Fahamu kuhusu uwekezaji wa hatifungani

Katika ulimwengu wa uwekezaji, hatifungani ni moja ya njia salama na zinazotabirika za kukuza mtaji.

Hatifungani ni hati za dhamana zinazotolewa na serikali au mashirika binafsi kwa ajili ya kukopa fedha kutoka kwa wawekezaji, kwa ahadi ya kulipa faida baada ya muda fulani.

Hatifungani hizi ni kivutio kwa wawekezaji wa aina zote, ikiwa ni pamoja na wawekezaji binafsi na taasisi, kwa sababu ya mapato ya riba yanayothibitika na usalama wa uwekezaji .

Makala hii inafafanua baadhi ya mbinu na mikakati, kama vile faida za kutumia mikopo kwa ajili ya kununua hatifungani na biashara ya tofauti ya bei (arbitrage), zinazoweza kutumika ili kuongeza mapato ya uwekezaji katika hatifungani kwenye Soko la hisa la Dar es Salaam.

Hatifungani ni aina ya dhamana ya Serikali au shirika lililo na dhamana ambapo mwekezaji anatoa fedha kwa taasisi husika kwa muda fulani na baadaye anapata riba na kurudishiwa mtaji wake.

Hati hizi ni vyombo vya madeni vya muda mrefu vinavyotolewa na Serikali au taasisi nyingine na mara nyingi huwa na riba ya kudumu au inayobadilika.

Hatifungani hutumika kama njia ya serikali au taasisi kutafuta mtaji kwa ajili ya miradi mbalimbali, na kwa upande wa mwekezaji, hutumika kama njia ya kupata mapato ya riba kwa kiwango cha uhakika.

Hatifungani za Serikali hutolewa kwa niaba ya Serikali na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kuanzia Januari 2025, BoT imeamua kuweka viwango vya riba vya dhamana kulingana na hali ya soko la sasa badala ya viwango vilivyowekwa awali ambavyo havikuruhusu ubunifu kwa muda mrefu.

Kwa matokeo hayo, hatifungani za Serikali za sasa zinatarajiwa kuwa na faida zaidi kuliko zamani.

Hatifungani hutofautiana kwa muda wa kumalizika, vipindi vya riba zinazojikusanya kwa muda, na muda wa kuiva ambao unaweza kuwa kati ya miaka miwili, mitano, saba, 10, 15, 20 au 25.

Wawekezaji wanaweza kupata na kuuza dhamana zao za hazina kupitia soko la sekondari la Soko la Hisa la Dar es Salaam. Hii inawapa fursa ya kubadilishana dhamana zao kabla ya kumalizika muda wake.

Ili kuanza biashara kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) unahitaji kwanza kufungua akaunti na dalali wa soko la hisa la Dar es Salaam mwenye leseni, dalali huyu atakuwa ni mshauri na mnunuzi kwa niaba yako.

Ni muhimu kuhakikisha unampatia taarifa zako muhimu kama vile namba ya NIDA na namba ya mlipa kodi, picha ndogo na Akaunti ya Benki wakati wa ufunguzi wa akaunti yako.

Mara akaunti yako itakapokuwa tayari, unaweza kushiriki kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, ambapo dhamana zinaweza kununuliwa na kuuzwa, na hivyo kuchukua fursa ya mabadiliko ya bei.

Kwa ujumla uwekezaji wa hatifungani ni njia nzuri kwa mtu binafsi au taasisi kupata faida ya uhakika huku wakihifadhi mtaji wao kwa usalama.

Kwa mtu anayetafuta uwekezaji wenye hatari ndogo lakini wenye manufaa ya muda mrefu, hatifungani ni chaguo bora. Serikali na wawekezaji wanapaswa kuhimiza matumizi ya chombo hiki cha kifedha ili kukuza uchumi na kuboresha hali ya kifedha ya wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *