
Dar es Salaam. Miongoni mwa maswali yanayozunguka vichwa vya wengi ni kuhusu namna ambavyo Tanzania itanufaika, ikiwa Mtanzania atapata nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa kanda ya Afrika, Shirika la Afya Duniani (WHO).
Ili kukutegulia kitendawili hiki, Mwananchi imekusogezea faida sita (6) zitakazoinufaisha nchi, iwapo mgombea aliyeteuliwa na nchi (Profesa Mohammed Janabi) atafanikiwa kushinda kiti hicho.
Wakati mijadala ikikolea zaidi baada ya mgombea huyo na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuonekana jijini Ouagadougou na Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, jana (juzi) Aprili 17, 2025 wachambuzi wameanika faida hizo.
Miongoni mwa faida zilizotajwa ni pamoja na kuingiza fedha za kigeni pamoja na baadhi ya Watanzania kupata nafasi za kufanya kazi katika shirika hilo kufuatia mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika sekta ya afya.
Mafanikio hayo kwenye miundombinu katika ngazi ya msingi, kupunguza vifo vya wajawazito na afya kwa wote ni miongoni mwa sifa kupata nafasi hiyo ambayo ni mara ya kwanza kupewa nchi za Afrika Mashariki.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema kuna faida nyingi kwa nchi kupata nafasi hiyo, amesema Taifa litanufaika moja kwa moja ikiwa nafasi hiyo itakaliwa na Mtanzania.
“Tutaingiza fedha za kigeni, kiongozi mkuu atalipwa mshahara kwa fedha za kigeni kupitia ofisi zake za Tanzania ni mamilioni ya fedha. Lakini hawezi kwenda mwenyewe kuna Watanzania wanafanya vizuri maeneo kadhaa ikiwemo eneo la kupunguza vifo vya mama na mtoto.
“Vifo vya uzazi asilimia 60 vinatokea Afrika sasa ukiangalia sisi tumefanikiwa kupunguza kufikia 104 kati ya vizazi hai 100,000 lakini nchi za Sudan Kusini bado vipo 1,100 kila vizazi hai 100,000 na Kenya ni miongoni mwa nchi zilizo kwenye nchi 10 zinazoongoza.
“Waliohusika kufanikisha haya wana nafasi kubwa ya kuambatana naye WHO ili kusaidia kupunguza hili tatizo na pia magonjwa ya mlipuko na maeneo mengine,” amesema Dk Mugisha.
Ametaja faida nyingine za kiutumishi, kwamba nchi itafahamu mengi yanayoendelea ndani ya Shirika na itakuwa sehemu ya washiriki na hivyo kuongeza mchango wake Afrika na Taifa litafaidika kupata kazi, kandarasi kadha wa kadha na taarifa.
Pia amesema kuna mambo yatakayojitokeza katika uendeshaji wa shirika, kama nchi wanachama tutafaidika kwa kiasi fulani na miradi na mikakati inayowekwa.
“Kuna faida za kidiplomasia, tuna fahari kuwa sasa tuna watu kama hao nje ya nchi kwa sababu Tanzania ina mchango wake mkubwa katika kuendeleza Afrika, ukombozi wa nchi mbalimbali. Ni wakati mwingine tunatapata mtu ambaye atatuwakilisha kupambana na maradhi ya kuambukizwa na yasiyoambukiza,” amesema.
Amehimiza kuwa faida nyingine ni kuwafungua vijana kwamba inawezekana kuiongozi wa Afrika kutoka nchini kwake, wengi wana sifa lakini wamekuwa hawaombi nafasi hizo, ushiriki umekuwa mdogo kwa muda mrefu na kwmaba hiyo ni hamasa watoke kama ilivyo kwa Wakenya na Nigeria.
Gharama za kampeni
Mchakato wa kumpata kiongozi wa WHO Kanda ya Afrika, unahusisha kura moja kutoka mataifa 46 yanayounda bara zima, kura hizi huamuliwa na kiongozi mkuu wan chi husika, huku akiwakilishwa na kiongozi wa juu wa sekta ya afya katika upigaji kura ambaye ni Waziri wa Afya.
