
Tuanze na uzoefu wangu utotoni. Naamini uzoefu huu utakuwa ni wa kawaida kwa kila mtoto bila kujali kabila au taifa lake. Mtoto mdogo kwa kawaida huanza kuona mambo mbalimbali katika mazingira yanayomzunguka.
Kwa wale kama mimi tuliokulia kijijini, tulipitia mazingira ya kilimo, ufugaji, uvuvi, uwindaji na kadhalika. Akili yetu ya kitoto ilituonyesha kwamba yote yaliyotuzunguka yalihusiana vizuri tu.
Kwa maneno mengine tuliona yafuatayo bila kufikiria kwamba yametanganishwa kimsingi (unconsciously and preconsciously): mimi niliona na kuelewa kwamba ng’ombe, mbuzi na kondoo wanakula majani, niliona kwamba sisi wanadamu tulikula mboga, nafaka, matunda na nyama, niliona kwamba mimea, misitu na vichaka vilikuwa chanzo cha chakula chetu wanadamu na cha wanyama wetu.
Kwa wale watoto waliokulia kando ya mito, maziwa au bahari, waliona jinsi wazazi wao walivyotegemea mazingira hayo kupata samaki kwa chakula na jinsi maji yalivyokuwa msingi wa maisha yao.
Kama ulikulia katika jamii ya kifugaji, uliona jinsi wanyama walivyotegemea majani na jinsi mvua zilikuwa sehemu muhimu katika maisha ya binadamu na wanyama.
Kwa kufupi, utotoni tuliona jinsi viumbe vyote vinavyotegemeana. Binadamu tulihitaji mimea kwa chakula, dawa, nyumba na kadhalika. Tulihitaji mvua na hali inayogetegemeza mimea na viumbe wengine wote.
Siku moja bibi yangu mzaa baba akaniuliza: eti mjukuu wangu, unadhani wewe na huu mgomba wa ndizi, ni nani anamhitaji mwingine zaidi? Haraka haraka, kwa vile nilijiona mimi ni binadamu nikajibu kwamba mgomba unanitegemea mimi niutunze, niupalilie na kadhalika.
Bibi akanijibu: hii migomba haituhitaji sisi wanadamu, ilikuwepo na itaendelea kuwepo baada ya sisi wanadamu kutoweka. Hii miti, misitu, vichaka na maji yaliyotuzunguka imekuwepo hata kabla ya wanadamu kuwa duniani.
Ndipo hapo nikaanza kuelewa kwamba sisi wanadamu tunaihitaji migomba na mazingira mengine yaliyotuzunguka. Nikajifunza kuuheshimu mgomba. Nikajifunza kuipa heshima miti na misitu iliyotuzunguka utotoni. Haya yote nilijifunza bila kufikiri sana (unconscious learning).
Naamini kwamba watoto wengi duniani, hasa wa vijijini, wanajifunza yote haya bila mzazi au mlezi kuwaketisha watoto darasani au kuwaambia: kaeni chini niwapatie somo.
Haya yote tulijifunza nyumbani, mashambani, misituni, na katika mazingira ya ufugaji, uvuvi, ufundi, katika sherehe, katika misiba, na katika hali za kawaida za maisha.
Hatukupewa mitihani, lakini tulijifunza, tulikosea, na tulikosolewa huko huko mashambani na mahali pengine. Dunia yetu ilikuwa ndiyo somo kuu na nyumbani na mashambani kulikuwa ndilo darasa ya siku hizo.
Utangulizi huu unatuonyesha kwamba ile falsafa ya Kiafrika ya mviringo ni ya msingi katika fikra za mababu zetu. Naiita falsafa ya mviringo.
Mababu zetu walielewa kwamba dunia yote ya binadamu, wanyama, udongo, miti, vichaka, ndege, wadudu, mito, mabonde, milima, vilima na kadhalika, vyote vinahusiana, vinategemeana, na vimeunganika (interrelated, interdependent, and interconnected).
Nilipoingia chekechea nilikuwa na msingi huu wa mawazo. Niliona dunia kama kitu kimoja kilicho na uhusiano wa msingi, niliona dunia kama uwanja wa watu na vitu vinavyotegemeana, na vilivyoungana.
