
Ethiopia inapanga kusafirisha takriban megawati 100 za umeme kwa Tanzania kupitia Kenya, ikiwa ni hatua muhimu ya ushirikiano wa nchi za eneo hilp katika masuala ya maendeleo.
Mtendaji Mkuu katika Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Kenya, John Mativo, amenukuliwa akisema kuwa, umeme utazalishwa Sodo, kusini mwa Ethiopia, kisha kupelekwa Suswa nchini Kenya, na baada ya hapo utasafirishwa hadi Arusha kaskazini mwa Tanzania.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa mikataba kati ya Ethiopia na Tanzania, baadaye kati ya Kenya na Tanzania, imetiwa saini ili kufanikisha mradi huo.
Hapo awali, Shirika la Umeme la Ethiopia (EEP) lilisema kuwa mauzo ya nishati ya nchi hiyo yalifikia dola milioni 140 katika mwaka wa fedha wa 2016, na kuashiria ongezeko la 16% kutoka mwaka uliopita. Ashebir Balcha, Mkurugenzi Mtendaji wa EEP, wakati wa mkutano na waandishi wa habari, alihusisha ukuaji huo na ongezeko la mahitaji ya nishati, hasa kutokana na uchimbaji wa data, ambao ulichangia dola milioni 27 kwa jumla ya mapato ya nje.
Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye wakazi wengi zaidi wasio na umeme barani Afrika na hivyo inahitaji kununua umeme kutoka nje kukidhi mahitaji yake.