
Chama kikuu cha upinzani nchini Ethiopia, Tigray People’s Liberation Front (TPLF), siku ya Alhamisi kimeelezea maagizo kutoka kwa Tume ya Uchaguzi ya kupiga marufuku shughuli za kisiasa kama “tishio kubwa” kwa mchakato wa amani.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
TPLF iliongoza mapinduzi yaliyopindua serikali ya kimabavu ya Derg mwaka 1991 na kisha kutawala Ethiopia hadi mwaka 2018, wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alichukua madaraka na kukiweka kando chama hicho.
TPLF iliendesha vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya serikali ya shirikisho kutoka mwaka 2020 hadi mwaka 2022, ambayo iligharimu maisha ya watu wapatao 600,000.
Katika barua kwa Umoja wa Afrika, TPLF imeitaka AU kuishinikiza serikali ya Ethiopia kusitisha utekelezaji wa marufuku hiyo.
Kulingana na ripoti hiyo, uamuzi huu “unainyima TPLF haki iliyokuwa imepata tena kutokana na makubaliano ya Pretoria na ni tishio kubwa kwa misingi ya mchakato wa amani.”
Ingawa mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Pretoria ulimaliza vita mnamo mwezi wa Novemba 2022, eneo la Tigray limekatishwa tamaa na kutotekelezwa kwa masharti yake, ikiwa ni pamoja na kurejea kwa takriban watu milioni moja waliokimbia makazi yao kutokana na vita.
Chama hicho kilichotawala siasa za Ethiopia kwa takriban miaka 30, kilifutiwa usajili rasmi siku ya Jumatano kwa kushindwa kufanya mkutano mkuu.
Hatua hiyo inafuatia miezi kadhaa ya mivutano ya kisiasa katika eneo la kaskazini la Tigray na inakuja kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini Ethiopia kabla ya mwezi Juni 2026.
TPLF ilikuwa tayari imesimamishwa kwa muda wa miezi mitatu mwezi Februari na kutishia kufutiwa usajili ikiwa haitachukua “hatua za kurekebisha” ndani ya miezi mitatu.
Bado chama hiki kinaweza kutuma maombi ya kujiandikisha tena kwa uchaguzi wa mwaka 2026.
Malumano ndani ya TPLF yalisababisha makabiliano mapema mwaka huu na kuondolewa kwa kiongozi wa mkoa Getachew Reda, ambaye amejiunga na serikali ya shirikisho.
Uhusiano pia umezorota kati ya Ethiopia na Eritrea, nchi ambayo inashiriki mpaka mrefu na Tigray.