Fadlu aipata dawa ya Yanga

HOMA ya pambano la Dabi ya Karikoo, imeanza kupanda mapema kwa mashabiki wa Simba na Yanga, kila mmoja akitamba kupta ushindi, japo wale wa Simba wanaonekana kuwa wanyonge mbele ya wenzao kutokana na kupoteza mechi nne mfululizo zilizopita katika mashindano tofauti.

Hata hivyo, kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids ameshtukia jambo na fasta akawatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo akiwaambia kwamba makosa yaliyosababisha timu hiyo kupoteza mechi mbili mfululizo ikiwa chini yake, ameshaipata na Jumamosi wajiandae tu kushangweka.

Pamoja na kuwepo kwa vikao vya hapa na pale zilivyoisha vya mabosi wa klabu hiyo na benchi la ufundi katika kutafuta njia nzuri y Simba kutoka na ushindi Kwa Mkapa mbele ya Yanga, lakini kocha Fadlu amefichua hana presha na mechi hiyo kwa vile ameshagundua kilichowaangusha mwanzoni.

Fadlu aliyepoteza katika Ngao ya Jamii kwa kufunga mchezo wa nusu fainali kwa bao 1-0 la Maxi Nzengeli Agosti mwaka jana kabla ya kulala tena 1-0, baada ya beki Kelvin Kijili kujifunga katika harakati za kuokoa mpira wa Maxi.

Hata hivyo mechi hizo zote mbili, kocha huyo raia wa Afrika Kusini akikumbana na mziki wa Miguel Gamondi ambaye kwa sasa hayupo Yanga baada ya kutimuliwa mwishoni mwa mwaka jana na kuletwa Sead Ramovic ambaye hata hivyo hakudumu sana kabla ya kuajiriwa Miloud Hamdi anayekutana naye.

Gamondi, ndiye aliyeiongoza Yanga katika mechi nyingine mbili za msimu uliopita za Ligi Kuu ambazo aliifunga Simba mabao 5-1 siku ya Novemba 5, 2023 na kuitambia tena 2-1 zilipokutana Aprili mwaka jana na kuifanya Simba icheze mechi nne mfululizo za Dabi bila ushindi mbele ya watani wao.

Simba ilishinda mara ya mwisho katika mechi ya duru la pili la msimu wa 2022-2023 kwa mabao 2-0 Aprili 16, 2023 yaliyofungwa na beki Henock Inonga na Kibu Denis, kisha zilipokutana katika ya Ngao ya Jamii ya msimu uliopita mechi iliisha suluhu ndani ya dakika 120 kabla ya kupigwa penalti ambapo Simba ilishinda 3-1.

Hata hivyo ni kwamba, Fadlu anaenda kukutana na Yanga ya Hamdi ambaye hana muda mrefu tangu aajiriwe kuchukua nafasi ya Ramovic, huku akiwa na rekodi nzuri ya kuiongoza katika mechi saba na kushinda sita kwa idadi kubwa ya mabao na mchzeo mmoja dhidi ya JKT Tanzania ukiisha kwa suluhu.

Katika mechi hizo sita ikiwamo ile aliyoiongoza akiwa jukwaani dhidi ya KenGold akimuacha kocha msaidizi Abdihalim Moallim benchini, Yanga imefunga jumla ya mabao 22 na yenyewe kufungwa mawili matatu.

Kutokana na hali hiyo, kocha Faldu na benchi nzima la ufundi wamekuwa bize na mbinu za kiufundi, kwa lengo la kuhakikisha wanarejea uwanjani kwa nguvu baada ya kupoteza mara mbili msimu huu kwa Yanga akisema ameshazungumza na wachezaji ili kuepuka makosa yaliyowaangusha mechi zilizopita.

“Tunahitaji kuwa bora katika kila eneo,” amesema Fadlu ambaye kikosi chake kimeruhusu mabao machache zaidi (8) katika Ligi Kuu hadi sasa, Yanga ikifungwa tisa, japo mabao ya kufunga Yanga inayo 58 dhidi ya 46 ya watani wao hao.

Katika kuhakikisha wanajifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya Yanga, Fadlu anawaandaa wachezaji wake kupitia programu maalum ya mazoezi na mikakati ya kiufundi.  

“Yanga ni timu inayojua kupambana, lakini hatuwezi kuwa na hofu. Tuna wachezaji bora na ni muda muafaka wa kuonyesha nguvu yetu. Hii ni fursa ya kurejesha furaha kwa mashabiki wetu, walio na maumivu kutokana na matokeo ya michezo iliyopita,” amesema kocha huyo aliyeiongoza Simba kushinda mechi 17 kati ya 21 ilizocheza ikipoteza mara moja na kutoka sare tatu, huku akiivusha timu hiyo katika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrka ikiwa ni timu pekee ya Tanzania iliyosalia CAF.