Fadlu: Nitawajibika Simba ikishindwa kufuzu nusu fainali CAFCC

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameweka wazi kuwa endapo kikosi chake kitashindwa kuiondoa Al Masry kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, Jumatano hii, atakuwa tayari kuwajibika.

Kauli hiyo ameitoa katika mkutano na waandishi wa habari leo, baada ya kuulizwa swali la kuhusu uwajibikaji wake iwapo Simba itatolewa.

“Majukumu yote huwa mabegani mwangu, hilo halina shaka. Wachezaji nawaachia wafanye kazi yao na mimi nabeba presha yote mwenyewe. Nitaendelea kufanya hivyo bila kujali matokeo. Huwezi kujiunga na klabu kubwa kama Simba bila kuelewa uzito wa majukumu yake,” amesema Fadlu.

Kesho Simba itakuwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano dhidi ya Al Masry ambapo mchezo wa kwanza uliochezwa Misri kwenye uwanja wa Suez Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1.

Simba inahitaji kupata mabao matatu bila kuruhusu bao katika mchezo wa kesho ili ifuzu kwenda katika hatua ya nusu fainali.

Hata hivyo, wekundu wa Msimbazi wataingia uwanjani na rekodi ya kushinda michezo mingi dhidi Waarabu kwenye dimba la Benjamin mkapa kwani mara ya mwisho ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Al Ahly Tripol, 2-1 dhidi ya CS Sfaxien na 2-0 dhidi CS Constantine.

Katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ilimaliza nafasi ya kwanza katika kundi A baada ya kukusanya jumla ya pointi 13 mbele ya CS Constantine ambayo ilimaliza ya pili ikiwa na pointi 12.

Mara ya mwisho Simba ilicheza mchezo wa robo fainali katika Kombe la Shirikisho msimu wa 2021-2022 ambapo iliondolewa kwa mikwaju ya penalti na Orlando Pirates y Afrika Kusini baada ya timu zote kupata ushindi wa bao moja zilipokuwa nyumbani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *