

“Wanamtafuta kila mahali na mtu huyo hata hajajificha” ni maneno ya wimbo wa Los Tucanes de Tijuana, kwa heshima ya Ismael “El Mayo” Zambada.
Mlanguzi wa dawa za kulevya mwenye umri wa miaka 76, mmoja wa waanzilishi watatu na, hadi sasa, kiongozi wa genge la Sinaloa la Mexico, alikamatwa siku ya Alhamisi na mamlaka ya Marekani.
Pia aliye kizuizini ni Joaquín Guzmán López, mtoto wa miaka 38 wa mwanzilishi mwingine wa shirika hilo, Joaquín “El Chapo” Guzmán – ambaye amekuwa akitumikia kifungo cha maisha nchini Marekani tangu 2019.
Likinukuu maafisa wa Mexico na Marekani, gazeti la Wall Street Journal linaripoti kuwa Zambada alidanganywa kuingia ndani ya ndege hiyo na mwanachama wa ngazi ya juu wa Sinaloa kufuatia operesheni ya miezi kadhaa ya Uchunguzi wa Usalama wa Ndani na FBI.
Ni pigo kubwa kwa walanguzi wawili wa dawa za kulevya wanaosakwa zaidi duniani, wanaotuhumiwa kwa utakatishaji fedha, rushwa, ulanguzi wa dawa za kulevya na uhalifu mwingine.
El Mayo, ambaye pia anajulikana kama “The Man with the Hat”, amevutia hali ya kuustajabisha wengi na kujulikana kwa zaidi ya miongo mitano katika biashara hiyo.
Wimbo wa Los Tucanes, ambao umetazamwa mara milioni 10 kwenye YouTube, unaendelea: “Sheria inataka kumzuia, maadui wanataka kumuua, lakini hakuna aliyefaulu – shetani anawatokea.”
Kutokamlanguzi hadi kiongozi

Kupanda kwa Zambada kutoka mlanguzi wa kawaida hadi kuwa “capo de capos” (bosi wa mabosi), kama anavyoitwa mara nyingi, ni hadithi ya mtu anayefahamu uhalisia wa mambo, ujanja na ufisadi.
Baada ya muda mfupi kama mfanyabiashara wa samani katika mitaa ya Culiacán, jiji lililo kaskazini-magharibi mwa Mexico, Zambada alianza kazi yake ya ulimwengu wa uhalifu kama mlanguzi katika miaka ya 1970.
Kwanza alifanya kazi kwa kampuni ya Guadalajara, mwanzilishi katika tasnia hiyo, ambayo iliuza opium, bangi na, hatimaye, kokeini.
Kisha alifanya kazi katika shirika la Juárez, kwanza kama meneja wa kati na kisha kama kiongozi, akizidi kuwa karibu na Amado Carrillo, anayeitwa “Bwana wa Anga”.
Kutoka huko, inaaminika kuwa aliunda mtandao wa mawasiliano huko Colombia, nchi ambayo aliendelea kupata marafiki wakubwa na washirika wa kutengeneza kokeini.
Wakubwa wengine walipokufa au kukamatwa, Zambada alizidi kuwa na nguvu. Hakuwa na tatizo la kumsaliti mshirika wake.
Lakini ikiwa kuna jambo lolote linalomtofautisha na vigogo wengine wa dawa za kulevya, ni kwamba hakuwa najionesha hadharani. Ni nadra sana kuzipata picha zake.
Imeripotiwa kuwa amefanyiwa upasuaji kubadili sura yake. Kwamba ana urefu wa 1.8m. Kwamba yeye ni mkubwa na mwenye nguvu. Kwamba ana wake na watoto wengi. Lakini hakuna zaidi ya hayo yanayofahamika.
Bajeti ya hongo ya $1m
Mmoja wa wana wa El Mayo, Vicente Zambada Niebla, alizuiliwa na mamlaka ya Mexico mwaka wa 2009. Shajara yake ya gereza ilitolewa baadaye.
Ndani yake, na katika ushahidi alioutoa kwa mamlaka ya Marekani, Zambada junior alisema kuwa baba yake alipanga bajeti ya $1m kwa mwezi kutoa hongo, na kwamba mtandao wake wa ushirikiano ulijumuisha benki na serikali.
El Mayo pia ameripotiwa kuwa mmoja wa walanguzi wa dawa za kulevya wanaojali sana kutengeneza uhusiano na jamii yake.
Amekuwa mlinzi wa El Álamo, makao yake ya asili, na miji mingine katika eneo la Sinaloa, akifadhili kazi na sherehe zao.
Mmoja wa warithi wa El Chapo

Chanzo cha picha, Getty Images
Machache yanajulikana kumhusu Joaquín Guzmán López, ambaye alizuiliwa pamoja na Zambada siku ya Alhamisi.
Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 38, anayejulikana kama El Güero, ni mtoto wa El Chapo na Griselda López Pérez, mke wa pili wa mlanguzi huyo wa dawa za kulevya.
El Chapo alikuwa na watoto 10 na wake watatu: Alejandrina Salazar, Griselda López na Emma Coronel.
Joaquín ni mwanachama wa Los Chapitos, seli inayosheheni watoto wa El Chapo, akiwemo kaka yake Joaquín Ovidio, ambaye alirejeshwa Marekani Septemba mwaka jana, kufuatia kukamatwa kwake nchini Mexico Januari 2023.
Wengine huzingatia jukumu la Joaquín katika shirika la uhalifu kama la kiasi kidogo kwa Ovidio. Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inasema kwamba Joaquín alifanya “kazi za kiwango cha juu cha uongozi na udhibiti” katika kundi la Los Chapitos na shirika la Sinaloa.
Mamlaka za Marekani zinashikilia kwamba baada ya kifo cha mtoto mkubwa wa Chapo, Edgar, Joaquín na Ovidio walirithi faida nyingi kutokana na mauzo ya mihadarati na kuanza kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kununua bangi nchini Mexico na kokeini nchini Colombia.
Kulingana na washirika wa zamani wa El Chapo, Joaquín na Ovidio pia walihusika katika kumsaidia mlanguzi huyo wa dawa za kulevya kutoroka kutoka katika gereza lenye ulinzi mkali nchini Mexico mwaka wa 2015 – kutoroka kwake jela kwa mara ya pili baada ya mashtaka yanayohusiana na mauaji na ulanguzi wa dawa za kulevya mnamo 1993.
Mamlaka za Marekani pia zinashikilia kuwa Joaquín na Ovidio Guzmán López wanaendesha angalau maabara 11 zinazozalisha methamphetamine katika jimbo la Sinaloa la Mexico.
Joaquín alishtakiwa kwa mara ya kwanza kwa mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya mwaka wa 2018 nchini Marekani.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah