Fei Toto ataja ishu ya kubusu miguu

Kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ni mmoja ya wachezaji waliobahatika kubusiwa miguu uwanjani tangu akiwa Yanga na hata sasa akiwa na Azam, huku akisema hata yeye anaweza kuwabusu wachezaji wenzake ikitokea kitu cha kumlazimisha kufanya hivyo.

Fei Toto aliwahi kubusiwa miguu yake ya msemaji wa zamani wa Simba na Yanga, Haji Manara na juzi kati aliofanyiwa tena na Gibril Sillah baada ya kufunga moja ya mabao yaliyoipa Azam ushindi katika Ligi Kuu Bara.

Akizungumzia matukio hayo alisema kwake ni heshima, lakini hata yeye kuna siku atafanya kwa yeyote kulingana na tukio litakalotokea siku husika.

Agosti 29, 2021, Manara wakati anatambulisha kikosi cha cha msimu cha Yanga, zamu ya Fei Toto alianza kwa kumfunga kamba za kiatu kisha akaubusu mguu wake, tukio hilo limejirudia Februari 6,2025  Azam FC  iliposhinda mabao 2-0 dhidi ya KMC, Sillah baada ya kupewa pasi ya bao la pili na Fei Toto alikwenda kuubusu mguu wake.

Msimu wa 2021/22, ambao  Manara aliubusu  mguu wa Fei Toto alimaliza na asisti nne, tofauti na misimu mingine ya nyuma ambayo hakuwa na asisti isipokuwa alikuwa anafunga mabao.

“Kuubusu mguu wa mchezaji inatokana na matukio husika, mfano Sillah nilipompa pasi ya bao la pili dhidi ya KMC, alifurahia na aliniambia amependa nilichokifanya, hivyo uwanjani mtu akifurahia kinaweza kikatokea chochote,” alisema Fei Toto na kuongeza;

“Kwa upande wangu ninaweza nikaubusu mguu wa mchezaji yeyote kulingana na matukio, hivyo siwezi kumchagua ni nani kwa sababu bado haijatokea ama siwezi nikasema nitaubusu mguu wa Lionel Messi nitakuwa nadanganya maana hakuna tukio la kutukutanisha.”

Fei Toto ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao 19 na sasa ana mabao manne na asisti 10 alisema Tanzania kuna wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa ambao anaweza akaibusu miguu yao, hivyo anaona  ni suala la muda kufanya hivyo.

Sillah ambaye anamiliki mabao matano na msimu uliopita alimaliza na manane alisema aliubusu mguu wa Fei Toto kwa sababu ni kati ya wachezaji wa Kitanzania ambao wana kipaji kikubwa.

“Fei Toto ni mchezaji mkubwa, ana uwezo wa kuichezesha timu na kuamua mechi, hivyo sikukosea kuubusu mguu wake ni kitu ambacho nilikifurahia na kujivunia kukutana na mchezaji wa aina yake na kucheza naye pamoja,” alisema Sillah.