Fadlu na kibarua kingine kwa wasauzi

Bao la dakika ya 79 lililofungwa na kiungo Sihle Nduli limetosha kuitupa nje Zamalek ya Misri kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini likiivusha Stellenbosch ikiwafuata Simba.

Ushindi huo wa ugenini wa Stellenbosch unaifanya timu hiyo  kukutana na Simba, ikiwazuia wekundu hao kurudi Misri huku ikimrudisha kocha Fadlu Davids kukutana na Wasauzi wenzake.

Simba mapema imepata tiketi ya kufuzu nusu Fainali ya mashindano hayo baada ya kuiondoa Al Masry ya Misri kwa matuta 4-1 baada ya timu hizo kumaliza mchezo kwa ushindi wa mabao 2-0 lakini matokeo ya jumla yakawa 2-2 kufuatia Wekundu kupoteza mchezo wa kwanza kwa idadi kama hiyo.

Matokeo hayo ya Stellenbosch yameshtua Zamalek yakiwaacha na kilio mbele ya mashabiki wake kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo huku wenyeji wakiwa wameutawala mchezo kwa dakika zote 90.

Fadlu anakwenda kukutana na kocha mkongwe Msauzi Steve Barker (57) ambaye anajuana vyema na kocha wa Simba.

Zamalek kutupwa nje matokeo hayo yanaweza kuhatarisha kibarua cha kocha Jose Peseiro ambaye ni raia wa Ureno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *