Elimu yetu inaandaa watu wenye hekima na busara?

Tuanze na msemo huu wa Wamarekani wa asili ambao wazungu wa Ulaya waliwaita kimakosa kwa jina la Wahindi wekundu. Hawa wana msemo huu: ‘’Chochote utakachofanya angalia kitawaathiri vipi vizazi vinne vijavyo?

Kwa mfano kama tunataka kufanya kilimo mahali fulani, au tunataka kujenga nyumba sehemu hiyo, au tunataka kujenga barabara itoke huku iende kule, tufikirie kwa kina mambo haya yatawaathiri vipi wajukuu wa watoto wetu?

Msemo huo wa busara ndio unaotungoza katika tafakari ya leo inayolenga kuonyesha kwamba elimu bora tunda lake ni hekima na busara.

Elimu bora ni lazima ituonyeshe ni jinsi gani mambo yote tunayoyafanya sasa yatawaathiri wenzetu miaka 100 au 200 ijayo.

Kwa maneno mengine, elimu hii inapaswa kutuonyesha pasipo shaka kwamba tuna uhusiano wa karibu sana, uhusiano wa kiutu na wenzetu wa miaka mingi ijayo.

Kwa miaka mingi elimu yetu Tanzania imesisitiza kukariri maarifa ya kila aina ili mwishowe mhitimu ashinde mtihani, apate ajira ya kumpa kipato.

Katika elimu hiyo, sijaona kwamba ilikuwepo nia ya makusudi ya kuwaivisha wanafunzi katika hekima na busara.

Hiyo ndiyo elimu niliyopitia mimi hadi nilipokuwa nafanya masomo na utafiti katika somo la falsasa, bahati nzuri nikakutana na profesa mmoja ambaye alielewa vizuri uhusiano wa msingi uliopo kati ya elimu na busara.

Kati ya walimu zaidi ya 30 walionifundisha katika maisha yangu, huyu ndiye mwalimu wa kweli. Apumzike kwa amani.

Hata elimu yetu ya sasa, pamoja na huu mtalaa mpya, sijaona kwamba kuna misingi bora ya kujenga wanafunzi wenye busara na hekima.

Nimeona vitabu vya darasa la tatu na nne vilivyo na kichwa hiki: Historia ya Tanzania na Maadili.

Katika hivyo vitabu sikuona viashiria halisi vinavyowatayarisha wanafunzi wetu wawe watu wenye busara na hekima.
Yaani, kazi bado ipo, hata kama tunaelekea kwenye elimu ya ufundi, amali na elimu vitendo. Hili jambo la hekima na busara silioni lipo katika mitalaa hii mipya ya sasa.

Tunahitaji elimu ipi?
Nitaeleza sasa aina ya ufundishaji na ujifunzaji wa elimu ambayo itawajenga wanafunzi wawe na busara na hekima. Mtaalamu wa elimu, John P. Miller, profesa wa chuo kikuu cha Toronto, Canada, anasema elimu inayowatayarisha wahitimu wawe na hekima na busara, sharti iwaonyeshe wanafunzi uhusiana wa karibu katika haya yafuatayo:

Uhusiano kati ya mtu na mtu mwingine; uhusiano kati ya sisi binadamu na dunia au mazingira yanayotunzunguka; uhusiano kati ya jamii hii na nyingine (nchi hii na nchi nyingine, taifa hili na taifa lingine).

Pia, uhusiano kati ya yale tunayoyawaza (seeing the connections in our thinking, the way I think now and the way I thought yesterday); uhusiano kati ya akili na mwili, na uhusiano kati yetu na roho zetu, ambao tunauita wakati mwingine, ulimwengu wa roho.
Hebu niambie msomaji: ulikwishaona katika elimu uliyopata mambo hayo sita, au hata mojawapo?

