
Shinyanga. Tumezoea kuona baadhi ya watu wakiweka urembo katika meno yao, hata hivyo wengi wao hawajui faida na athari za kuweka urembo huo.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wana mapendekezo kwa wale wanaopendelea kuweka urembo huo, wakishauri uwekwe kwa wasio na magonjwa ya muda mrefu.
Wasiopendekezwa kuweka urembo huo ni pamoja na wenye magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu na magonjwa mengine yanayohusiana na upungufu wa kinga mwilini.
Hata hivyo, wengi hufanya hivyo kuongeza mvuto, sababu mbalimbali ikiwemo za kiafya na wengine wakishindwa kujua faida na hasara za urembo huo.
Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na urembo huo, mkazi wa Shinyanga, Maresiana George amesema alishawishika kuuweka baada ya kuvutiwa na mwonekano wa meno ya rafiki yake.
“Binafsi nimevutiwa na urembo huu nikaamua kuweka, japo sijui hasara zake nimeweka tu kupata mwonekano mzuri wa kinywa. Huwa nikicheka watu wanasema nina meno mazuri,” amesema Maresiana.
Kauli ya Maresiana inaungwa mkono na Jackline Joachim, anayedai kuwa urembo ni jadi ya mwanamke hivyo ili kujipendezesha analazimika kufanya kila awezalo kwa lengo la kuongeza mvuto wa mwonekano wake.
Faida za urembo wa meno
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Upasuaji Maalum (ENT) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk Anord Christian, ametaja faida, sababu na athari za kuweka urembo huo.
Dk Christian amesema watu huweka urembo huo ili kuimarisha na kuweka umaridadi wa meno na kuongeza tabasamu usoni, hasa kwa wasichana kwa kile anachodai meno ni mapokezi ya kila mtu anapozungumza.
Dk Christian amesema urembo huo hauna athari zozote kwa binadamu kwani unatumia gundi maalumu ambayo haina athari kiafya.
“Hakuna kinachopungua kwenye meno wala kuongezeka, urembo huu unawekwa kwa gundi maalumu ambao unashika meno na muda wowote ukihitaji unaweza kutoa na tunashauri mtu akiweka akae nao miezi mitatu tu na kutoa,” amesema Dk Christian.
Aidha, Dk Christian, amesema kitaalamu inashauriwa kwa walioweka urembo huo kwenye meno kufanya usafi wa meno yao vizuri ili kuondoa mabaki ya chakula yanayoweza kung’ang’ania kwenye meno na kusababisha harufu mbaya ya kinywa.
Athari za urembo wa meno
Dk Christian amesema kabla ya mlengwa kufanyiwa upasuaji wa kupachika urembo huo, hushauriwa na wataalamu kupima afya, huku akidokeza kuwa watu wanaopendekezwa kuweka urembo huo ni wasio na magonjwa ya muda mrefu.
“Huwa tunashauri wateja wenye magonjwa ya muda mrefu wasiweke kwa sababu kinga zao za mwili zinakuwa zimeshuka akiongeza kitu cha ziada ni kama tunazisumbua zilizopo,” amesema.
Ametaja magonjwa ambayo wataalamu huyapima kabla ya kutoa ridhaa kwa mtu anayetaka kupachika urembo kwenye meno kuwa ni pamoja na kisukari na shinikizo la damu na magonjwa mengine yanayohusiana na upungufu wa kinga mwilini.
Walichokisema wadau
Baadhi ya wananchi wametoa maoni yao kuhusiana na uwekaji wa urembo huo, huku wengine wakidai kufanya hivyo ni kukiuka mila na utamaduni wa Kitanzania na kuiga utamaduni wa mataifa ya nje.
“Kuweka urembo huo sio vizuri kwa sababu sio tamaduni za Kitanzania bali ni utamaduni wa nchi za magharibi na kwa ushauri mabinti mnatakiwa kulinda heshima zenu amesema Frank Masaganya.
“Binafsi siwezi kuruhusu watoto wangu waweke vitu hivyo kwanza katika jamii nitaonekana sina malezi bora kwa wanangu na itakuwa na mtazamo hasi juu yangu na pia inashusha heshima ya familia,” amesema Esther Busunzu.
“Mwanamke wa aina hiyo mimi binafsi siwezi hata kumuoa kwa sababu anakosoa uumbaji wa Mungu kwa kujiongezea mapambo mwilini, kwa mtu anayejitambua nashauri aache kuweka urembo huo,” amesema Amos John.