
London, England. Timu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu England (EPL) ni miongoni mwa nne zilizopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu baada ya utabiri uliofanywa na kampuni ya takwimu ya Opta kuzipa asilimia kubwa ya kutwaa ubingwa huo kulinganisha na timu za ligi nyingine.
Timu hizo ni Liverpool na Arsenal ambazo zimeingia katika kundi la timu nne zinazoongoza kwa kupewa nafasi kubwa ya kupata taji la mashindano hayo yenye hadhi na thamani kubwa zaidi kwa soka la ngazi ya klabu barani Ulaya.
Liverpool inayonolewa na kocha Arne Slot ndio imetabiriwa kuwa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa ambapo imepewa asilimia 17.2 ya kuondoka na taji la mashindano hayo msimu huu.
Timu inayopewa nafasi ya pili ni Barcelona ambayo Opta imeipatia asilimia 15.4 za kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu.
Katika hatua ya 16 bora, Barcelona imepangwa kukutana na Benfica na iwapo itasonga mbele, katika robo fainali itacheza na mshindi wa mchezo baina ya Borussia Dortmund na Lille.
Inayoshika nafasi ya tatu kwa asilimia za kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu kwa mujibu wa utabiri wa Opta ni Arsenał.
Timu hiyo inayonolewa na kocha Mikel Arteta, katika hatua inayofuata imeangukia kwa PSV na iwapo itafanikiwa kusonga mbele, itakabiliana na mshindi baina ya Real Madrid na Atletico Madrid.
Nafasi ya nne katika utabiri huo imeangukia kwa miamba ya Ligi Kuu ya Italia, Inter Milan ambayo yenyewe imepewa asilimia 12.7.
Katika hali ya kushangaza mabingwa watetezi na wa kihistoria wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid wamewekwa katika nafasi ya tano kwenye utabiri huo wakipata asilimia 11.6.
Inayofuatia baada ya Real Madrid ni PSG ambayo imepewa asilimia 8.8 ikifuatiwa na na Bayer Leverkusen ambayo yenyewe imepewa asilimia 5.8 za kutwaa ubingwa na Bayern Munich imejikuta ikipewa asilimia 4.8.
16 bora Ligi ya Mabingwa Ulaya
Aston Villa vs Club Brugge
PSG vs Liverpool
Arsenal vs PSV
Real Madrid vs Atletico Madrid
Benfica vs Barcelona
Borussia Dortmund vs Lille
Bayern Munich vs Bayer Leverkusen
Feyenoord vs Inter Milan