Elimu inavyoweza kuchochea ujumuishi huduma za kifedha

Kujenga ujuzi wa kifedha ni ufunguo muhimu wa kuongeza ujumuishi katika matumizi ya huduma rasmi za kifedha. Kadiri watu wengi wanavyozidi kuelewa dhana za msingi za fedha, mfano kuweka akiba, kupanga bajeti, kuwekeza, kutuma na kupokea fedha kidijitali na mengine ndivyo huduma za kifedha zinavyohitajika zaidi.

Utafiti umeonyesha kuwa watu wenye ujuzi na maarifa ya kifedha wana uwezo mkubwa wa kuepuka vitendo vya udanganyifu wa kifedha na mipango yenye nia mbaya. Katika chapisho lao, Fanta na Mutsonziwa (2021) wanaeleza kuwa kuelewa viwango vya riba na mfumuko wa bei kunawasaidia watu kugundua makosa katika mikataba ya mikopo, pamoja na kubaini kama faida inayotolewa na uwekezaji fulani ni ya kuaminika au la.

Vilevile, benki na taasisi za huduma ndogo za kifedha huvutiwa zaidi na wateja wanaoonyesha ujuzi wa kifedha, kama vile maarifa ya uwekezaji, jinsi ya kuhudumia ombi la mkopo, na mengineyo. Utafiti wa Kaiser et al. (2020) umeonyesha kuwa wateja wanaoomba mikopo ambao wamepata elimu ya kifedha wana uwezekano mkubwa wa kuaminiwa na kupata mikopo ukilinganisha na wale wasio na sifa hiyo.

Hivyo, kwa biashara ndogo na nyinginezo zisizo rasmi, zinaweza kujiandaa kwa kutunza taarifa zao za hesabu zao za biashara kwa umakini, kujua kiwango halisi cha faida kinachopatikana, na kuweka utaratibu rasmi wa kutathmini utendaji wao ili kuimarisha uaminifu miongoni mwa taasisi za kifedha.

Kadhalika, kuongezeka kwa maarifa ya kifedha kunawasaidia wateja wa huduma za kifedha kuelewa jinsi ya kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo wanapotumia huduma hizo. Hii inawajengea ujasiri wanapofanya miamala na kushirikiana na taasisi za kifedha.

Kwa mfano, mteja mwenye uelewa wa kifedha anapokosea muamala au anapokumbana na ucheleweshaji wa taarifa fulani, atajua jinsi ya kushughulikia suala hilo kwa utulivu na taratibu sahihi. Kinyume chake, mteja asiye na maarifa ya kifedha anaweza kupoteza imani kwa watoa huduma, jambo linaloweza kumfanya aache kabisa kutumia huduma hizo, hivyo kumkosesha fursa muhimu za kifedha.

Hata hivyo, elimu bora ni ile inayojengewa misingi imara mapema. Ujuzi wa masuala ya kifedha unapaswa kuanza kufundishwa katika ngazi za awali ili uote mizizi na kuleta matokeo chanya ya muda mrefu. Kwa mfano, kujumuisha elimu ya msingi ya kifedha katika shule za msingi na sekondari kutawasaidia watoto kuelewa dhana za fedha mapema, hivyo kuwajengea tabia za usimamizi mzuri wa fedha zitakazodumu maisha yote.

Vilevile, elimu ya fedha ni haki ya kila mtu na haipaswi kuwa kwa wanafunzi wa shule pekee. Programu za uelimishaji kuhusu dhana mbalimbali za kifedha zinapaswa kufanyika kwa njia tofauti ili kuwafikia watu wengi zaidi. Kwa mfano, kampuni zinazotoa huduma za kifedha zinaweza kutumia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kuelezea dhana muhimu za kifedha. Pia, vipindi vya televisheni vinavyotumia michezo ya kuigiza vinaweza kusaidia kueneza uelewa wa masuala ya fedha kwa njia inayoeleweka kirahisi.

Kadhalika, elimu ya fedha inaweza kuingizwa kwenye michezo maarufu inayofuatiliwa na wengi, kama vile mpira wa miguu, ili kufikisha ujumbe kwa hadhira kubwa kwa njia ya burudani na mafunzo kwa wakati mmoja.

Programu za kuelimisha masuala ya kifedha zinapaswa kupimwa na kufanyiwa tathmini ili kubaini kwa kiasi gani zinasaidia au zimefikia malengo yaliyokusudiwa. Mipango rasmi ya tathmini na ufuatiliaji inatakiwa kuwepo ambayo itafanyika mara kwa mara baada ya utekelezaji wa programu hizo.

Kwa kufanya hivyo, itakuwa rahisi kutathmini mwenendo wa utoaji elimu hiyo kwa walengwa, kubaini changamoto zinazojitokeza, na kurekebisha mbinu zinazotumiwa ili kuhakikisha zinafanana na mahitaji halisi ya jamii husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *