Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amefikisha jumla ya michezo 10 ya Ligi Kuu Bara tangu alipoanza kukinoa rasmi kikosi hicho Julai 5, mwaka huu akichukua nafasi ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyeondoka kikosini humo Aprili 28, 2024.
Fadlu raia wa Afrika Kusini ameanza vyema tangu aipe ubingwa wa Ligi Kuu Morocco, Raja Casablanca akiwa ni msaidizi wa Josef Zinnbauer na kupitia yeye nakuletea makocha waliopita Simba na walichokifanya katika michezo 10 ya mwanzoni tangu 2019.

SVEN VANDENBROECK
Baada ya Simba kuachana na Patrick Aussems ilimpa kazi Mbelgiji wenzake, Sven ambaye alianza kuchukua mataji matatu akianza na taji la Ngao ya Jamii mwaka 2020, pia Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) msimu wa 2019-2020.
Sven alinza kazi Simba Desemba 12, 2019 na katika michezo yake 10 ya mwanzoni alishinda minane, sare mmoja na kupoteza mmoja.
Michezo aliyoshinda ni (4-0) v Lipuli, (0-2) v KMC, (2-0) v Ndanda, (2-1) v Mbao, (4-1) v Alliance FC, (3-2) v Namungo FC, (2-0) v Coastal Union, (2-1) na Polisi Tanzania huku sare ni (2-2) v Yanga na kichapo ni cha (1-0) v JKT Tanzania.
Katika michezo hiyo, Sven alikusanya pointi 25, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 23 na kuruhusu manane.

DIDIER GOMES DA ROSA
Mfaransa huyu alijiunga na Simba Januari 24, 2021 akichukua nafasi ya Sven ambaye kipindi hicho alijiunga na FAR Rabat ya Morocco.
Katika michezo yake 10 ya mwanzo, Gomes alishinda minane na kutoka sare miwili ambapo ya ushindi ni (2-1) v Dodoma Jiji, (1-0) v Biashara United, (3-0) v JKT Tanzania, (5-0) v Mtibwa Sugar, (1-0) v Mwadui FC, (2-0) v Kagera Sugar na (1-0) v Gwambina.
Mingine ni (3-1) v Dodoma Jiji huku ile miwili ya sare ni (2-2) v Azam FC na (1-1) v Maafande wa Tanzania Prisons ambapo Gomes alivuna pointi 26 katika michezo hiyo.]

PABLO FRANCO MARTIN
Raia huyo wa Hispania alitambulishwa Simba Novemba 8, 2021 akitokea klabu ya Ligi Kuu ya Kuwait ya Al-Qadsia akichukua nafasi ya Gomes aliyeondoka baada ya kutolewa raundi ya kwanza tu ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Katika michezo 10 ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara, Pablo alishinda sita, sare miwili na kupoteza pia miwili huku ya ushindi ni (3-1) v Ruvu Shooting, (2-1) v Geita Gold, (4-1) v KMC, (2-1) v Azam FC, (1-0) v Tanzania Prisons na (1-0) v Mbeya Kwanza.
Michezo ya sare ni (0-0) v Yanga, (0-0) v Mtibwa Sugar huku ile ya kichapo ni (1-0) v Mbeya City na (1-0) v Kagera Sugar ambapo Pablo alikusanya pointi 20 na katika mechi hizo alifunga jumla ya mabao 13 tu na nyavu zake kutikiswa mara sita.

ZORAN MANOJLOVIC MAKI
Kocha huyo mwenye uraia pacha wa Serbia na Ureno alijiunga na Simba Juni 28, 2022 ingawa aliondoka Septemba 6, 2022 kwa kile kilichoelewa na aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu wa kikosi hicho, Barbara Gonzalez kufikia makubaliano ya pande mbili.
Katika kipindi chake cha uongozi, Zoran aliiongoza Simba katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara na kushinda yote akianza na ushindi wa (3-0) v Geita Gold, (2-0) v Kagera Sugar huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao matano bila ya kuruhusu.

JUMA MGUNDA
Baada ya kuondoka Zoran, Simba ilimtangaza aliyekuwa kocha mkuu wa Coastal Union kwa wakati huo, Juma Mgunda Septemba 7, 2022, ingawa kwa sasa anaifundisha Namungo na katika michezo 10 ya mwanzo alishinda sita, sare mitatu na kupoteza mmoja.
Michezo ya ushindi ni (1-0) v Tanzania Prisons, (3-0) v Dodoma Jiji, (5-0) v Mtibwa Sugar, (1-0) v Ihefu SC, (1-0) v Namungo FC na (4-0) v Ruvu Shooting huku ya sare ni (1-1) v Yanga, (1-1) v Singida Fountain Gate na (1-1) v Mbeya City.
Mechi aliyopoteza ni (1-0) v Azam FC ambapo Mgunda katika michezo hiyo 10 alikusanya jumla ya pointi 21, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho kwa wakati alichokiongoza kilifunga mabao 18, huku eneo lake la ulinzi likiruhusu manne tu.

ROBERTO OLIVEIRA ‘ROBERTINHO’
Januari 3, 2023 uongozi wa Simba ulimtambulisha Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuwa kocha mpya kwa mkataba wa miaka miwili.
Katika michezo 10 alishinda minane na kutoka sare miwili ambapo ya ushindi ni (3-2) v Mbeya City, (1-0) v Dodoma Jiji, (3-1) v Fountain Gate, (3-0) v Mtibwa Sugar, (2-0) v Ihefu SC, (2-0) v Yanga, (3-0) v Ruvu Shooting na (6-1) v Polisi Tanzania.
Sare ni (1-1) v Azam FC na (1-1) v Namungo FC ambapo ‘Robertinho’ katika utawala wake alivuna pointi 26, katika michezo 10 ya mwanzo, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 25 na eneo la ulinzi likiruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

ABDELHAK BENCHIKHA
Benchikha alijiunga na kikosi hicho Novemba 24, 2023 akitoka kuipa USM Alger ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Yanga kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya 2-2 na CAF Super Cup mbele ya Al Ahly ya Misri.
Kocha huyo katika michezo yake kumi ya kwanza alishinda saba, sare miwili na kupoteza mmoja.

FADLU DAVIDS
Kwa sasa kikosi cha Simba kinanolewa na Fadlu Davids ambaye alijiunga nacho Julai 5, mwaka na katika michezo yake 10 ya mwanzo tayari ameshinda minane, sare mmoja na kupoteza pia mmoja.
Michezo ya ushindi ni ile ya (3-0) v Tabora United, (4-0) v Fountain Gate, (2-0) v Azam FC, (1-0) v Dodoma Jiji, (1-0) v Tanzania Prisons, (3-0) v Namungo FC, (1-0) v Mashujaa na (4-0) v KMC FC, huku mchezo wa sare ni (2-2) v Coastal Union.
Kichapo kwa Fadlu ni cha bao 1-0 dhidi ya Yanga huku safu ya ushambuliaji ikiwa imefunga jumla ya mabao 21 na kuruhusu matatu.