Faida ya wazazi kutenga muda kusikiliza watoto

Dar es Salaam. Je, wewe mzazi au mlezi katika ratiba yako ya siku nzima,  huwa unatenga muda kwa ajili ya kusikiliza yale anayotaka kukuambia au kukusimulia mtoto?

Katika mzunguko wa siku nzima watoto hukutana na mambo mbalimbali ambayo wanaporudi nyumbani, hutamani kuwahadithia walezi ama wazazi wao wakati mwingine kwa lengo la kujua uzuri au ubaya juu walichokiona.

Kwa bahati mbaya baadhi ya wazazi hawazingatii hilo na kuwaona watoto kama wasumbufu,  jambo linalowafanya watoto kutozungumza  na wazazi wao kuhusu mambo wanayokutana nayo kila siku au yale yanayohitaji utatuzi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa wataalamu wa saikolojia na malezi,  mawasiliano kati yake na mzazi ni jambo la msingi linalochangia ukuaji wake wa kihisia, kijamii, na kiakili.

 Akizungumza na Mwananchi, mtaalam wa malezi kutoka shirika linaloshughulikia masuala ya watoto na malezi,  Bright Jamii Initiative, Irene Fugara  anasema jambo hilo ni muhimu kuzingatiwa kwani mtoto anapojua kuwa mzazi wake anapenda kuwa karibu naye,  inamjenga kujiamini na kuona kuwa anathaminiwa.

Hata hivyo,  Fugara anasema mara nyingi watoto huwa wana mambo mengi ya kuzungumza kwa walezi wao, lakini uwasilishaji wao huwa tofauti kulingana na umri.

Anasema kwa watoto wenye umri mdogo sana huwasilisha kwa njia ya kusimulia bila mpangilio.

“Ndani ya hayo masimulizi yasiyo na mpangilio,  kuna taarifa nzima ya kile alichotaka kukueleza hivyo ni vyema mzazi kuwa makini, ”anaeleza.

Anaongeza kuwa ni muhimu wazazi kufahamu kuwa watoto hawana muda rasmi wa kusema kile wanachotaka kuwaaambia wazazi wao.

“Mzazi kazi yake ni kuwa tayari kumsikiliza na kuwa makini na kile anachokizungumza na kuwa mbali na mazingira ambayo yatakuondolea umakini kumsikiliza,. Kwa  mfano,  weka kando matumizi ya simu kwa wakati huo, ”anaeleza.

Anaongeza kuwa ni vyema mzazi kuwa mvumilivu na msikivu kwani kuna mambo anaweza kuyazungumza lakini yakawa  hayaeleweki au hayana mwelekeo.

“Baadhi ya wazazi baada ya kuona stori hazina mwelekeo huwaza kuwafokea watoto, hiyo siyo sawa. Mzazi anatakiwa awe mwepesi wa kusikiliza na kuuliza ili kumfanya mtoto kuwa huru kuendelea kuzungumza akijihisi yuko salama.

Anasisitiza kuwa kwa mzazi hata ukiona anazungumza kitu ambacho haukubaliani nacho usikimbilie kumfokea na kumpiga,  bali endelea kumdadisi ili aweze kukuelezea zaidi na kumfundisha kwa nini jambo hilo si sahihi.

Anasema kuwa kitendo cha mzazi kumpa fursa mtoto kuzungumza na kumsikiliza,  kunamsaidia  kujua mazingira anayoishi, watu wanaomzunguka mtoto pindi unapokuwa mbali naye.

Wazazi wanafanya hivyo?

Neema Shabani ambaye ni mama wa watoto wawili anasema kupitia ‘story’alizokuwa akisimuliwa na mtoto wake,  zilimsaidia kubaini mtoto wake alikuwa katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya kikatili.

“Alinihadithia kuwa kuna kijana anampatia peremende na kumuita mchumba na kumwambia apite nyumbani kwake atampatia peremende nyingine zaidi”

Anasema kama mzazi ilimtia shaka na kuamua kuweka mtego ambao ulisaidia kumnasa kijana huyo na kumuepusha mtoto wake kufanyiwa vitendo vya kikatili.

Joseph Kalokaza ambaye ni baba wa watoto wanne anasema ni mara chache anapata muda wa kuzungumza na watoto wake,  kutokana na shughuli za kutafuta mkate wa kila siku.

“Mara nyingi huwa wako na mama yao na ndio wanamsimulia na wakati mwingine ananieleza kile walichomwambia,  lakini mimi binafsi ni mara chache kufanya hivyo kutokana na kukosa muda, ”anaeleza.

Faida zake ni zipi?

Mtaalamu wa malezi na saikolojia, Modesta Kamonga anasema pamoja na mambo mengine kitendo cha mzazi kumsikiliza mtoto,  kinajenga ukaribu na upendo zaidi baina yao.

Anasema kwa kufanya hivyo,  humjenga mtoto kumuona mzazi au mlezi wake kama rafiki na kuwa huru kumueleza juu ya yale anayopitia.

“Kwa kufanya hivyo utamuepusha mtoto na kupata majibu ya maswali yake kutoka kwa watu wengine, ambao wakati mwingine wanaweza kumpotosha”

“Mtoto anapohisi kusikilizwa, hujenga imani na ukaribu na mzazi wake, Hili humwezesha kushiriki mawazo yake kwa uwazi na kwa uhuru zaidi, ”anasema.

Anaeleza kuwa kwa kufanya hivyo pia kunamjenga mtoto kujiamini na kuboresha uwezo wake wa kujieleza.

“Watoto wanapojua kuwa wazazi wao wanawasikiliza kwa umakini, hujifunza kuthamini mawazo yao na kupata ujasiri wa kujieleza. Hii husaidia kukuza kujiamini kwao na kuwafanya wawe watu wenye mtazamo chanya kuhusu maisha,”anasema.

Pia anasema kupitia mazungumzo ya mara kwa mara, mzazi anaweza kuelewa vizuri mahitaji na changamoto anazopitia mtoto na kuchukua hatua stahiki mapema.

“Mzazi anapotenga muda wa kumsikiliza mtoto wake, anapata nafasi ya kuelewa chanzo cha changamoto fulani ambayo imemkuta mtoto wake na kumpatia msaada unaohitajika kwa haraka,”anasema.

 Kusikiliza watoto si tu jukumu bali pia ni fursa ya kuwasaidia kukua vyema na kuwa watu wazima wanaojiamini na wenye maadili mema.

“Mzazi anapaswa kutenga muda wa kuzungumza na mtoto wake kila siku, kumsikiliza kwa umakini na kumwonyesha kuwa mawazo na hisia zake ni muhimu. Kwa kufanya hivyo, tunajenga jamii yenye watu waliokuzwa kwa upendo,”anaeleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *