Nairobi. Familia ya Paul Mutongori, ambaye amekamatwa akituhumiwa kuhusika katika tukio la kurushiwa kiatu kwa Rais wa Kenya, William Ruto, imeamua kuomba msamaha na kuiomba radhi rasmi Serikali ya Kenya.
Tukio hilo lilitokea Jumapili, Mei 4, 2025, katika siku ya tatu ya ziara ya Rais Ruto katika Kaunti ya Migori, magharibi mwa nchi hiyo.
Wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kehancha, kiatu kilirushwa kutoka kwa mmoja wa waliokuwapo kusikiliza hotuba ya Rais, na kumfikia kwenye mkono wake wa kushoto.
Kipande kifupi cha video kilichosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kinaonyesha tukio hilo, ambapo kiatu hicho kinamfikia Rais Ruto akiwa juu ya gari akihutubia wananchi.

Familia ya Mutongori kwenye taarifa yao imelaani tukio hilo na kusisitiza kuwa kitendo hicho hakikuwakilisha msimamo wala maadili ya familia yao.
Wameomba msamaha kwa Rais Ruto, Serikali na wananchi kwa ujumla, huku wakiomba uchunguzi ufanyike kwa haki na kwa kuzingatia hali ya kihisia ya mtuhumiwa.
Kikosi cha usalama wa Rais Ruto kilichukua hatua za haraka kumlinda baada ya tukio la kurushiwa kiatu, ingawa tayari kilikuwa kimempiga mkononi.
Rais Ruto licha ya kurushiwa kiatu hicho, aliendelea kuhutubia wananchi hao akielezea juhudi za Serikali yake za kupunguza gharama ya pembejeo kwa wakulima wa eneo la Kehancha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Tuko News, familia ya Paul Mutongori kutoka Kaunti ya Migori imejitokeza kwa mara ya kwanza mwishoni mwa juma na kueleza masikitiko yao kuhusiana na tukio hilo.
Mutongori ni mmoja wa watu watatu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwa sasa bado anazuiliwa na vyombo vya usalama.
Familia hiyo sasa inatoa wito kwa Rais Ruto aweze kuonyesha huruma na kuangalia uwezekano wa kumwachilia huru, wakisisitiza kuwa kitendo hicho hakikuwa na nia ya kisiasa bali kilichochewa na msukumo wa hasira na hali ya kihisia.
Wakizungumza na NTV, wanafamilia ya Mutongori, wameiomba msamaha Serikali kwa niaba ya mtoto wao aliyehusishwa na tukio hilo ambaye mikononi mwa vyombo vya usalama wakiomba asamehewe.
Mama wa Mutongori amesema amemlea mwanaye huyo kwa nidhamu kubwa na ameshangaa, kushtuka na kuingiwa hofu kwa sababu bado yuko chini ya ulinzi wa polisi.
“Nilimuuliza mmoja wa vijana waliokuwa hapa kuhusu aliko mwanangu, nikajua kwamba alikuwa amekamatwa. Nilishtuka kwa sababu nimekuwa nikiwaadhibu watoto wangu kila wakati.
“Namuomba Rais Ruto amsamehe kama vile baba anavyomsamehe mtoto wa kiume aliyemkosea,” amesema.
Familia hiyo imesema Mutongori ni mtu mtulivu asiyekuwa mbishi na mwenye heshima katika jamii. “Hata ukiuliza watakuambia ana heshima kwa kila mtu katika jamii,” amesema.
Familia hiyo imesema ina amini wahusika watagundua kuwa si yeye aliyerusha kiatu hicho, huku ikisema uchunguzi ukifanyika kwa kina itabainika hakufanya hivyo.