Kitendo cha mwisho cha upinzani alichoonyesha kiongozi wa Hamas Shahidi Yahya Sinwar, kilichonaswa na kamera ya ndege isiyo na rubani ya jeshi la utawala wa Kizayuni na kurushwa hewani duniani kote, kimeibua msemo mpya wa lugha ya Kiarabu wenye maana ya ‘ukinzani’ na kuashiria moyo usiotetereka wa Wapalestina wa kupambana hadi pumzi ya mwisho.
Ingawa haijulikani ni nani aliyetumia msemo huo kwa mara ya kwanza lakini “Asaa al Sinwar” – kwa Kiarabu “Fimbo ya Sinwar” – sasa imekuwa kilio cha watumiaji wa mitandao ya kijamii tangu kiongozi huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas aliponaswa kwenye kamera kabla ya kifo chake, akiirushia fimbo ndege isiyo na rubani ya jeshi la Kizayuni ndani ya jengo lililobomolewa huko Ghaza.
Tangu wakati huo, kitendo hicho cha Shahidi Sinwar kimekuwa sitiari yenye nguvu ya Muqawama kwa Wapalestina huko Ghaza na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu ambapo wamekuwa wakikabiliwa na vita vya kinyama na kikatili vya utawala ghasibu wa Israel tangu Oktoba 7, 2023.
“Alikufa kishujaa, akishambulia bila kukimbia, akiwa ameshika bunduki yake, na kukabiliana na jeshi la uvamizi kwenye mstari wa mbele,” ilieleza harakati ya Hamas katika taarifa iliyotoa mapema mwezi huu kuthibitisha kuuawa shahidi kwa kamanda huyo wa Muqawama.

Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wameshiriki kutoa maelezo sawa na hayo kuelezea kitendo cha mwisho cha kiongozi huyo wa Hamas na kuufasiri msemo Fimbo ya Sinwar kwa kusema:
“ ‘Nilirusha fimbo ya Sinwar’ inamaanisha kuwa nimejaribu kutumia kila njia na sikubakiwa na chochote kingine zaidi ya fimbo”.
Wengine wakasema: “‘Nilirusha fimbo ya Sinwar’ ikimaanisha, ulitumia silaha ya mwisho uliyonayo baada ya kumaliza juhudi zako zote kufikia malengo yako.”
Zafarul-Islam Khan, mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Jamii ya Wachache ya Delhi nchini India amesema, “Walidhani amekufa, na pamoja naye, imekufa pia Harakati ya Uhuru wa Palestina. Lakini ndani ya siku chache za kuuawa kwake, Sinwar amekuwa ngano. Methali mpya ya Kiarabu imetungwa hivi punde: “Nilimpiga kwa fimbo ya Sinwar”, ikimaanisha, nilipigana naye kwa nguvu zangu zote hadi pumzi ya mwisho”.
Mtumiaji mwingine wa mitandao ya kijamii, Tariq Mehmood, amesema, “Fimbo ya Sinwar ina nguvu zaidi kuliko Tembeo ya David, inafyatua kutoka kwenye mioyo ya mamilioni”. Tembeo ya David ni mojawapo ya mitambo kadhaa ya ulinzi wa makombora inayotumiwa na Israel.
Wataalamu wa masuala ya usalama wamesema jeshi la utawala wa Kizayuni lilifanya makosa kwa kusambaza video ya lahadha za mwisho za uhai wa Sinwar, kwa sababu imemtengenezea taji kiongozi huyo wa Muqawama wa Palestina…/