Dar es Salaam. Familia ya Tundu Lissu imewataka wabaya wake kumsikiliza kwa umakini hoja anazopigania za uhuru wa kweli Tanzania.
Licha ya familia hiyo kusema inamuunga mkono katika harakati zake, imesisitiza itakuwa ya kwanza kumkosoa na kumrudi pale atakaporudi nyuma kwenye kupigania haki kwa kutekwa na ‘machawa.’
Hayo yamesemwa leo Jumapili, Februari 16, 2025, katika misa ya shukrani iliyofanyika Kigango cha Mahambe, wilayani Ikungi, Mkoa wa Singida, na kuongozwa na Padri Francis Lyimo, Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida.

Mahambe ni sehemu ambapo Tundu Lissu alizaliwa. Misa hiyo imefanyika kama shukurani na kumwombea katika majukumu yake mapya ya uenyekiti baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema Januari 21 hadi 22, 2025 kumchagua kuwa Mwenyekiti.
Katika uchaguzi huo, Lissu aliibuka na ushindi wa kura 513, sawa na asilimia 51.5, dhidi ya Freeman Mbowe aliyekuwa anatetea nafasi hiyo aliyoiongoza kwa miaka 21, akipata kura 482, sawa na asilimia 48.3, huku Charles Odero akipata kura moja. Kura zilizopigwa zilikuwa 999, halali zikiwa 996 na tatu ziliharibika. Mbowe alikubali matokeo na aliwataka wanachama wa chama hicho kuwaunga mkono na kuwapa ushirikiano viongozi wapya waliochaguliwa.
Jana, Jumamosi, Februari 15, 2025, Lissu alirejea nyumbani kwao na kufanya mkutano wa hadhara Ikungi ikiwa na shughuli ya kichama. Leo Jumapili, Lissu akiwa na viongozi wa chama pamoja na familia yake, akiwemo kaka mkubwa Alute Mughwai na Vincent Mughwai, mdogo wa Lissu, walikuwapo, baada ya misa kumalizika, familia na wageni mbalimbali walipata fursa ya kutoa salamu za shukrani mbele ya mamia ya waumini kanisani, kisha walikwenda kwenye boma la Mzee Mughwai kwa shughuli za kifamilia.
‘Maswali kwa wabaya wa Lissu’
Katika maelezo yake, Alute ambaye kitaalamu ni wakili amesema pamoja na mambo yote wanamuombea kwa Mungu apate nguvu na morali katika kuijenga Tanzania bora kwa kuwa na jamii inayojengwa katika misingi ya uhuru, demokrasia na haki.
“Familia na ukoo tutaendelea kukuunga mkono kwenye juhudi zako hizi, na tutakuwa wa kwanza kukukosoa na kukurudi pale ambapo utaacha kupigania misingi hii ambayo nimesema awali, kukubali kutekwa na ‘machawa,’ kulewa madaraka. Ukifanya hivyo tutakurudi na tutakuwa wa kwanza,” amesema wakili Alute.
Amesema amani ni tunda la haki, kwani haki na amani vinahusiana, na mara nyingi baadhi ya viongozi Tanzania wanakosolewa kwa kuhubiri habari ya amani zaidi kuliko haki. “Haki lazima itangulie, halafu amani itafuata,” amesema.
Wakili Alute ameendelea kusema kwamba wabaya wa Lissu wataendelea kusema kuwa Lissu ni mtu asiyekuwa na heshima kwa wengine, mgomvi, mkorofi, na kwa hivyo asisikilizwe katika harakati zake za kupigania uhuru, ulinzi wa raslimali asili, ardhi, madini, mito, wanyama, bandari, na ndege.
“Wapinzani wako (Lissu) watauliza Mahambe wameona kitu gani kiasi cha kumfanyia sherehe hii mtu huyu anayejifanya mkorofi, Jasiri, mjuaji na ukoo tuna tabasamu hivi,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu akiwa na ndugu zake nyumbani kwao Singida
Wakili Alute amesema kwa kuwa familia hiyo wanamfahamu Lissu vizuri, anaamini kama wangesikiliza kwa makini mambo anayopigania, wangeshajua ni kwanini wanakijiji cha Mahambe wanampenda kwa dhati na kumpatia heshima hiyo.
Alute amesema familia yao imejaaliwa kuwa na padri, sista, na mchungaji, huku Paroko wa Parokia ya Ikungi, Vicent Alute, akimtaka Lissu kuendelea kumtegemea Mungu katika kutekeleza shughuli zake.
Alichokisema Paroko
“Mungu hawaachi watu wanaomcha. Tundu, endelea kumtegemea Mungu, endelea hivyo baba, Mungu anakusudi na wewe na kama ilivyo kila mmoja ameletwa duniani kwa maskudi na amebeba ujumbe wa Mungu,” amesema Paroko Vicent.
Paroko Vicent amesema ni muhimu kutenda haki na ndugu kuendelea kuishi pamoja kwa upendo, huku akitahadharisha kuendekeza suala la ubinafsi, kwani litawamaliza.
“Tutende haki, ubinafsi ni kitu kibaya na utatumaliza. Upendo aliotupatia Mungu inapendeza ndugu kukaa pamoja. Mahali pengine ni vita, mitutu, unasikia mirindimo ya risasi, lakini sisi tunamuabudu Mungu katika hali ya amani na utulivu. Je, tumechoka utulivu na amani?” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Iringa, Fenk Nyalusi, amesema hawajafika walipo kwa bahati mbaya, kwani ushindi wa Lissu katika uchaguzi ulikuwa unahitajika na Watanzania wote. “Viongozi wa dini mlioko hapa tusaidieni namna ya kukemea hao wanaodhurumu haki za watu ili kazi ya Lissu iweze kuheshimisha nchi yetu,” amesema.

