
Dar es Salaam. Shule za msingi na sekondari za jijini Dar es Salaam zimejitokeza kuadhimisha Siku ya Skauti wa Kike (Girls Guide) huku msisitizo ukitolewa kwa wazazi kuwahamasisha watoto wao kujiunga na kundi hilo.
Yakiwa na lengo la kuwajenga watoto wa kike wenye umri mdogo katika kujitambua, kujiamini, na hata kujenga uzalendo katika nchi yao, maadhimisho hayo yamefanyika leo Februari 22, 2025 huku mgeni rasmi akiwa Ofisa Tawala wa Wilaya ya Ilala Frola Mgonja.
Katika maadhimisho hayo Frola amesema kujitambua kwa mtoto wa kike kunaanzia kwa wazazi wake nyumbani, kama wazazi watapendana basi ni rahisi hata watoto kujitambua na kujiamini kwake kujijenga kwa wepesi.
“Mtoto wa kike kujiamini kunaanzia kwa wazazi, kama wazazi watapendana hata mtoto ataiga hivyo,” amesema huku akiahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo.
Kwa pamoja amewaomba wazazi na walimu kuwasisitiza watoto wakike kujiunga na skauti kwani kufanya hivyo kutawapa mtoto kujiamini, kujitambua hata uzalendo wa nchi yake.
Kwa upande wa mkuu wa skauti wa kike (Girls Guide) inchini Tanzania Marry Richard amesema kumuondoa hofu mtoto wa kike husaidia kumjenga kujipatia fursa awapo mkubwa.
“Maana kamili ya maadhimisho haya ni kumjenga kiakili mtoto wa kike na kwa kufanya hivyo ni rahisi kumpata Samia (Rais wa Tanzania) mwingine,” amesema Marry.
Ameendelea kusema “Leo hii tupo hapa kwenye jua tunajadili namna ya kumjengea uwezo mtoto wa kike unaweza kuona kama tunacheza lakini tunafanya kitu kikubwa sana,” amesema.
Mmoja wa wanafunzi kutoka shule ya sekondari Kibasila Lisa Renatus, amesema ni mara ya kwanza kushiriki maadhimisho hayo lakini kuna mengi amejifunza kutoka kwa wenzake.
“Leo nimejionea jinsi watoto wa kike wadogo wanavyojiamini kwani wanaweza kuongea mbele ya umati wa watu pasipo hofu yoyote,” amesema Renatus ambaye anasoma kidato cha pili.
Kwa kawaida maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka Februari 22 ikiwa ni sehemu ya kumuenzi waasisi wa siku hio ambao ni Lord Robert Powell na mke wake Olave Baden Powell waliozaliwa siku mmoja huko jijini London.