Pia kuna hili: niliona na kuelewa kwamba Imani yetu ya jadi kwa Muumba wa Yote ilikuwa sehemu ya yote hayo niliyoyaelewa. Nilielewa pia nafasi ya utawala wa wakati huo na nafasi ya wazazi na walezi katika kulea jamii, yote haya yalikuwa sehemu nyeti ya hiyo falsafa ya mviringo.
Mwalimu wetu wa chekechea alikuwa naye mbobezi wa falsafa hii hivyo malezi yake kwa kiasi kikubwa yalijikita katika falsafa hiyo.
Lakini hapa ndipo sisi watoto tulianza kupewa sumu ya mfumo wa elimu iliyotoka Ulaya na Marekani kwamba kuna somo linaloitwa dini, kuna lugha, kuna historia, kuna jiografia, kuna kemia, fizikia, elimu viumbe na kadhalika.
Hii elimu ya kikoloni ya kutofautisha na kugawanya ulimwengu katika vipande, ati kwa lengo la kusoma masomo mbalimbali, ndiko kumekuwa sumu kubwa ya kuharibu falsafa yetu ya asili ya mviringo, ambayo ilituonyesha kwamba kila kitu ulimwenguni pamoja na binadamu wote vinahusiana, vinategemeana na vimeunganika (interrelated, interdependent, interconnected).
Elimu hii ilitutoa katika reli sahihi ya kuona dunia kama kitu kimoja ikatuingiza katika mfumo mbovu wa kushindwa kuona uhusiano uliopo ulimwenguni.
Ni elimu hii mbovu imetufanya tuwe wabinafsi kupita maelezo, tunashindwa kuona jinsi tunavyotegemeana, tunashindwa kuona utu wa wenzetu na uzito wa mazingira yaliyotuzunguka, tunashindwa kuona madhara ya utawala mbovu kwa masilahi ya wote na uzito wa mazingira.
Ni katika mazingira haya ya elimu mbovu wamejitokeza wataalamu wachache wa elimu wanaotuasa kwamba tukiendelea na elimu hii ya kugawanya dunia katika vipande, eti ni elimu ya masomo mbalimbali, tunaelekea kujiangamiza wenyewe pamoja na dunia yetu.
Hatuhitaji ushahidi wa maangamizi haya: tunaona na kushuhudia matatizo makubwa ya sana katika kile tunachokiita tabia nchi, climate change.
Watalaamu hawa kama vila Profesa John P. Miller, wanasisitiza kwamba tubadilishe kabisa mfumo huu wa kutenganisha masomo na kuyafundisha katika mfumo tofauti unaozingatia ile falsafa ya mwunganiko ulio ulimwenguni.
Elimu hii itasaidia wanafunzi wetu waelewe kwamba binadamu tunagemeana na ubinafsi utatuangamiza. Kama wenzetu wa Gaza au Ukraine wanaumia ni sisi tunaumia wote, wale ni ndugu zetu. Kama bahari ikichafuliwa huko Japan na Marekani, sisi hapa Tanzania mwishowe na sisi uchafu huo utatufikia.
Waingereza wana msemo: What goes around, comes around, yaani, kile kinachoendelea huko, iko siku kitatufikia huku tuliko. Hivyo tuamke: tufumue kabisa huu mfumo wa elimu unaogawanya dunia katika vipande, ati ni mfumo wa masomo mbalimbali.
Masomo yetu kama yalivyo sasa yanaugawanya ulimwegu vipande vipande, yanagawanya ule msingi wa umoja wa ubinadamu wetu, na mwishowe tunakuwa na jamii isiyojali masilahi ya wengine, tusiojali uzito wa kuheshimu, kutunza na kuendeleza mazingira yetu.
Katika makala itakayofuata nitapendekeza mfumo bora zaidi wa kufundisha haya masomo tofauti kwa namna inayowapa wanafunzi fursa ya kuelewa kwamba dunia yetu ni kitu kimoja kilichounganika na hatuna budi kuheshimu na kulinda mwunganiko huo. Francis wa Assisi (1182-1242) anasema: milima ni ndugu zetu, jua ni kaka yetu, maji ni dada yetu.