019, nilishinda pambano la kwanza lakini nilifukuzwa gym.
“Kilichopelekea hadi nifukuzwe nilikuwa nafanya tofauti na maelekezo ambayo nilikuwa napewa, lakini baada ya kwenda kuomba msamaha nikarudishwa tena gym nikawa naendelea na mazoezi.
“Nikapewa nafasi nyengine lakini niliambiwa ndiyo nafasi ya mwisho ila nilivyopewa mechi ikawa yaleyale, nikafukuzwa ikabidi niongee na familia ambayo nikaenda nayo kuomba msamaha.
“Nashukuru baada ya hapo kila kitu kimekuwa historia upande wangu, nimefikia nyota mbili na nusu, sijawahi kupigwa hapa ndani katika pambano lolote hivyo nashukuru Mungu kuona naendelea kupiga hatua katika mchezo huu.
Unazungumziaje kuwa kwenye kumi bora ya mabondia wa Tanzania?
“Binafsi kwanza nashukuru Mungu pamoja na uongozi wangu wa Sharif Boxing ambao kwa kuweza kunifikisha hapa lakini ukiangalia siyo jambo rahisi kupenya katika orodha ya mabondia wenyewe viwango vikubwa hadi kuwa hapo nilipo.
“Ukiangalia siyo bondia najulikana sana kwa sababu pengine sipati mapambano makubwa kama wengine lakini juhudi na nidham imekuwa sababu kubwa ya kuwa kwenye nafasi hiyo ya kumi bora kwangu ni hatua kubwa ingawa bado sijafika mwisho,” anasema Fikiri.