Arsenal imejikuta katika wakati mgumu jana baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Everton katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa kwenye uwanja wa Goodison Park.
Arsenal ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Leandro Trossard ambaye alifunga katika dakika ya 34 baada ya kumaliza pasi ya Rahem Sterling.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Arsenal ilienda mapumziko ikiwa inaongoza.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Iliman Ndiaye alifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 49 kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Arsenal, Myles Lewis kumchezea rafu mshambuliaji wa Everton, Jack Harrison katika eneo la hatari.

Baada ya kupata matokeo hayo Arsenal imefikisha pointi 62 zinazoendelea kuiweka katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa EPL ikiwa nyuma kwa pointi 11 dhidi ya Liverpool inayoongoza ikiwa na pointi 73.
Liverpool hadi sasa inahitaji pointi 11 ili iwe bingwa wa EPl msimu huu kwani inatakiwa kushinda mechi nne huku ikiwa imebakiza michezo saba kukamilisha ratiba ya msimu wa 2024-2025 ambapo leo itakuwa na kibarua kigumu ugenini dhidi ya Fulham.

Michezo mingine iliyochezwa jana ilishuhudiwa Aston Villa ikiifunga Nottingham Forest mabao 2-1 kwenye dimba la Villa Park. Mabao ya Morgan Rogers katika dakika ya 13 na Donyell Malen ambaye alifunga dakika ya 15 yalitosha kuipa ushindi Aston Villa wakati bao la kufutia machozi la Nottingham Forest likifungwa na Jota Silva katika dakika ya 57.
Ushindi ilioupata Aston Villa unaifanya kusogea mpaka nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha jumla ya pointi 51 katika michezo 30 iliyocheza .

Wolverhampton imeifunga Ipswich Town mabao 2-1 ilipokuwa ugenini kwenye uwanja wa Portman Road.
Crystal Palace ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brighton, mabao ya Jean Mateta ambaye alifunga katika dakika ya tatu pamoja na Daniel Monoz aliyepachika bao dakika ya 55.

Katika mchezo huo ilishuhudiwa mwamuzi wa mchezo huo Anthony Taylor akitoa kadi tatu nyekundu ambapo mbili zilienda upande wa Crystal Palace kwa Eddie Nketiah aliyeonyeshwa katika dakika ya 78 huku nyingine ikionyeshwa kwa Marc Guehi dakika ya 90 wakati kwa upande wa Brighton, beki, Jan Paul Van Hecke alionyeshwa katika dakika za nyongeza.

West Ham ililazimishwa sare ya mabao 2-2 kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya Bournemouth. Katika mchezo huo West Ham ndiyo ilitoka nyuma na kusawazisha mabao mawili iliokuwa imefungwa.
Ligi Kuu ya England itaendelea tena leo katika viwanja vinne tofauti ambapo Manchester United itakuwa nyumbani ikiwakaribisha Manchester City, Tottenham itakuwa nyumbani dhidi ya Southampton, Liverpool itakuwa ugenini dhidi ya Fulham wakati Brentford itakuwa nyumbani dhidi ya Chelsea.