Faili la Yanga CAS kutibua kikao cha dabi dar?

MACHI 8, 2025, ilitarajiwa kuchezwa mechi ya Ligi Kuu Bara namba 184 kati ya Yanga dhidi ya Simba, lakini Bodi ya Ligi iliahirisha saa tano kabla ya kuanza kwa mchezo huo uliopangwa kuanza saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Simba ilidai makomandoo wa Yanga waliwakatalia kuingia uwanjani kwa ajili ya mazoezi siku moja kabla ya mchezo kama kanuni zinavyoelekeza ndipo wakatoa taarifa rasmi kwa Bodi ya Ligi Kuu na TFF, hawatoshiriki mchezo huo kwa sababu haki yao ya kufanya mazoezi kabla ya mechi ilikuwa imekiukwa, kama ilivyobainishwa katika kanuni za Bodi ya Ligi.

Kwa upande mwingine, Yanga ilisisitiza mchezo huo ungechezwa kama ilivyopangwa, kulingana na kanuni za ligi. Lakini badae haukuchezwa, Bodi ya Ligi ilitoa tamko rasmi la kuahirisha mchezo.

Serikali chini ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi imeitisha kikao kitakachofanyika Alhamisi hii Jijini Dar es Salaam ikiwakutanisha Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB), Klabu ya Yanga na Simba ili kutatua mgogoro unaoendelea kuhusu kuahirishwa kwa mchezo huo. 

Mwanaspoti linajua eneo utakapofanyika mkutano huo umefanya siri kubwa ili kuepusha uwepo wa watu wasiohusika kutokana na presha ya sakata hilo.

Kama Yanga itathibitisha kikaoni kwamba imefungua kesi kwenye Mahakama ya usuluhishi ya kimataifa ya michezo(CAS) huenda ajenda za kikao hicho zikabadilika ghafla na pengine kikaishia dakika chache zinazofuata,Mwanaspoti limebaini.

Serikali chini ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi imeitisha kikao kitakachofanyika Alhamisi asubuhi Jijini Dar es Salaam ikiwakutanisha Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPLB), Klabu ya Yanga na Simba ili kutatua mgogoro unaoendelea kuhusu kuahirishwa kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Bara uliotakiwa kuchezwa usiku wa Machi 8.

Wakili maarufu na mdau wa michezo, Aloyce Komba ameonya kuwa maamuzi ya kikao hicho lazima yatangazwe kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia kanuni za soka nchini.

Komba alisema ni vyema Waziri Kabudi akaitisha kikao hicho ili kutatua mkanganyiko uliopo, lakini tahadhari lazima ichukuliwe ili kulinda maslahi ya soka nchini na kuzingatia Fifa.

“Waziri kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ndiyo mamlaka ya msingi ya kusimamia michezo nchini, ikiwamo soka. Ni dhahiri TFF limesajiliwa BMT kupitia kwa msajili wa vyama na vyombo vya michezo, hata hivyo kanuni za Fifa ziko wazi, na maamuzi ya mkutano huu yasipingane na kanuni hizi,” alisema Komba.

Komba alibainisha kuna mambo mawili ya msingi yanapaswa kuangaliwa kwani endapo Yanga ikieleza imewasilisha suala hilo CAS, basi kikao hicho hakitakuwa na mamlaka ya kujadili na lazima kusubiri uamuzi ya CAS. “Kuna mambo mawili ya msingi ya kuzingatia katika kikao hiki, kwanza ni kikao cha maamuzi ikiwa Yanga hawajapeleka suala hilo CAS, iwapo Yanga hawajapeleka suala hilo CAS, kikao kinaweza kutoa maamuzi ambayo kwa maoni yangu yatangazwe na TFF au TPLB.

“Iwapo Yanga itaeleza kuwa tayari imeshawasilisha suala hilo kwa CAS, kikao hicho hakitakuwa na mamlaka ya kujadili suala hilo na ni lazima kusubiri uamuzi wa CAS. Kwa hiyo suala hili ni gumu,” alisema Komba.

Alifafanua kuwa Fifa imeweka wazi kuwa kesi au malalamiko yote lazima yashughulikiwe na vyombo vyake vilivyoteuliwa na si vingine.

Wakati Komba akiyasema hayo, Mwanasheria Emmanuel Muga alisema; “Ujue kamati husika ndio zilitakiwa kufanya hayo, ila kwa sababu haikutimiza majukumu yake bali waliamua kisiasa, ndio maana hayo yanafanyika sasa.

“Ninachokiona ni kwamba inakwenda kufanyika upatanishi kati ya hizi timu mbili na sio kutoa maamuzi ya nini kifanyike. Fifa kanuni zake ziko wazi kwamba Serikali haipaswi kuingilia maamuzi ya soka, ila kwa kwetu kinachokwenda kufanyika kinatuweka kwenye mikono salama ya kisheria za mpira wa miguu,” alisema Muga.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, amesema; “Kikao hicho naamini kitakuwa maalum kwa ajili ya kujadili tatizo lililosababisha mchezo huo usichezwe kwa kusikiliza pande zote husika na kuangalia ni nini cha kufanya, kitendo cha namna hiyo hakina maana Serikali inaingilia masuala ya michezo.”

Angetile alisema ikiwa kama Serikali itatoa kauli ya mchezo huo uchezwe au usichezwe katika kikao hicho hapo ndio ina maana wameingilia masuala ya michezo tofauti na kanuni, ila anachoamini mwisho wa siku mamlaka zitaachiwa zimalize zenyewe.

TAARIFA ZA KUWEPO KIKAO

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa,kikao hicho kimepangwa kufanyika Dar es Salaam. Msigwa alisema kuwa viongozi wote wa Yanga, TFF, na TPLB wamejulishwa na kuthibitishwa kuhudhuria kikao hicho.

“Kikao kitafanyika kama ulivyopangwa, na viongozi wote wamejulishwa na kuthibitishwa kuhudhuria. Mahali pa mkutano ni siri,” alisema Msigwa.

TUMEFIKAJE HAPA?

Machi 8, 2025, ilitarajiwa kuchezwa mechi ya Ligi Kuu Bara namba 184 kati ya Yanga dhidi ya Simba, lakini Bodi ya Ligi iliahirisha saa tano kabla ya kuanza kwa mchezo huo uliopangwa kuanza saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Simba ilidai makomandoo wa Yanga waliwakatalia kuingia uwanjani kwa ajili ya mazoezi siku moja kabla ya mchezo kama kanuni zinavyoelekeza ndipo wakatoa taarifa rasmi kwa Bodi ya Ligi Kuu na TFF, hawatoshiriki mchezo huo kwa sababu haki yao ya kufanya mazoezi kabla ya mechi ilikuwa imekiukwa, kama ilivyobainishwa katika kanuni za Bodi ya Ligi. Kwa upande mwingine, Yanga ilisisitiza mchezo huo ungechezwa kama ilivyopangwa, kulingana na kanuni za ligi.

Hata hivyo, baadaye mchana, Bodi ya Ligi ilitoa tamko rasmi ikitaja wasiwasi wa Simba na kutaja Kipengele cha 34.1 (1.3) cha kanuni kinachotoa ruhusa ya kuahirisha michezo kwa mazingira ya dharura.

Baada ya kuahirishwa kwa mchezo huo, Yanga iliendelea na taratibu za mchezo na ilikwenda uwanjani licha ya mechi kuahirishwa, baadaye ikaiandikia barua Bodi ya Ligi kuomba kupatiwa alama tatu kufuatia wapinzani wao kutofika uwanjani lakini baada ya kutoridhishwa na majibu kutoka Bodi ya Ligi, wakaenda CAS kudai haki yao.

MATOKEO YA KUFUNGIWA

Endapo kukifanyika tofauti na maelezo ya hapo juu kutoka kwa wataalamu na Serikali ikibainika kuingilia masuala ya kimichezo, rungu la Fifa litaiangukia Tanzania huku adhabu ya namna hiyo huzigusa timu zote za nchi kuzuiwa kushiriki mashindano ya kimataifa kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya taifa.

