
Simba imemtangaza mshambuliaji wake Ladack Chasambi kuwa mgeni rasmi katika mechi yake leo dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam wakati huo kocha wake mkuu, Fadlu Davids ametoa msimamo wa benchi la ufundi juu ya mchezaji huyo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Simba imetamba kuwa mchezaji huyo ambaye alijifunga katika mchezo dhidi ya Fountain Gate ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 kuwa ndio mgeni rasmi.
“Mabibi na mabwana karibuni kwenye mchezo wa leo ambao mgeni rasmi ni Mtoto wa Maajabu. #WenyeNchi #NguvuMoja,” ameandika Simba.
Kocha Fadlu Davids amesema kuwa benchi lake la ufundi linamtazama Chasambi kama mchezaji muhimu zaidi kikosini na atakayekuwa msaada mkubwa kwa taifa siku za usoni hivyo litaendelea kumlinda dhidi ya presha na changamoto zozote anazokutana nazo kuanzia pale alipojifunga dhidi ya Fountain Gate.
“Ninamuamini (Chasambi) kwa asilimia mia moja. Ninamchezesha kwa ajili ya matokeo? Hapana, matokeo ni juhudi za kitimu. Hatumpi Presha na tunamlinda sana.
“Ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sio kwa ajili ya Simba tu bali hadi timu ya taifa. Hiki anachopitia kitamkomaza zaidi na kumuendeleza kwa haraka zaidi kwa sababu kucheza timu kubwa kama Simba sio jambo rahisi,” amesema Davids.
katika mchezo dhidi ya Fountain Gate uliochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Chasambi alijifunga bao katika dakika ya 75 baada ya mpira aliorudisha kwa kipa Mousa Camara kushindwa kuokolewa na kujaa wavuni na kufanya matoke ya mchezo huo kuwa ya sare ya bao 1-1.
Kabla ya hapo, Chasambi ndiye alipiga pasi iliyozaa bao la Simba katika dakika ya 57 lililofungwa na Lionel Ateba.