Nimeandika katika makala zangu kwamba mojawapo ya misingi ya falsafa ya Kiafrika ni jinsi kila kitu na kila mwanadamu alivyo na muunganiko na kila kitu kingine (tumeunganika na kila kitu, tuna ujamaa na kila kitu, na tunategemeana
Tuangalie maana ya hekima na busara: John P. Miller anasema kwamba busara si mkusanyiko mkubwa wa maarifa ya kila namna, bali ni kuwa na maono ya ndani (insight), unyenyekevu (humility), na upendo (love).

Mtu mwenye busara huona undani wa vitu na maisha kwa macho ya rohoni, huona zaidi ya kile kinachoonekana kwa macho ya mwili, husikia mwangwi wa mambo ambayo masikio yake mawili hayasikii na huona kile kilicho nyuma ya pazia.

Msemo huu wa wale Wamarekani wa asili nao unakoleza maana ya hekima na busara: ni mtu kichaa tu anayefikiri kwa kichwa chake.

Ni jamii kichaa inayofikiria kwa kichwa tu. Lakini mtu au jamii yenye busara hufikiri kwa akili (kichwa) na kwa moyo.

Kwa mfano kama kiongozi fulani anatayarisha mkataba wa kutoa msitu wetu kwa mwekezaji wa ng’ambo, akifiri kwa kichwa tu ataona hela nyingi zitaingia, lakini akiongeza kufikiri kwa moyo, ataona jinsi vizazi vyetu vijavyo vitakavyokuwa watumwa kwa mwekezaji huyo.

Ataona kwamba mkataba huo hauna masilahi kwa vitukuu vyake miaka 100 ijayo. Atasukumwa na upendo wa jamii yake kuachana na mkataba huo wa kinyonyaji.

Mtu mwenye hekima na busara
Sasa turudi kwa sifa ya kwanza ya mtu mwenye hekima na busara: anaona kwa macho ya roho uhusiano kati yake na binadamu mwingine.

Ataelewa fika kwamba huyu binadamu mwingine ni ndugu yangu. Nimpende, nimjali, nimsaidie. Hakuna njia ya mkato hapa.

Ukitaka kupima utu wa mtu, utu wa jamii, utu wa Serikali, angalia jinsi wanavyomjali mtu mwingine, hasa yule aliyedharauliwa, yule maskini, yule asiyeweza kujisaidia. Kwa kipimo hiki wengi tutashindwa mtihani.
Watu waliotukuka katika historia, walio na utu ulio mkubwa kuliko wanavyoonekana ni kama wazazi wangu.

Hawa walinifundisha nisiwe mchoyo kwa yeyote na nisichukue kisicho changu hata siku moja. Wengine walio na utu huo ni Mama Teresa wa Kalkuta, India, yeye aliwaokota maskini barabarani akawakumbatia, akawapeleka nyumbani, akawalisha, akawatibu.

Yupo Nelson Mandela aliyekuwa tayari kufa ili wananchi wenzake wapate uhuru; Mwalimu Julius Nyerere, Rais wetu wa kwanza, aliyependa kuitwa ndugu, na wala si kuitwa mheshimiwa, mtukufu au bosi. Aliondoka duniani bila akaunti ya fedha benki na wengine kama hao.
Hao ni mifano ya watu waliopata elimu bora. Ni watu wenye hekima na busara. Wana upendo, unyenyekevu na maono ya roho.
Pili, na la mwisho kwa leo: mtu mwenye busara anaelewa fika uhusiano wa msingi uliopo kati yake na mazingira yake na dunia inayomzunguka.

Anaelewa kwamba dunia inayomzunguka ndiyo nyumba yake. Ikiungua, ataungulia humo ndani. Ikiwa bora, ni faida yake. Hivyo dunia ni ndugu yake wa karibu. Ni mwenzake.

Binadamu tumekosa busara hii, angalia mabadiliko ya tabia nchi yanavyotuathiri vibaya. Sasa tuhakikishe wahitimu wetu wana busara ya aina hii.