EAC na SADC zafikiria kupeleka wanajeshi mashariki mwa Kongo

Nchi za Afrika Mashariki na kusini zinachunguza uwezekano wa kupeleka wanajeshi kulinda maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo kwa sasa yanadhibitiwa na waasi wa M23, kulingana na waraka ambao shirika la habari la  REUTERS limepata kopi siku ya Jumanne.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Jumuiya za kikanda za EAC na SADC tayari zimetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini, ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 7,000 tangu mwezi wa Januari, kulingana na waziri mkuu wa Kongo.

Hati ambayo shirika la habari la REUTERS limepata kopi inaelezea mapendekezo kwa wakuu wa ulinzi baada ya mkutano wa wataalamu wa kiufundi nchini Tanzania mnamo Februari 23. Wakuu wa majeshi wanatarajiwa kutayarisha ripoti kwa majadiliano mwishoni mwa juma hili.

Waraka huo unabaini kwamba jumuiya hizo za kikanda zinafikiria kuomba mamlaka, pamoja na vikosi vya Umoja wa Afrika ambavyo havijatajwa, kupata maeneo yanayodhibitiwa na M23 katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini, na kwamba ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO pia unaweza kuombwa kuimarisha uwepo wake katika eneo hilo.

“Ni pendekezo, bado hatujafahamishwa,” chanzo cha Umoja wa Afrika kimesema, na kuongeza kuwa ushiriki wowote wa AU itabidi uidhinishwe na Baraza lake la Amani na Usalama.

Waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wameteka miji mikubwa miwili ya nchi hiyo, Goma na Bukavu, na viwanja vya ndege, na kukata njia kuu za kutoa misaada kwa mamia yaa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao.

Ili kuboresha utoaji wa misaada ya kibinadamu, kusaidia kuwarejesha makwao wafu na kuwahamisha majeruhi, wataalam kutoka kambi zote mbili wanashauri kufanya mazungumzo na M23 ili kufungua upya njia na uwanja wa ndege wa Goma.

Waraka huo unabainisha kuwa hadhi ya ujumbe wa jumuiya ya kusini mwa Afrika nchini Kongo, inayojulikana kama SAMIDRC, lazima ijadiliwe na wahusika katika mzozo huo.

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yenye wanachama 16, ambayo iliongeza muda wa misheni yake ya kijeshi nchini Kongo mwishoni mwa mwaka jana kusaidia jeshi la Kongo kupambana na waasi, imepata hasara tangu kuanza kwa mwaka 2025.

Rwanda inakanusha madai kwamba inasambaza silaha na wanajeshi kwa kundi la waasi la M23, ambayo ni ya hivi punde katika safu ndefu ya waasi wanaoongozwa na Watutsi kuibuka mashariki mwa Kongo. Rwanda inasema inajilinda dhidi ya tishio la wanamgambo wa Kihutu ambao inasema wanasaidia jeshi la Kongo katika vita vyake.