Familia ya kada wa CCM aliyetekwa ‘yamwangukia’ Rais Samia

Mwanza. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza likieleza kutokuwa na taarifa zozote kuhusu alipo mjumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chonchorio maarufu kama Chox, familia ya kada huyo imesema imeanza kuonja machungu ya kutoweka kwa ndugu yao huku wakituma ujumbe kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Jana Ijumaa, Machi 28, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa jeshi hilo hadi sasa halijui alipo kada huyo wa CCM, huku akiomba umma ama mtu yoyote mwenye taarifa itakayosaidia kupatikana kwake atoe taarifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Machi 29, 2025, msemaji wa familia ya Chonchorio, Lucy Mdimi amesema maisha ya familia ya kada huyo yameanza kutetereka kutokana na kutoweka kwake.

“Kama tunavyojua, baba wa familia akiondoka hatujui tutakulaje, hatujui watoto watasomaje, kumbuka watoto wake wengine wako nje wanasoma. Atakayebeba huo mzigo ni nani, kumbuka kwetu tuna hakohako katoto ka kiume (Chonchorio) ambako kamekuwa nguzo ya familia,” amesema Lucy.

Lucy amemuomba Rais Samia kuingilia kati suala hilo na kutoa maelekezo ili ndugu yao apatikane na kuendeleza majukumu yake kwenye familia yake.

“Familia tunajiuliza kama mama yetu Rais Samia asipoingilia kati, hatuna mtu mwingine wa kusomesha watoto hawa,” amesema.

Alivyotoweka

Kwa mujibu wa Lucy, mdogo wake (Chonchorio) ambaye pia ni mfanyabiashara, aliondoka nyumbani kwake Mtaa wa Temeke, Kata ya Nyakato jijini Mwanza, saa 2 asubuhi Machi 23, 2025.

Ilipofika saa 5:00 asubuhi akiwa hajarudi, familia yake walianza kumtafuta kwenye simu zake ambazo hazikupatikana ndipo walipoenda kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Nyakato.

Msemaji wa Familia ya Kada wa CCM, Daniel Chonchorio, Lucy Mdimi akizungumza na vyombo vya habari leo.

“Polisi walikuja kupekua hapa nyumbani baadaye shuhuda mmoja aliyemuona kabla, akasema alimuona akiongea na simu wakati anafanya mazoezi, ndipo watu wanne wakamzunguka, baadaye ikatokea gari aina ya Land Cruiser ikamchukua na kuondoka naye, hakurudi tena mpaka sasa,” amesema Lucy.

“Aliyeshuhudia siyo mwanafamilia, lakini tulitoka kwa majirani kufuatilia kujua pengine kama wamebaini chochote kuhusiana na ndugu yetu, ndipo tukaambiwa hivyo,” amesema.

Kiongozi wa dini

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ameitaka jamii kutenda kila jambo kwa hofu ya Mungu kwa kile alichodai mtu mwenye hofu ya Mungu ndani hawezi kuwa na uthubutu wa kumteka binadamu mwenzake.

Sheikh Kabeke amewataka viongozi wa dini kwenye jamii kutumia mafundisho ya kwa kujikita kufundisha waumini masuala yanayoendana na matukio yanayotokea katika jamii ya sasa ikiwemo uhalifu na matukio ya utekaji.

“Naitaka jamii kuishi kwa kumhofia Mungu na kuamini kwamba ipo siku utaondoka duniani,” amesema Sheikh Kabeke.

Askofu wa Kanisa la International Evangelical Tanzania, David Mabushi amesema kutokea kwa matukio ya utekaji ni ishara ya uwepo wa roho ya uasi katika jamii.

Mkazi wa Pansiasi Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Jackline Sospeter amesema tukio hilo linashtua huku akiliomba Jeshi la Polisi kuendeleza jitihada zake za kuhakikisha wanaotekwa wanapatikana na kushughulikiwa.

“Tumekuwa tukishuhudia matukio mengi ya watu kutekwa yakiripotiwa maeneo mbalimbali nchini, wakati umefika wa Serikali na mamlaka za ulinzi kuimarisha intelijensia yao na kuyakomesha ili kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya kuishi kama ambavyo tunasifika kuwa kisiwa cha amani,” amesema Jackline.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *