Euro-Med Human Rights Monitor: Israel inanyonga raia wa kaskazini mwa Gaza

Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Med limesema kwamba limesajili makumi ya kesi za mauaji ya kukusudia na vitendo vya kunyongwa raia vinavyofanywa na jeshi la Israel Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, ndani ya mfumo wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yanayoendelea kwa zaidi ya miezi 13.

Shirika la Euro-Med Human Rights Monitor limeeleza katika taarifa yake kwamba, jeshi la Israel limeendelea kwa muda wa siku 43 kufanya uvamizi na mashambulizi ya tatu ya kijeshi dhidi ya eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na wakazi wake, likifanya ukatili wa kutisha ambao ni pamoja na kuua raia, kuwatishia na kuwafukuza kutoka kwenye makazi yao na kuwalazimisha kuhama eneo hilo, kama sehemu ya operesheni kubwa zaidi ya kuwalazimishwa watu kuwa wakimbizi katika zama za sasa.

Euro-Mediterranean Human Rights Monitor inayojiarifisha kama shirika huru, lisilo la faida la linalotetea haki za binadamu Ulaya, Mashariki ya Kati na eneo la Afrika Kaskazini, imetangaza kuwa, kati ya jinai nyingi zilizofanywa na wanajeshi wa Israel ni pamoja na kulipua nyumba juu ya vichwa vya wakazi wake na kuwaua kwa umati, kuua watu katika vituo vya wakimbizi na kulenga mikusanyiko ya raia na magari. Timu ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu la Ulaya pia imerekodi kesi za mauaji ya moja kwa moja na mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na wanajeshi wa Israel dhidi ya raia bila sababu yoyote.

Watoto wa Gaza

Miongoni mwa kesi zilizosajiliwa na timu ya Euro-Med ni mauaji ya jeshi la Israel dhidi ya Khaled Mustafa Ismail Al-Shafi’i (umri wa miaka 58) na mtoto wake mkubwa Ibrahim (umri wa miaka 21) baada ya kuwafyatulia risasi ndani ya nyumba yao, mbele ya familia yao huko Beit Lahia, Jumatano iliyopita.

Euro-Med imeripoti kuwa maelfu ya Wapalestina waliozingirwa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza wanasumbuliwa na njaa na hofu, na wale wanaojeruhiwa mara nyingi hawawezi kuhamishwa kwa ajili ya matibabu au hata kutibiwa uwanjani, na idadi yao kubwa hufariki dunia polepole kutokana na ukosefu wa huduma ya matibabu ya kuokoa maisha.