
KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids ameshamaliza kazi aliyioifuta jijini Arusha wkati walipoikabili Coastal Union na kupata ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ambapo Steven Mukwala alifunga hat trick, ikiwa ni ya tatu kwa msimu huu katika Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo anajua kibarua kilichopo mbele yake kwa sasa ni kuikabili Yanga katika pambano la Dabi ya Kariakoo litakalopigwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam likiwa ni pambano la pili kwa msimu huu katika Ligi Kuu na la 114 tangu katika Ligi ya Bara tangu 1965.
Katika kuwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo, Kocha Fadlu amewahakikishia kuwa, kipa Moussa Camara na beki, Fondoh Che Malone wataliamsha katika Dabi ya Kariakoo wikiendi hii Kwa Mkapa.
Nyota hao wawili wa kikosi cha kwanza walikosa pambano la juzi dhidi ya Coastal Union na Simba ilishinda kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ikiwa ni mara ya kwanza kwa wachezaji hao kukosekana hususani kipa Camara na wote walikuwa majeruhi.
Wachezaji hao waliumia katika pambano la Dabi ya Mzizima dhidi ya Azam FC lililoisha kwa sare ya mabao 2-2, Wanalambalamba wakichomoa dakika za jioni bao la pili kupitia mtokea benchi, Zidane Sereri, wakati Simba ikiongoza kwa mabao 2-1 hadi dakika ya 87.
Simba iliyorejea jijini Dar es Salaam inajiandaa kuvaana na Yanga wikiendi hii katika pambano la 114 la Dabi ya Kariakoo katika Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965 na Fadlu amewahakikishia mashabiki na wapenzi wa timu hiyo, nyota hao wawili watakuwepo katika pambano hilo.
Fadlu anaenda katika mchezo huo akiwa na mwenendo mzuri ndani ya ligi baada ya kucheza mechi 21 na kukusanya pointi 54 katika nafasi ya pili, nne tofauti na ilizonazo kinara Yanga yenye pointi 58 kutokana na mechi 22. Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Oktoba 19, 2024, Yanga ilishinda 1-0.
Kocha huyo, aliyeiwezesha Simba kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikijiandaa kuvaana na Al Masry ya Misri mapema mwezi ujao, alisema wachezaji hao hadi Jumamosi watakuwa fiti tayari kwa pambano hilo dhidi ya Yanga litakalopigwa Uwanja wa Mkapa.
“Che Malone na Camara watakuwa tayari kwa Dabi, kwani tuna wiki ya kufanya maandalizi kwa ajili ya mchezo huo, lakini kila mchezaji kwa sasa anayepata nafasi anacheza vizuri,” alisema Fadlu, raia wa Afrika Kusini aliyetua Msimbazi msimu huu kutoka Raja Casablanca ya Morocco na kuongeza;
“Hata mechi iliyopita dhidi ya Coastal unaona alikaa nje Mohamed Hussein, lakini Valentin Nouma akacheza vizuri, kulia kulikuwa na David Kameta ‘Duchu’ akacheza vizuri pia Deborah Mavambo akacheza vizuri sana hivyo naweza kusema kila mchezaji anajua namna ya kutimiza wajibu wake.”
Fadlu aliongeza, kazi kubwa ambayo watafanya kama timu ni kuwa tayari kwa ajili ya mchezo wa Dabi ili kwenda pia kupata ushindi utakaoongeza morali na kutengeneza njia nyeupe ya kwenda kwenye kilele cha mafanikio ambayo ni kutwaa ubingwa wa ligi.
“Tuna mapumziko ya siku moja au mbili ili kupata nafuu kisha tunaanza maandalizi ya mchezo huo dhidi ya Yanga, tunajua itakuwa ni wiki ya kusisimua kwa mashabiki ambayo ni muhimu kwetu sisi kuwafurahisha,” alisema Fadlu.
Camara aliyetumika katika mechi 20 zilizopita za ligi ikiwa ni sawa na dakika 1,800 ameruhusu mabao manane tu akiifanya Simba kuwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi hadi sasa, huku mwenyewe akiwa na rekodi ya clean sheet 15, kama zilizowekwa msimu uliopita na Ley Matampi aliyekuwa Coastal.
Kwa Che Malone anayeitumikia Simba kwa msimu wa pili, amekuwa nguzo imara ya ulinzi ya timu hiyo akishirikiana na mabeki Abdulrazaq Hamza na Chamou Karaboue na alikuwa ametafutiwa daktari maalumu ili kumsaidia apone haraka kabla ya mechi ya Dabi Jumamosi hii.