Fabrice Ngoma ndiye gumzo Morocco

KWA huko nyumbani Tanzania, mashabiki wa Simba huwaambii kitu kwa winga, Ellie Mpanzu Kibisawala kutokana na namna alivyoteka hisia zao tangu alipojiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili la Januari.

Hata hivyo, mambo ni tofauti baada ya timu hiyo kuja Morocco, kwani mashabiki wengi wa soka hapa licha ya kuifahamu Simba, mchezaji anayejulikana sana hapa kwa Wekundu hao ni Fabrice Ngoma.

Umaarufu wa Ngoma umechangiwa kwa kiasi kikubwa na nyota huyo kuwahi kuichezea kwa mafanikio makubwa Raja Casablanca ya hapa kuanzia mwaka 2019 alipojiunga akitokea AS Vita Club ya DR Congo hadi 2022 alipoachana nayo na kujiunga na Al-Fahaheel ya Kuwait.

Akiwa na Raja Casablanca, kiungo huyo alitoa mchango mkubwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2020-2021 na taji la CAF Super Cup mwaka 2019.

Katika maeneo mengi yenye mkusanyiko mkubwa wa watu ambayo Simba imekuwa kinapita, Ngoma amekuwa akiombwa kupiga picha na mashabiki wengi wanaonekana kuwa wa Raja Casablanca.

Baadhi ya mashabiki hao mbali na kupiga picha, wamekuwa wakizungumza zaidi na kiungo huyo ingawa pia wapo ambao wanaonekana kumfahamu vilivyo kocha wa Simba, Fadlu Davids.

Ngoma amekuwa mchezaji aliyechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Simba hadi ikatinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu na katika mashindano hayo amecheza idadi ya mechi 11.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *