Dar es Salaam. Mondi anakawaida ya kutoa wimbo kila wiki. Na siyo kutoa tu. Na wimbo ‘ukahiti’. Yaani ‘everi wiki anaririizi traki na inaenda vairo’. Jamaa kashika kila kitu kinachohusu muziki. Kuna wakati dunia inapendelea sana.
Dunia ya muziki Bongo ina mkataba na Mondi. Inampa anachotaka naye anaipa inachotaka. Mondi ni sehemu ya vijana wachache duniani, ambao wanafurahia kazi yao. Haya mambo ni ya kiroho zaidi ya malimwengu.

Unatamani kuwa Diamond? Hapana mimi sitamani hata kuwa na nusu ya alichonacho. Kuwa Diamond ni mzigo mzito sana. Mondi kila kitu kwake kinaenda sawa. Muziki mkubwa, jina kubwa, akaunti kubwa na umri wake mdogo.
Mondi ameelemewa. Kama angekuwa na kichwa kidogo (akili na utulivu). Ni rahisi kuwa mwehu. Tuliwashuhudia wanamuziki ambao walipata pesa na jina katika umri mdogo. Mwishowe wakawa wehu. Walifeli kila kitu na kwa muda mfupi.
Tunaongelea Diamond wa miaka 14 akiwa kileleni. Staa mkubwa zaidi. Yupo juu ya wote na kwa kila kitu katika muziki wetu. Ni dogo ambaye anapata ambacho waliomtangulia wote hawakupata. Hii siyo kawaida kawaida.
‘Malti talentedi’ ndo huyu. Kwa maana kwamba anaweza kufanya gemu lake vizuri. Anaweza kutengeneza pesa na anaweza kujitunza yeye na pesa zake. Wapo wanaopata pesa lakini hukosa hekima ya kutumia pesa. Hupoteza kila kitu.

Wapo wanaopata jina kubwa lakini hawawezi kuyatunza. Na kuna wale wenye vipaji vikubwa lakini hawawezi kujisimamia. Kipaji ni jambo moja na kukisimamia kipaji ni mtambuka. Yes ni ngumu sana na wengi walishindwa.
Msanii unahitaji akili kubwa ya juu yako ili kuweza kusimamia nyendo zako. Lakini Diamond ni ‘fulu pakeji’, ana kipaji cha muziki na kipaji cha kujisimamia. Hii ni karama kubwa sana na hutokea kwa wachache.
Mondi wa sasa kila lililo lake hugeuka dhahabu. Kavuka daraja la kuweza kuyumba kimuziki. Hashuki leo wala kesho achana na mtondogoo. Tupo naye sana. Simuoni akishuka kisanii na pia sioni akishika kiuchumi.
Hii ni kwa sababu dogo anatenda vitu vya mbele ya muda. Mondi wa Nenda Kamwambie alifanya vitu vya 2020 ikiwa ni mwaka 2010. Tusichukuliane poa kwenye hizi mishe za maisha.
Hivi sasa anafanya mzuki kionekane kitu chapesi sana. Nyimbo aina ya Ukimuona, Nataka Kulewa, Nitarejea, Je Utanipenda sijui Moyo Wangu. Ni nyimbo ambazo anaweza kuachia kila mwisho wa wiki na akafunika.
Mondi kishavuka kuwaimbua wakazi wa Maji Matitu, siyo mali ya Kitunda na Mpiji Majohe. Alishahama Mawazo ya Kwa Msisiri. Mondi huyu ni mali kamili ya dunia. Shida yetu tunapenda sana kuwadogosha washikaji.
Tunachukuliana poa poa sana. Hasa ‘Kiibodi Woriazi’ ambao kwao ‘kutaipu’ chochote kwa mtu yeyote huona sawa tu. Mtu ana bando la buku jero, haoni hatari kumtusi milionea. Unaweza kumpuuza lakini heshimu pesa zake basi.
Wiki hii Diamond ametoa wimbo wake unaitwa Moyo. Kabla ya huo aliachia mnanda wake unaoitwa Nitafanyaje. Hizi ukizisikiliza unaweza kudhani ni nyimbo zake za zamani. Hii siyo kwa sababu ya kufanana kwa melodi au mashairi.
Ni kwa sababu haziendani na Mondi wa sasa. Ngoma hizo hizo zikitolewa na mwingine zitampaisha kisanii kwa siku moja. Lakini Diamond kwake ni ngoma zinazopendwa sana na raia ila hazina uzito wake. Noma na nusu.
Mondi soko lake ni Free Town mpaka Bulawayo. Hizi nyimbo mbili alizotoa ni kama shukurani kwa mashabiki wa nyumbani. Ukweli ni nyimbo nzuri na tamu lakini zipo daraja la Mbosso na wenzake. Mondi ana ‘klasi’ yake.
Mondi ana dunia yake. Ni miaka mingi kaachana na sisi kimtazamo. Tatizo wengi tulichelewa kumuelewa kama hayupo nasi. Mondi wetu aliishia ni ngoma ga Number One. Mondi wa Eneka kuja juu hakuwa Mondi wetu tena.
Wakaanza kusema kashuka kisanii. Hawezi kuandika kama zamani. Na anaiga Wanaijeria. Na zaidi wakaja tena na kauli za anaandikiwa nyimbo na kina Mbosso. Kila neno la kutaka aonekane kashuka lilisemwa.
Ajabu wakati anasemwa hivyo, tayari alikuwa anafanya shoo nyingi za nje kuliko ndani. Leo Mayote kesho Naii keshokutwa Ubelgiji. Hakuwa msanii wa Ubena Zomozi wala Pasiansi. Ni wazi kwamba alituacha mbali.
Dogo amekuwa mbele ya muda kwa wakati wote. Tangu atoke kisanii na ngoma ya Nenda Kamwambie, Mondi hajawahi kutoa video yenye hadhi ya ‘besidei’, ‘komonio’ wala ‘kicheni pati’. Pini juu ya pini.
Alivyozidi kusogea mbele, na muziki wake ukazidi kusogea mbali. Kutoka Dar mpaka Dakar. Toka Nairobi mpaka Gaborone. Kutoka shoo jukwaa la Dar Live Mbagala hadi jukwaa la AFCON kule Rabat!
Kuna Bongo Fleva na kuna Diamond. Huyu ni muziki ndani ya muziki. Ni pesa ndani ya pesa. Hivi vitu ni zaidi ya vipaji vya kawaida. Ni karama. Dogo aliumbwa awe alivyo sasa, tajiri katika umri mdogo.
Haya mambo ni Mungu zaidi.