Ushauri wa Bavicha
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Deogratias Mahinyila, amesema yakitokea mashindano yeyote au uchaguzi, lazima yatokee makundi mawili ya walioshinda na walioshindwa.
“Nawaombeni watulikuwa wanamuunga mkono Lissu, kanuni za asili zinawataka walioshinda kuwa na busara zaidi kuliko walioshindwa. Tulioshinda busara yetu iwe juu, kulinda chama chetu,” amesema Mahinyila.
Mahinyila amesema walioshinda waache maneno maneno, wakiendelee walishindwa watakuwa na vidonda: “Walioshindwa nawao kama wanavidonda wanyamaze, wakisema sema tulioshinda si wanyonge.”
Amesema ni wakati wa wote kuungana kuwa kitu kimoja kuhakikisha wanaendeleza mapambano ya kudai na kupata katiba mpya na Tume huru ya Uchaguzi.

Alichokisema Lissu
Akiwa mzungumzaji wa mwisho, Lissu amewashukuru wanakijiji wa Mahambe, akiwaambia wageni na wana-Chadema waliosindikiza kwamba hakuzaliwa sehemu ya ajabu. Mbele kulipofanyika Misa kuna mabakuri ya babu, baba yao na ndugu wengine.
“Karibuni Mahambe, hiki kijiji kina historia kubwa, na nafikiri kina miaka takribani 300. Kimepita mapito mengi. Nikiwa na miaka sita, nilishuhudia nyumba zikibomolewa na kubaki tano tu kwa amri ya serikali,” amesema.
Lissu aliongeza kuwa watu wa Mahambe ni wema na kwamba ujasiri wake unatokana na asili ya wazazi wake.
“Kama nilivyo mwenyewe na kama mimi ni wakorofi ni kwa sababu watu wa Mahambe ni wakorofi, walikataa kuhama kwenye operesheni Vijiji na kwanini nimesoma hawa wazee waliopo hapa mmoja wao alitoa nyumba yake ya tembe ili iwe shule,” amesema.
Amesema baada ya kutolewa nyumba hiyo na yeye (Lissu) alianza darasa la kwanza huku akisema alikuwa kinara wa uchelewaji kuwahi shuleni na alikuwa anashindana na wenzake kupigwa viboo vya uchelewaji.
“Hapa kwetu pana historia nzuri, hii hadithi ya kijiji kidogo hiki na mambo yake makubwa inatuambia jinsi ambayo sisi binadamu na karama tunazopewa na Mungu tunaweza kufanya mambo ya ajabu pamoja na kutokea kwenye mazingira ya kawaida kama haya ya Mahambe,” amesema.
Amesema watu wengi wamekwenda kwenye kijiji cha Mahambe ni kwa sababu Mwenyekiti wa Chadema (Lissu) amezaliwa sehemu hiyo na hata ujasiri wake unatokana na asili ya wazazi wake.
“Siku ya leo ilikuwa ya watu wa Mahambe na mtoto wao, na wageni wao, mimi ni mtoto wa Mahambe, Wanachadema wote kote mlikotoka hii habari ilianzia hapa, huu ni udongo ulionizaa, hawa watu wa Mahambe ndio walinizaa,” amesema Lissu mwenye miaka 57.
Sheikh amwombea Lissu
Sheikh Dulle Ntandu, akimtumaini Lissu kwa kumwombea, amesema wachawi, wanafiki, na wenye kutuma mapepo iwe mwisho kwao.
“Mungu mbariki Lissu na mnyanyue ili aweze kutimiza malengo yake na nchi iwe na haki na baadaye amani,” amesema.
Awali, Askofu Maximilian Machumu, maarufu Mwanamapinduzi alisema anamuunga mkono Lissu kwa sababu anakipigania kile anachokiamini na siku akiacha ataungana na familia kumkemea.
“Kumuambia hakuwa hivi tangu mwanzo, ulituvuta, ukatushawishi kukuelewa kwa misimamo yako, utendaji wako wa haki na kupigania haki za wengine badala ya zile za kwako,” amesema.
Amesema nafasi hiyo ameipata baada ya minyukano mingi na ilikuwa haki yake kumshukuru Mungu, angeendelea na kazi bila kushukuru angemshangaa. Mwanamapinduzi alitumia fursa hiyo naye kumwombea kwa kumwekea mikono akiwa na Rose Masesa ambaye ni dada yake Lissu.
Rose ambaye ni mchungaji akitoa huduma ya kiroho Songea, Mkoa wa Ruvuma amesema Lissu ni mtu mwenye haki, kwakuwa anatetea haki ndiyo maana Mungu amtetea na kufika hadi sasa.
“Mungu si dhalimu anachukizwa na maovu, dhuluma, ufisadi na rushwa inayopovusha watawala na pasipo haki Taifa linaangamia, Mungu akubariki Lissu, umeahidi kukutete haki na demokrasia na maombi yote haya yakawe mafuta na uinuke ukaitende,” amesema.