Erdogan: Marekani inayatumia makundi ya kigaidi katika eneo kudhamini usalama wa Israel

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema, Marekani inayatumia makundi ya kigaidi katika Mashariki ya Kati kwa ajili ya kudhamnini usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Erdogan ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari waliokuwamo ndani ya ndege yake wakati akirejea Uturuki kutoka Russia alikohudhuria mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa BRICS na akasisitiza kwa kusema: “ni ukweli unaojulikana wazi sasa kwamba Marekani inayatumia makundi ya kigaidi katika eneo kwa maslahi yake na kwa ajili ya usalama wa Israel”. 

Aidha, Rais wa Uturuki amesema nchi yake imeanzisha mpango chini ya Umoja wa Mataifa wa kuiwekea Israel vikwazo vikubwa vya silaha, wakati mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Ghaza na Lebanon yakiwa yanaendelea kuteketeza roho za mamia ya watu kila siku.

Erdogan

Erdogan amebainisha kwamba idadi ya nchi zinazounga mkono wito wa Ankara wa kuuwekea vikwazo vya silaha utawala haramu wa Israel inaongezeka.

Ameongezea kwa kusema: “tuna matumaini ya kufanikiwa katika hili katika sura yaa Muungano wa Ubinadamu na kufungua mlango wa amani ya kudumu”.

Kuhusu shambulio la kigaidi lililofanywa na kundi la PKK kwenye makao makuu ya Sekta ya Anga ya Uturuki (TAI) katika mji mkuu Ankara, ambalo liliua watu watano na kujeruhi wengine 22, Erdogan amesema, Uturuki inaendelea na juhudi zake za “kuukausha kikamilifu ugaidi kwenye chanzo chake”.

Baada ya shambulio hilo, jeshi la Uturuki na shirika la intelijensia la nchi hiyo zilianzisha mashambulizi ya anga katika maeneo ya PKK/YPG kaskazini mwa Iraq na Syria.

“Magaidi ni vibaraka. Lengo letu ni kuwa na Uturuki isiyo na ugaidi,” amesisitizaa Erdogan na kuongezea kwa kusema: “hatutalegeza msimamo juu ya hili”…/