Kama rungu hilo likiiangukia Tanzania, maana yake ni kwamba itaigusa Taifa Stars ambayo inajiandaa kushiriki mashindano ya CHAN mwaka huu ambapo Tanzania ni wenyeji, pia michuano ya AFCON 2025 itakayofanyika Morocco, pia Serengeti Boys iliyopo Morocco kwa ajili ya mashindano ya AFCON U17. Kwa upande wa klabu, kwa sasa itaiathiri Simba ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa hatua ya robo fainali.

Pia marufuku hiyo ikitokea kwa muda mrefu kama ilivyokuwa Kenya iliyofungiwa kwa takribani miezi tisa kabla ya kufunguliwa, maana yake msimu ujao hatutakuwa na wawakilishi kimataifa wakati huu ambao Tanzania inaingiza timu nne katika mashindano ya CAF.

Jambo lingine kuhusu marufuku hiyo, itawagusa waamuzi ambao watazuiwa kushiriki katika majukumu ya kimataifa, sambamba na TFF kusitishiwa fedha za miradi ya maendeleo ya soka kutoka Fifa.

KENYA, ZIMBABWE WALIKIONA

Februari 2022, Fifa ilitoa taarifa ya kuzipiga marufuku Kenya na Zimbabwe kushiriki katika shughuli zote za mpira wa miguu kutokana na hatua ya serikali kuingilia masuala yake.

Rais wa Fifa, Gianni Infantino alisema: “Bila ya kuathiri uchunguzi wowote wa mamlaka ya kitaifa au vyombo vingine vya mahakama, baraza la Fifa pia liliamua kusimamisha Shirikisho la Soka la Kenya na Chama cha Soka cha Zimbabwe mara moja kutokana na kuingiliwa isivyofaa na serikali.”

Hatua hiyo ilifuatia baada ya Waziri wa michezo nchini Kenya, Amina Mohammed, Novemba 11, 2021 kulifuta shirikisho la soka nchini humo (FKF) lililokuwa likiongozwa na Nick Mwendwa na badala yake kuunda kamati simamizi, miongoni mwa masuala mingine, ili kuendesha soka kulingana na katiba ya shirikisho hilo.

Katibu mkuu wa Fifa, Fatma Samoura, aliandikia Serikali ya Kenya mara mbili baada ya kuvunjwa kwa shirikisho hilo la soka, akiitaka Serikali kuirudisha ofisini kamati ya FKF ili kuendelea kutafuta suluhu. Rais wa FKF, Nick Mwendwa alikamatwa katika matukio mawili tofauti na kushtakiwa kwa kushiriki katika ufisadi kabla ya kujiuzulu.

Uamuzi wa FKF kuvunjwa ilitajwa kuwa ni kinyume na miongozi ya Fifa huku ikitoa vitisho vya kupiga marufuku soka nchini. Shirikisho hilo katika msururu wa mawasiliano yake na serikali lilisisitiza kurudishwa ofisini kwa FKF na kuanzisha mipango ya majadiliano ili kutatua tatizo lililopo. Hata hivyo marufuku hiyo iliyodumu kwa takribani miezi tisa, hatimaye Novemba 25, 2022 FIFA iliifungulia Kenya na viongozi wa FKF kurejea ofisini.

UGANDA CHUPUCHUPU

Mwaka 2019, nchi ya Uganda ilikaribia kufungiwa baada ya FIFA kuipa onyo ikiwa Serikali ya nchi hiyo itaingilia masuala ya soka.

Onyo hilo lilitolewa siku chache baada ya Serikali ya Uganda kutangaza nia ya kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za ubadhilifu wa fedha zinazomkabili Rais wa Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa), Injinia Moses Magogo.

Magogo alikuwa akidaiwa kuhusika na mauzo holela ya tiketi za kutazama Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 zilizofanyika nchini Brazil ambazo Fufa ilipatiwa na Fifa jambo lililofanya FIFA kuanzisha uchunguzi uliomtia hatiani na kupelekea kupewa adhabu ya kufungiwa kujihusisha na soka kwa muda wa miezi miwili sambamba na faini ya kiasi cha fedha Sh37 milioni za Uganda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *