EWURA YAKUTANA NA WADAU SEKTA NDOGO YA MAFUTA MWANZA

Na.Mwandishi Wetu-MWANZA

WANANCHI wa Kanda ya Ziwa wametakiwa kutumia Nishati Safi ya kupikia ya Gesi na Umeme ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya Nishati Chafu.

Hayo yameelezwa na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina,wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wadau wa Sekta ndogo ya mafuta yaliyofanyika jijini Mwanza yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Bw.Mhina,amesema kuwa mabadiliko ya matumizi ya nishati si ya mwaka mmoja, bali yanahitaji mpango wa muda mrefu unaojumuisha elimu endelevu na ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo waandishi wa habari.

“Suala la kubadili mtazamo wa wananchi kutoka kutumia nishati chafu ya mkaa na kuni siyo la muda mfupi, linahitaji muda na sasa kamati mbalimbali zimeisha undwa za kuhakikisha huduma na elimu inawafikia wananchi.Pia nishati safi siyo gesi tu kwa sasa kuna mkaa wa kisasa ambao ni rafiki kwa mazingira,”.amesema Bw.Mhina
Aidha ameelezea kuwa safari hiyo ya miaka 10  (2024-2034), ya asilimia 80 iwe inatumia nishati safi ya kupikia,ilianza rasmi mwaka jana, ikiwa na mikakati ya pamoja ya wizara, taasisi na wadau mbalimbali, wakiwemo TAMISEMI, Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha, kuhakikisha elimu inatolewa, vifaa vinapatikana, na sera zinazowezesha matumizi ya nishati safi zinaimarishwa.
Naye Ofisa Biashara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Evalina Ndeji,amewataka washiriki wa semina hiyo kupeleka elimu waliyoipata kwa wananchi, hasa wanawake wanaopika wakiwemo mama ntilie ili waondokane na matumizi ya nishati chafu na kufikia malengo hayo ya miaka 10.
Pia ametoa wito kwa serikali  kupitia EWURA kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi hususani  wa vijijini juu ya matumizi ya nishati safi,kwani wengi wao uelewa bado ni mdogo huku mfano hali ni   eneo analofanyia kazi.
Pia kuona namna ya kupunguza gharama za kujaza gesi ili kuwawezesha wanawake wa kipato cha chini kutumia nishati safi.
Kwa upande wake Ofisa Masoko wa kampuni ya Kayonza LTD Oryx, Joaness Kashaga, amesema  kuwa watu wengi waishio vijijini bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu faida na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesisitiza kuwa kufikia lengo la serikali la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034 kunahitaji uwekezaji  elimu kwa jamii.
“Elimu ndio mkombozi wa wananchi kuacha matumizi ya nishati chafu kama mkaa,hivyo nasisitiza EWURA kutisaidia kutoa elimu na kampeni za kuhamasisha na kuwajengea uelewa wananchi hususani wa vijijini ili waondokane na matumizi ya nishati chafu,”amesema Kashaga.

The post EWURA YAKUTANA NA WADAU SEKTA NDOGO YA MAFUTA MWANZA appeared first on Mzalendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *