DAKIKA 40 ndiyo zitaamua. Ni fainali ya Ligi ya Kikapu Daraja la Kwanza Dar es Salaam, kati ya Polisi dhidi ya Stein Warriors itakayopigwa kesho, kwenye Uwanja wa Donbosco, Oysterbay, kuanzia saa 1:00 usiku.
Timu hizo pia zimekata tiketi ya kucheza Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) kutokana na kumaliza katika nafasi mbili za juu.
Kwenye mchezo huo ni robo nne zitachezwa huku kila moja ikiwa na dakika 10 huku kila moja kocha anaweza akaomba muda wa kutoa maelekezo kwa dakika moja.
Baada ya robo moja kumalizika wachezaji watapumzika kwa dakika mbili na baada ya robo mbili kumalizika watapumzika kwa dakika 15.

Utamu wa mchezo huo wa fainali unatarajiwa kunoga kutokana na timu hizo kukutana tena na katika mchezo wa kwanza wa mzunguko, Polisi iliichapa Stein kwa pointi 71-58.
Nyota wa Lawi Mwambasi amesema timu hiyo imejipanga vizuri kushinda katika fainali hiyo.
“Tumefanya mazoezi makali na wachezaji wote wanaisubiri fainali hiyo kwa hamu,” alisema Mwambasi ambaye akishirikiana na nyota wenzake kama Fahmi Hamadi, Issa Ismail, Augustino Kassim, Noel Mwazembe na Siaba Saidi.
Kwa upande wa Stein iliyo na mashabiki wengi zaidi inawategemea mafundi wa kutupia James Ngaboyeka na Lius Nyoni. Wengine ni Davis Mshamu, Mwinyipembe Jumbe, Nassir Mussaji na Davis Mshamu.
Kurasini, Mlimani zitauana
Mchezo huo utatanguliwa na mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu kati ya Kurasini Heat dhidi ya Mlimani B.C ambao walitolewa na Polisi na Stein kwenye nusu fainali.
Polisi iliifunga Mlimani B.C kwa pointi 85-78, huku Stein Warriors ikiifunga Kurasini Heat kwa pointi 69-50.

Mchezo huo unatarajia kuwa ni mgumu kutokana na kila timu kusaka nafasi moja ya kucheza ligi ya BDL na kupanda pamoja na Polisi na Stein .
Maafande waandika historia
Polisi imeweka historia ya kutofungwa na timu yoyote katika ligi hiyo tangu ianzishwe miaka 20 iliyopita na ilimaliza michezo yake 17 huku ikikusanya pointi 34.
Baada ya hapo ilitinga robo fainali, ikaifunga Yellow Jacket kwa pointi 88-66 na nusu fainali ikaishinda Mlimani B.C kwa pointi 97-78.
Stein Warriors katika ligi hiyo ilishika nafasi ya pili kwa pointi 32, katika michezo yake ilifungwa na Polisi kwa pointi 71-58, na baada ya hapo ikafungwa na Chang’ombe Boys kwa pointi 68-57.

Timu 18 zilishiriki ligi hiyo ambazo ni; Polisi, Stein Warriors, Kurasini Heat, Mlimani B.C, Mbezi Beach, Kigamboni Heroes na Yellow Jacket.
Zingine ni Kibada Riders, PTW, Christ the King, Magone, Premier Academy, Dar King, Donbosco VTC, Mgulani Warriors, Magnet na ST.Joseph.
Kurasini yapiga mkwara
Baada ya Kurasini Heat kutolewa nusu fainali na Stein Warriors, nahodha wa timu hiyo, Dominic Zacharia anasema nguvu yao kwa sasa wameielekeza katika mchezo wao na Mlimani B.C.
Alisema mchezo huo utakuwa na umuhimu mkubwa kwao, kutokana na timu itakayoshinda itaungana na Polisi na Stein Warriors kucheza ligi ya BDL mwaka huu.
“Mapungufu ya Mlimani B.C tuliyaona katika mchezo wao na Polisi, na tumeyafanyika kazi na hivyo tumejipanga kutoa kichapo kwa timu hiyo,” alisema Zacharia na kuongeza kiu yao ni kucheza ligi ya BDL mwaka huu.

Mushi wa Premier ataja kilichowaangusha
Nyota wa Premier Academy, Calvin Mushi anayecheza nafasi ya ‘shooting guard’ alisema ukosefu wa pesa na hamasa ndiyo sababu za timu hiyo kufanya vibaya katika michuano hiyo.
Alisema walikosa pesa za nauli na hivyo kushindwa kusafirisha wachezaji wote ikiwamo pia kukosa pesa za kununua maji wakati wa mchezo.
“Tulikuwa tunajichangisha wenyewe nauli na wakati mwingine kocha wetu, Stephen Aloo alikuwa ana sapoti,” alisema na kuongeza;
“Ikipatikana fedha kwa wadau, tunanunua maji lakini hayatoshelezi.”
Mushi aliyeshika nafasi ya saba kwa kufunga eneo la ‘three points’ 24, alisema endapo watapata udhamini watakuja kucheza robo fainali.
Timu ya Premier Academy katika msimamo wa ligi hiyo ilishika nafasi 13 kwa pointi 23, kati ya michezo 17 iliyocheza.