Dar es Salaam. Katika dunia ya sasa, mabadiliko ya mwili na afya ni jambo la kawaida, lakini katika yote ni vyema ukafahamu namna bora ya kuondokana na mabadiliko hayo, bila kuathiri utendakaji kazi wa viungo vingine vya mwili.
Wapo wanaoamini unywaji wa pombe hupunguza msongo wa mawazo, vinywaji vyenye kafeini ni tiba ya uchovu (energy drinks) na matatizo ya ngozi ni matokeo ya utumiaji wa vipodozi vikali pekee.
Wakati unaendelea na mapumziko ya mwisho wa wiki, unapaswa kufahamu kuwa, ulaji wa baadhi ya matunda, wakati wa mabadiliko ya vipindi fulani vya maisha na mwili, hufanya kazi kubwa kuliko yale mnayoyaamini ambayo si sawa kiuhalisia.
Aliekwambia unywaji wa pombe hupunguza mawazo, alipaswa akwambie tikiti maji na ndizi mbivu huondoa msongo wa mawazo, kuliko kukaanga ini kila kukicha na hii ni kwa mujibu wa tafiti ya Frontiers in Psychology ya mwaka 2020 na tovuti ya Educativefeed.
Tovuti hiyo, pia ilieleza kuwa licha ya matumizi ya aina mbalimbali za vipodozi ili kupendezesha ngozi tiba ya kwanza ni ulaji wa limau, tufaa, nazi na karoti, ambapo hukuepusha na vipodozi vingi vya kujichubua kupata rangi kadhaa mwilini, mithili ya upinde wa mvua.

Ni ndoto ya kila binadamu kuwa na macho meupe, lakini wengi hukumbana na changamoto au aina fulani ya maisha, ambayo huwabadilisha macho na kuwa mekundi, tovuti hiyo imeeleza kuwa hali hii huondolewa na ulaji wa tufa na karoti kwa wingi.

Wapo wenye mzio wa baadhi ya vitu, ambapo kikohozi huwa maisha yao ya kila siku, watu hawa, hushauriwa kutumia nanasi, vitunguu saumu, na tangawizi, ili kuondoa tatizo hilo na kukuacha mwenye afya na kujiamini.

Pia, si amoeba pekee husababisha mvurugiko wa tumbo (diarrhea), lakini, hata baadhi ya vyakula vilivyokaa muda mrefu na kuharibika vinaweza kuwa chanzo cha hali hiyo, watu hawa, wanashauriwa kula parachichi au kutafuna nazi ili kukomesha tatizo hilo kwa haraka zaidi.

Japo wengi, hutambua kabeji kama mboga ya mwezi Januari, lakini wataalamu wa afya wanashauri matumizi ya mboga hiyo, kitunguu saumu na kitunguu maji, kuondoa tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu, na kuwa hali hiyo, huchochewa na mchakato hafifu wa mfumo wa umeng’enyaji wa chakula.

Aidha, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, binadamu asie na matatizo anapaswa kukojoa kati ya mara nne hadi nane kwa siku, na ikiwa hautimizi idadi hii, si maji pekee, yataondoa tatizo hilo, bali hata, ulaji wa matunda aina ya matango, tikiti na chungwa huongeza kiasi cha maji mwilini na kisha kutimiza idadi hiyo.

Pia, ili uwe na moyo wenye afya, wataalamu wanashauri ulaji wa parachichi, maharage, kitunguu saumu na kitunguu maji, ili kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo,

kwa kuboresha mzunguko wa damu, kupunguza shinikizo la damu, na kudhibiti viwango vya kolestroli mwilini, pia, maji lita mbili kwa siku, nyanya mbichi, ni ushauri wa wataalamu hao ili kuilinda afya ya figo yako.
