Ni usiku uliogubikwa na nyakati za furaha, huzuni, shangwe, vurugu na historia ya aina yake wakati Everton ilipotoka sare ya mabao 2-2 na Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL), jana Februari 12, 2025 katika Uwanja wa Goodison Park.
Bao la kusawazisha la jioni la James Tarkowski lililofungwa katika dakika ya mwisho ya nyongeza ya mchezo huo, liliihakikishia Everton sare hiyo ambayo imekuwa na maana kubwa kwao huku ikiinyima Liverpool fursa ya kuandika historia ya aina yake katika mechi hiyo ya watani wa jadi wa kitongoji cha Merseyside maarufu kama ‘Merseyside Derby’.
Ikiongoza kwa mabao 2-1, Liverpool ilikuwa inakaribia kuandika historia ya kupata ushindi mara nyingi zaidi kwenye Uwanja wa Goodison Park katika mechi ya watani wa jadi ya Merseyside lakini bao hilo la Tarkowski liliifanya Everton ilinde heshima nyumbani.
Ingekuwa ni maumivu zaidi kwa Everton ikiwa ingepoteza mechi ya jana kwa vile ilikuwa ya mwisho ya watani wa jadi wa Merseyside kuchezwa katika Uwanja wa Goodison Park kwa vile baada ya msimu huu kumalizika, utabomolewa na kujengwa mpya ambao Everton itautumia kwa mecho zake za nyumbani.
Kabla ya timu hizo kukutana jana, zilikuwa zimecheza mechi 82 za watani wa jadi wa Merseyside ambapo kila moja imepata ushindi mara 41 hivyo ambayo ingepata ushindi jana maana yake ingeondoka na historia tatu ya ubabe katika mechi baina yao uwwnjani hapo.
Everton ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 11 kupitia kwa Beto lakini dakika ya 16, Liverpool ilisawazisha kwa bao lililofungwa na Alexis Mac Allister na Mohamed Salah akafunga la pili katika dakika ya 73 na wakati ikionekana Liverpool inakaribia kuchukua pointi tatu, Tarkowski aliwainua vitini mashabiki wa Everton kwa bao lake la dakika ya mwisho ya tisa zilizoongezwa.

Ni mechi iliyoshuhudiwa refa Michael Oliver akitoa kadi nne nyekundu, mbili kwa wachezaji Curtis Jones wa Liverpool na Abdoulaye Doucoure wa Everton huku wengine wawili wakiwa ni kocha wa Liverpool, Arne Slot na msaidizi wake Sipke Hulshoff.
Sare hiyo imeifanya Liverpool iendelee kuongoza msimamo wa EPL ikifikisha pointi 57, saba zaidi ya zile za Arsenal inayoshika nafasi ya pili wakati Everton imepanda hadi katika nafasi ya 15 ikifikisha pointi 27.
Miaka 133 ya kipekee Goodison Park
Kitendo cha kutokubali kufungwa na Liverpool ndani ya Goodison Park kilimaanisha kuwa Everton imeukataa unyonge mbele ya watani wao hao wa jadi kwa miaka 133 tangu ulipojengwa mwaka 1892.
Uwanja huo unaingiza idadi ya mashabiki 39,414 kwa sasa lakini kutokana na mahitaji ya mashabiki, klabu hiyo imeamua kujenga uwanja mpya ambao utaingiza idadi kubwa zaidi ya mashabiki.
Gharama za ujenzi wa uwanja wa Goodison Park wakati huo zilikuwa ni Pauni 3,000.
Idadi kubwa ya mabao kufungwa katika mechi moja kwenye Uwanja huo ni 12 yakipatikana katika mchezo ambao Everton ilishinda kwa mabao 9-2 dhidi ya Sheffield Wednesdaya