Hii ndiyo sababu jana Mjumbe Maalumu wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete amehitimisha ziara yake kwa kukutana na Rais wa Burkina Faso, Captain Ibrahim Traoré katika mkutano uliofanyika jijini Ouagadougou na kuhudhuriwa na maafisa waandamizi kutoka Serikali zote mbili.
Katika mkutano huo Kikwete alisema, “Rais wangu amenituma nije kuwasilisha ujumbe maalum kwako na nimefurahi umenipa fursa hiyo na leo umeupokea rasmi.”
Pamoja na hayo Kikwete aliwasilisha ujumbe kutoka kwa Rais Samia kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za Afrika, hususani Burkina Faso na Tanzania na kwmaba anatamani kuona kwenye maeneo mengi ambayo wanaweza kushirikiana wanafanya hivyo ikiwemo kubadilishana uzoefu ili kwa pamoja Afrika iweze kuendeleza rasilimali zake.
“Miongoni mwa maeneo ambayo tunaweza kushirikiana ni pamoja na eneo la afya, hasa katika magonjwa ya moyo, timu ya teknolojia ya Burkina Faso watakutana na Profesa Janabi leo na kuzungumza namna ambavyo tunaweza kushirikiana katika eneo hilo na madaktari kuona namna gani tunaweza kufanya kazi pamoja,” alisema Kikwete.
Hata hivyo Dk Mugisha anasema kampeni za kimataifa si jambo rahisi, “Mchakato wa kumpata kiongozi huyo unahusisha kura na wapiga kura ni viongozi wa afya kwa maana ya mawaziri wa afya nchi wanachama 46.
“Marais wote nawakilishwa kupitia mawaziri wao, ukitaka kupiga kampeni kwa kuwa ni mambo ya kidiplomasia kiongozi wa nchi ndiye anayehusika kumwombea kura mgombea wake, kwa kiasi fulani mipango imeenda vizuri,” amesema
Hata hivyo amesema haijatumika gharama kubwa na hivyo ndivyo kampeni hufanywa. “Ujumbe utatumwa kwa Rais wa nchi husika. Rais anayemwombea kura mgombea wake hawezi kumtuma Katibu Tarafa atamtuma mtu mwneye hadhi kufikisha ujumbe wake.”
Mtaalamu wa Afya ya Umma ambaye pia amewahi kufanya kazi WHO kwa miaka 10, Dk Ali Mzige amesema Tanzania imefanya kampeni kubwa kumnadi mgombea wake.
Hata hivyo amesema Profesa Janabi anakabiliwa na kibarua kikubwa cha kujifunza kwanza namna ambavyo kazi zinafanywa WHO ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa Dk Faustine Ndugulile.
“Atatakiwa kujifunza kwanza, tofauti na ilivyokuwa kwa marehemu Dk Faustine Ndugulile ambaye alishawhai kukaa katika kamati fulani za WHO.”
Uzoefu wa kampeni
Uchaguzi huo umeitishwa kwa mara nyingine baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo, Dk Faustine Ndugulile kutoka Tanzania.
Dk Ndugulile aliyekuwa mbunge wa Kigamboni, alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Alitarajiwa kuanza kazi rasmi WHO Machi 2025, baada ya kupewa miezi sita ya kujipanga baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo Agosti 27, 2024.
Alishinda nafasi ya Mkurugenzi wa WHO, Kanda ya Afrika akiwashinda wagombea wengine ambao ni Dk Boureima Hama Sambo wa Niger, Dk N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast), Dk Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).
Baada ya nafasi hiyo kubaki wazi, Tanzania ilimpendekeza Profesa Janabi kuwania nafasi hiyo, uteuzi uliotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akisema uzoefu wake katika sekta ya afya unamfanya kuwa mgombea mwenye sifa stahiki kwa nafasi hiyo muhimu kimataifa.