FA yampiga rungu Slot, Heitinga kubeba mikoba

Meneja wa Liverpool, Arne Slot atatazama mechi mbili zijazo za timu yake akiwa jukwaani baada ya kupewa adhabu ya kufungiwa mechi mbili na Chama cha Soka England (FA) jana.

Adhabu hiyo imetolewa kutokana na kitendo cha kocha huyo kuwazonga marefa katika mechi dhidi ya Everton, Februari 12, 2025.

Adhabu hiyo haimhusu Slot pekee bali pia meneja msaidizi Sipke Hulshoff ambaye naye alishiriki tukio hilo la kumzonga na kutoa lugha zisizo na heshima kwa refa Michael Oliver.

Mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, iligubikwa na matukio ya vurugu pindi filimbi ya mwisho ilipopulizwa na refa Oliver ambayo yalipelekea timu zote mbili.

Vurugu za mechi hiyo zilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ugomvi uliowahusisha wachezaji Curtis Jones wa Liverpool na Abdoulaye Doucoure ambao wote walionyeshwa kadi nyekundu.

Kuadhibiwa kwa Slot na Hulshoff kunamaanisha benchi la ufundi la Liverpool katika mechi mbili zijazo litasimamiwa na nyota wa zamani wa Everton na timu ya taifa ya Uholanzi, Johnny Heitinga.

Mechi ambazo Slot atazikosa ni dhidi ya Newcastle United na Southampton.

Mbali na adhabu ya kutoruhusiwa kukaa kwenye benchi la ufundi, Slot pia ametozwa faini ya Pauni 70,000 (Sh230 milioni) huku msaidizi wake akitozwa faini ya Pauni 7,000 (Sh23 milioni).

Adhabu hizo pia zimetua kwa timu zote mbili kwa kosa la kushindwa kuchunga wachezaji wao katika mechi hiyo.

Everton imetozwa faini ya Pauni 65,000 (Sh213 milioni) na Liverpool imetozwa faini ya Pauni 50,000 (Sh164 milioni).