
MSHAMBULIAJI wa Makadi FC, Oscar Evalisto amesema mkataba wake na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Misri umemalizika na sasa anasikilizia dili nono zaidi kutoka timu hiyo au nyingine itakayomhitaji.
Evalisto alisajiliwa hivi karibuni na timu hiyo akitokea Mlandege FC ya Zanzibar kwa mkataba wa miezi sita, alikuwa kwenye kikosi cha Mlandege kilichoifunga bao 1-0 Simba, kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi Cup msimu uliopita.
Akizungumza na Mwanaspoti, akiwa nchini kwenye likizo yake Evalisto alisema tayari ameanza mazungumzo na klabu hiyo juu ya kuongeza mkataba mpya baada ya ule wa awali kutamatika hivi karibuni.
Aliongeza, pia amepokea ofa za nchi hiyo na hapa Tanzania ingawa wakala wake anaangalia ipi inafaa ili aweze kumwaga wino.
“Kwa sasa nipo nyumbani Iringa timu ninayochezea imemaliza nafasi ya nane kwa hiyo tumemaliza msimu ila kuna zile zinazocheza Play-off wao wanaendelea na michezo iliyosalia nashukuru ulikuwa msimu sio mbaya wala sio mzuri, nilicheza mechi tatu nikafunga mabao mawili na asisti,” alisema Evalisto na kuongeza.
“Baada ya mkataba kuisha, Rais wa timu pamoja na kocha waliniita kuzungumzia juu ya mkataba mpya lakini wakala wangu aliwaambia tunapaswa kusubiri hivyo naendelea kusikilizia japo kuna ofa za hapa Bongo.”