Fahamu maumivu ya kichwa yanayozidi uchungu wa uzazi, risasi

Dar es Salaam. Achana na maumivu ya kujigonga kiwiko cha mguu au mkono. Uchungu wa kujifungua ulihisiwa ndiyo wenye maumivu makali ya kiwango cha juu zaidi.

Hata hivyo, utafiti mpya umebaini maumivu ya kichwa yanayofahamika kama ‘Cluster headache attack’, ambayo maishani humkuta mtu mmoja kati ya 100, ndiyo yanayosababisha maumivu makali zaidi kuwahi kuhisiwa.

Ni maumivu ya upande mmoja wa kichwa yanayoweza kuambatana na machozi kutoka jichoni, kope kuanguka, na pua kuziba, yanayoweza kufafanishwa na kipandauso. Mashambulizi yake hudumu kati ya dakika 15 hadi saa tatu na hutokea kila siku au karibu kila siku kwa wiki au miezi.

Utafiti wa uliofanywa nchini Marekani umegundua kuwa maumivu hayo ni makali zaidi kuliko maumvu ya uchungu wa uzazi, majeraha ya risasi na mivunjiko ya mifupa.

Utafiti huo huo ulijumuisha kundi la watu 1,604 wenye maumivu hayo ya kichwa walioulizwa kulinganisha maumivu waliyopitia na majeraha na hali nyinginezo za maumivu waliowahi kupitia, ikiwa ni pamoja na majeraha ya kisu na shambulio la moyo.

Kwa utafiti huo, washiriki waliulizwa kupima kiwango cha maumivu waliyohisi walipokuwa wakiteseka na hali hiyo kwa kipimo cha 0 hadi 10.

Kilichoshangaza, uchungu wa uzazi ulikuwa na alama ya 7.2, miongoni mwa ana nyingine.

Wale walioshuhudia maumivu ya risasi walitoa wastani wa sita kwenye kipimo hicho cha maumivu.

Madaktari waliwahi kuripoti kuwa maumivu kutoka kwa majeraha ya risasi, hutofautiana sana kulingana na sehemu ya shambulio na tumbo, mgongo, kiuno na shingo vinajulikana kuwa na maumivu makali kwa sababu ya wingi wa neva.

Kutolewa kwa ‘disk’, ambapo tishu laini kati ya mifupa ya mgongo hujaa na kushinikiza neva, ilikuwa karibu na maumivu ya risasi kwa alama ya 5.9.

Migraine iliorodheshwa ya nane, ikiwa na alama ya 5.4, ikifuatwa na hali inayohusishwa na matatizo katika mfumo wa neva.

Mashambulio ya moyo yalikuwa na alama ya 5, ikiwa chini kidogo ya kuvunjika kwa mfupa.

Hii ilimaanisha kuwa hali zote mbili zilikuwa juu kidogo kuliko kuchomwa kisu, ambacho kilikuwa na alama ya 4.9 ingawa kama vile majeraha ya risasi, maumivu ya jeraha kama hili yanaweza kutofautiana kulingana na sehemu shambulio lilipotokea.

Maumivu ya cluster ni hali nadra na ambayo haieleweki vizuri, iliyowahi kuathiri takriban watu 65,000 nchini Uingereza.

Hata hivyo, wataalamu hawajui ni nini kinachosababisha maumivu haya, lakini inajulikana mara nyingi hutokea zaidi kwa watu walioko kwenye umri wa miaka 30 na ni mara sita zaidi kwa wanaume kuliko wanawake.

Wataalamu hutumia vipimo vya maumivu kama kiashiria cha uzoefu wa mtu kuhusu jeraha au hali Fulani, lakini kwa sababu maumivu ni uzoefu wa kibinafsi, vipimo hivi vina mipaka yake.

Watafiti, ambao walichapisha matokeo yao katika jarida la Headache, wanasema usahihi wa alama za maumivu za wagonjwa unaweza kupunguzwa na kumbukumbu duni ya washiriki.