KOCHA wa Simba, Fadlu Davids, aamesema timu yake itaenda Afrika Kusini kushambulia na kufunga, si kulinda bao moja walilopata nyumbani na kwamba katika dakika 10 za kwanza wataipa Stellenbosch ya Afrika Kusini presha kubwa ili kuimaliza mapema mechi yao ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba ilishinda 1-0 katika mechi ya awali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar na timu hizo zitarudiana Jumapili hii kwenye Uwanja wa Moses Mabhida mjini Durban.
“Tumeweka msingi, lakini nyumba haijajengwa bado. Tunakwenda kwenye mchezo wa marudiano tukiwa na lengo moja tu kutafuta bao la mapema na kumaliza kazi. Hatutacheza kwa kujilinda. Hatutacheza kwa woga. Hatutaki sare. Tunataka ushindi,” alisisitiza Fadlu.

Kwa Simba, huu ni mchezo wa kufa au kupona. Mara ya mwisho walifikia hatua ya nusu fainali ya michuano ya CAF mwaka 1993 na kutinga fainali ambapo walipoteza mbele ya Stella Abidjan. Hiyo ilikuwa ni katika Kombe la CAF ambalo mwaka 2004 liliunganishwa na Kombe la Washindi ikazaliwa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ndiyo hii Simba inacheza nusu fainali.
Fadlu alisema katika maandalizi watakayofanya kabla ya safari yao kuelekea Afrika Kusini, watajikita kwenye mipango ya kushambulia kuanzia dakika ya kwanza ili kusaka bao la mapema angalau dakika kumi za kwanza litakalowapa wakati mgumu wenyeji wao.
“Tunajua Stellenbosch ni timu ya vijana wenye kasi, lakini pia wana udhaifu mkubwa wanapowekwa chini ya presha. Wanafungika. Hilo ndilo tunalotaka kulitumia. Hatutaki kuwapa nafasi ya kujipanga. Tunakwenda kuwavamia,” alisema Fadlu.

Winga wa Simba, Elie Mpanzu, ambaye amekuwa injini ya mafanikio ya timu hiyo katika mechi za hivi karibuni amesema wachezaji wanaiona fainali mbele yao.
Mpanzu ambaye amejiunga na Simba kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea AS Vita ya kwao DR Congo, amekuwa akiwalaza na viatu wapinzani kwa moto anaowapelekea huku usajili wake ukitajwa kutoa majibu chanya kwa haraka ndani ya kikosi hicho.
Winga huyo aliyefunga bao moja wakati Simba ikishinda 2-0 dhidi ya Al Masry na kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameendeleza moto wake katika mchezo wa hatua hiyo dhidi ya Stellenbosch uliochezwa Jumapili iliyopita.
Baada ya mchezo huo wa mkondo wa kwanza, Mpanzu alisema: “Kwa sasa tunaangalia mbele. Tunaiona fainali, lakini hatuwezi kuifikia kwa ndoto tu, tunahitaji kazi, umoja na akili. Tunahitaji kuwakumbusha kila dakika kuwa tunahitaji zaidi yao.”

Kuhusu matokeo ya mchezo wa nyumbani na wanachokwenda kukifanya Afrika Kusini, Mpanzu alisema: “Tumeshinda nyumbani, lakini huu ni mwanzo tu. Mchezo mkubwa zaidi ndio uko mbele yetu. Bao moja linaweza kupotea kwa sekunde 10 tu, kwa hiyo hatuwezi kusema tayari tupo salama. Afrika Kusini tunaenda kuanza upya.
“Tunakwenda kucheza dhidi ya timu ambayo haijapoteza mchezo nyumbani katika michuano hii. Stellenbosch si wapinzani wa kubezwa. Tunahitaji kutuliza presha yao kwa kutawala na kuwalazimisha wacheze kwa kasi yetu.
“Wameona tunavyoweza kufunga. Tunapaswa kutumia nafasi hiyo kuwashangaza mapema kabla hawajapata morali ya mashabiki wao. Bao moja kule linaweza kuvunja kabisa imani yao. Lakini tusipojiangalia, nasi tunaweza kuumia,” alisema.
Kuelekea mchezo huo wa marudiano utakaofanyika Aprili 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Moses Mabhida uliopo Durban nchini Afrika Kusini, Simba wanahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili kufuzu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza, huku Mpanzu akisema hawatacheza kwa kutafuta sare bali ushindi.
“Hatutakiwi kwenda kutafuta sare. Tunatakiwa kwenda kushinda. Timu kubwa haichezi kwa kutetea bao, inacheza kutafuta bao jingine. Hiyo ndiyo falsafa tunayoambiana kila siku,” alisema.

Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein, alisema: “Tuna dakika 90 nyingine Afrika Kusini, jambo la msingi ilikuwa ni ushindi ambao una maana kubwa zaidi kuliko tungepoteza, hatukuwa tunafunguka kwa sababu ya kuheshimu wapinzani wetu ambao walionyesha ushindani.
“Siyo mechi rahisi kwa hatua tuliyofikia, kama wachezaji tuna nia moja ya kwenda kushinda na tunajipanga kwa hilo, faida nyingine ambayo tuko nayo kocha mkuu Fadlu Davids ni mwenyeji wa Afrika Kusini, atatusaidia kufahamu mazingira ya huko.
“Tumekuwa tukiishia robo fainali kwa miaka mingi, ila awamu hii tumefika nusu fainali, imebaki mchezo mmoja utakaoamua sisi kuingia fainali.”