Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitunukiwa tuzo ya Gates Foundation Goalkeepers kutokana na kazi kubwa anayofanya katika kupunguza utapiamlo, kuimarisha afya ya wananchi na kuendeleza afya na lishe ya mama, watoto na vijana.
Tuzo hii inaonyesha maendeleo ya Tanzania katika kukabiliana na utapiamlo na kuboresha afya chini ya uongozi wake.
Akizungumza katika hafla ya tuzo hizo Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza dhamira yake ya kuimarisha programu za afya na lishe, akisisitiza urutubishaji wa chakula kama mkakati muhimu.
Shirika la Feed the Children kama moja ya wadau muhimu katika masuala ya lishe nchini limekuwa likiunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa wazazi wa watoto chini ya miaka mitano, wakina mama walio katika umri wa kupata watoto na jamii nzima kwa ujumla.
Hii inahusisha elimu ya namna bora ya kuandaa chakula chenye virutubisho muhimu na kulima vyakula vilivyoongezwa virutubisho kibaolojia kama vile mahindi na viazi lishe.
Elimu ya afya hutolewa kama vile umuhimu wa chanjo kwa watoto, masuala ya usafi wa mazingira kwa kushirikiana na watoa huduma wa afya ngazi ya jamii. Hii inasaidia kupunguza athari za magonjwa yanayotokana na lishe duni na kuongeza ufahamu kuhusu lishe bora.
Pia Feed the Children inashirikiana na shule kupitia kamati za shule kutoa hamasa kwa wazazi ili kuweza kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora na chenye lishe bora kwa wanafunzi.

Wakina mama wenye watoto wadogo chini ya miaka mitano wakipata elimu ya lishe kutoka kwa muhamasihaji kutoka Feed the Children.
Hii si tu inasaidia kupunguza njaa na kuboresha afya zao, bali pia inasaidia kuboresha utendaji wa wanafunzi shuleni, kwa sababu watoto wanapata nguvu na uwezo wa kujifunza.
Miradi inayotekelezwa na Feed the Children ambayo inahusisha masuala ya lishe
Kupitia nguzo/idara za Lishe na chakula na afya na maji, Feed the Children inatekeleza mradi ambao unatoa mafunzo kuhusu lishe bora na umuhimu wa ulaji wa vyakula vyenye virutubisho kwa wazazi/ walezi wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili kusaidia katika ukuaji na maendeleo yao.
Pia elimu ya masuala ya lishe hutolewa kwa wanawake walio katika umri wa uzazi (miaka 18 – 49) ambapo mpaka sasa tumefikia wakina mama zaidi ya 1,500.
Kupitia shule za msingi 18, FEED imekuwa ikitoa elimu kwa wanafunzi kuhusu masuala ya lishe bora na ulaji unaofaa (kuzingatia mlo kamili) ili kuweza kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuzingatia wanachokula na sio kujaza tumbo.
Aidha, shirika linashirikiana na familia katika kupanga mikakati ya kujikimu kiuchumi, kama vile kilimo endelevu, ili kuwasaidia kupata rasilimali za kutosha kwa ajili ya mahitaji yao ya kila siku ya familia ikiwemo chakula bora.
Jamii na watoto ambao wamefikiwa na miradi ya Feed the Children
Mpaka sasa Feed the Children inafanya shughuli zake katika mikoa ya Pwani na Morogoro. Shirika limewafikia wanafunzi 22,516 wa shule za msingi na zaidi ya wazazi/walezi wenye watoto chini ya miaka mitano 1,500.
Ushirikiano wa Feed the Children na Serikali na jamii katika utekelezaji wa shughuli zake
Feed the Children imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali kuanzia ngazi ya Mkoa mpaka ngazi ya kijiji. Kupitia vikao vya kutathimini utekelezaji wa shughuli zetu katika mikoa husika pamoja na halmashaurii kupitia idara ya maendeleo ya jamii ili kujadili mafanikio na changamoto ambazo zinaweza zikawa zimejitokeza.
Viongozi wa jamii wanahusika moja kwa moja katika upangaji na usimamizi wa shughuli za shirika, jambo linalosaidia kuongeza ufanisi na ushirikiano wa jamii nzima.
Aidha, shirika limekuwa likiwashirikisha wazazi na walezi kupitia mikutano ya vijiji na vikao vya wazi, ambavyo vinatoa fursa ya kujadili utekelezaji wa miradi kwa pamoja. Pia, watu maarufu na wenye ushawishi katika vijiji wanatumika kama mabalozi wa kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za shirika.
Mafanikio ambayo Feed the Children inajivunia katika kuunga mkono upatikanaji wa lishe bora
Shirika la Feed the Children limejitolea kwa dhati kuboresha lishe bora katika shule za msingi. Kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, tuliwezesha shule 28 katika Wilaya ya Kisarawe kwa kuwapatia watoto unga wenye virutubisho na sukari kwa ajili ya kifungua kinywa cha asubuhi.

Mmoja wa wanufaika wa mbegu za viazi lishe, Zainabu Salumu akionyesha kiazi baada ya kulima katika kijiji cha Msonge wilayani Morogoro.
Pia, wazazi walihamasishwa kuhusu umuhimu wa kuchangia utoaji wa chakula shuleni ili kuwepo na uendelevu wa huduma hiyo, kwani utoaji wa chakula mashuleni huchangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa mahudhurio na ufaulu wa wanafunzi katika shule zilizoshiriki kwenye mradi huu.
Kwa sasa, shirika linaendelea na juhudi hizi katika Wilaya ya Morogoro kwa kuhamasisha wazazi kuhusu umuhimu wa chakula mashuleni na kutoa msaada wa vifaa muhimu vinavyosaidia upatikanaji wa lishe bora kwa watoto shuleni.
Aidha, shirika limekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya lishe na afya kwa wazazi wenye watoto walio na umri chini ya miaka mitano, ili kuhakikisha watoto wanapata msingi mzuri wa lishe tangu kipindi cha ujauzito hadi wanapoanza shule.
Kupitia vilabu vya lishe na afya, shirika hutoa maarifa muhimu yanayosaidia jamii kuwa na uelewa mpana kuhusu lishe na afya, hivyo kuchochea mabadiliko chanya kwa ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa mwaka 2024 shirika liliwapatia mbegu za viazi lishe 140,000 wakina mama wenye watoto chini ya miaka mitano zaidi ya 1,000 na mahindi lishe ili kuweza kusaidia upatikanaji wa chakula chenye afya na lishe bora katika wilaya ya Morogoro.
Changamoto na mikakati
Katika utekelezaji wa shughuli za shirika ili kuhakikisha watoto wanapata chakula na lishe bora, huwa kunakuwepo na changamoto mbalimbali zikiwemo uchache wa rasilimali fedha, jambo ambalo hupunguza uwezo wa kuwafikia watu na jamii nyingi katika maeneo ya mradi.
Wazazi na jamii kukosa uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa watoto na namna nzuri ya uandaaji wa chakula kwa watoto hii inasababishwa na wazazi wenyewe kutumia mifano ya maisha ya nyuma.
Mabadiliko ya hali ya hewa huwa yanaathiri uzalishaji wa chakula na kupelekea upungufu wa chakula kwenye familia na jamii kwa ujumla.
Sera za Serikali zinaweza kutokidhi mahitaji au kuzuia upatikanaji wa chakula kwa watoto mfano sera ya elimu bila malipo ilivyoanza utekelezaji wake ilipelekea afua ya utoaji chakula mashuleni kusuasua kwani wazazi walijua sera ile imekataza utoaji wa michango mashuleni kwa ajili upatikanaji wa chakula.