
Dar es Salaam. Ikiwa leo ni Jumatano ya Majivu mwanzo wa mfungo wa siku 40 wa Kwaresma, Wakristo wamekumbushwa kutenda mema, kujinyima na kuwakumba wenye mahitaji.
Sambamba na hilo katika mfungo huu wa Kwaresma kila anayetaka kufunga na afunge lakini msisitizo ni kwa wale wenye afya njema kama anavyosema Padre, Dk Clement Kihiyo Katibu Mtendaji Idara ya Liturujia wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),.
Akifanya mahojiano maalumu na Mwananchi hii leo Padre Kihiyo amesema anayepaswa kufunga lazima ana afya njema.
Amesema kwa watoto wadogo wanaohitaji kukua lazima wale.
“Wanafunzi wanaolazimika kushinda darasani wasome wafaulu masomo yao wanatolewa hiki kifungo cha kufunga ili waweze kusoma vizuri. Wagonjwa wanaotumia dawa za hospitalini ambazo lazima zisindikizwe na chakula hawapaswi kufunga.”
“Wazee ambao umri wao umeenda wakifunga afya zinaweza kuteteleka wakaingia katika hatari wanaambiwa wasifunge. Kina mama wanaonyonyesha ambao lazima wawe na maziwa mazuri yenye rutuba wasifunge wale chakula waweze kunyonyesha,” amesisitiza.
Padre Kihiyo anasema kipindi hiki ni cha toba na tafakari huku akisema hatufungi chakula tu bali na anasa na starehe pia tunapaswa kutenda mema ikiwemo kusaidia maskini.
“Kama umezoea kupata kinywaji basi kipindi hiki ni cha kufunga kinywaji, kama umezoea kucheza muziki, vishawishi vya macho unapaswa kuachana navyo,” amesisitiza.
Amesema chakula anachojinyima mtu anapaswa kuwapa maskini. “Siyo unajinyima asubuhi na mchana halafu jioni unajiachia, haipaswi kuwa hivyo kwani unapaswa kujitesa kwa ajili ya wenye mahitaji.
Kuhusu Jumatano ya Majivu amesema ni mwanzo wa kipindi cha Kwaresima, muda muafaka wa sala, toba na wongofu wa ndani katika matendo ya huruma kiroho na kimwili.
Padre Paschal Ighondo kupitia chapisho lake la Vatican News anasema Kwaresma ni safari ya maisha ya kiroho ambayo kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu wa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo linaloadhimishwa kuanzia Ijumaa kuu, Alhamisi kuu, Ijumaa kuu na Jumamosi kuu, kilele chake ni domenika ya Pasaka.
Kusali, kujitoa sadaka kwa ukarimu kwa wahitaji na kufunga, ndizo nguzo kuu tatu za kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba. Siku ya kwanza ya kipindi hiki cha Kwarema huitwa Jumatano ya Majivu kutokana na tendo la kupakwa majivu katika paji la uso na wakati huo mhudumu wa tendo hili takatifu la kiroho wakisema; Mwanadamu kumbuka, u mavumbi wewe na mavumbini utarudi. Jina hili la Jumatano ya majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbano II. mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”.
Majivu yanayotumika siku hii ya Jumatano ya majivu ni ya matawi ya mitende yaliyotumika Jumapili ya matawi ya mwaka uliopita ambayo yanaashiria ushindi dhidi ya dhambi na mauti kwa njia ya Yesu Kristo.