Enzo Fernandez aweka rekodi Chelsea ikiichapa Tottenham

London, England. Kiungo mshambuliaji wa Chelsea, Enzo Fernandez ameisaidia timu yake kupata ushindi baada ya kufunga bao pekee katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Fernandez ameingia kwenye rekodi hiyo baada ya kuwa kiungo wa tatu kuifunga Tottenham katika michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini baada ya Roberto Di Matteo kufanya hivyo katika msimu wa 1996-1997 na Gus Poyet ambaye alifanya hivyo msimu wa 1998-1999.

Muargentina huyo alifunga bao katika dakika ya 50 akiunganisha wavuni mpira kwa kichwa uliopigwa krosi na Cole Palmer. Hadi dakika 90 zinamalizika Chelsea iliondoka kifua mbele dhidi ya Tottenham.

Ushindi huo unaifanya Chelsea kusogea hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikifikisha jumla ya pointi 52 ikizishusha chini Manchester City na Newcastle United.

Mpaka sasa Chelsea imecheza jumla ya michezo 30 ya Ligi Kuu ambapo imeshinda mechi 15, imepoteza mechi nane na kupata sare mechi saba huku ikiwa imefunga mabao 54 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 37.

Chelsea imesalia na michezo minane kabla ya kukamilisha msimu huku ikipambana kumaliza nne bora ambapo idadi ya pointi 52 ilizonazo bado haziipi uhakika wa kumaliza kwenye nafasi hiyo kwani Newcastle United bado ina mchezo mmoja mkononi ikiwa na pointi 50 ambapo ikishinda itafikisha pointi 53 mpaka nafasi ya nne na kuiondoa Chelsea.

Katika michezo minane ambayo Chelsea imebakiza itakabiliana na Brentford, Ipswich Town, Fulham, Everton, Liverpool, Newcastle United, Manchester United na Nottingham Forest.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *