Dar es Salaam. Baada ya msanii wa singeli nchini Dulla Makabila kuongoza kwa kufanya vizuri kwenye muziki huo. Sasa ametangaza nia yake ya kufungua lebo ya muziki wa singeli.
Dulla ameyasema hayo kwenye mahojiano na Mwananchi na kuweka wazi kuwa tayari amepata msanii wa kumtambulisha kwa mashabiki.

“Nahitaji kufungua ‘record label’ na tayari nimeanza kutuma maombi sehemu mbalimbali. Kwa sababu sihitaji liwe jambo dogo lakini mpaka sasa msanii nimeshampata sio wa kuanza kutafuta,” amesema Dulla.
Lakini pia ameongezea kuwa msanii huyo, ana uwezo mkubwa wa kufanya singeli.
“Ni kiboko huyo mtoto mimi mwenyewe namuogopa. Mimi kwa nafasi yangu sitakiwa kumsaini mtu yeyote tu ilimradi. Huyo mtu anayekuja anajua sana kwa hiyo punde tutamtambulisha yeye pamoja na lebo,” amesema Dulla
Kutokana na uhaba wa wasanii wa kike kwenye muziki wa singeli, Dulla amesema msanii wake atakuwa wa kike.
“Msanii kutoka kwenye lebo, sio kwamba haridhishwi, ni kutaka kukua kwa hiyo watu wanatafsiri vibaya mimi siamini lebo zinawanyonya wasanii. Ila muda mwingine msanii anataka kukua na kuwasaidia watu wengine,” amesema Dulla.

Sambamba na hayo Dulla makabila amegusia kuhusu shoo yake ya Asante Singeli iliyofanyika Februari 2, 2025 kwenye viwanja vya Mbagala Zakiem. Akifanikiwa kuwakutanisha wasanii tofauti tofauti wakiwemo wa Bongofleva na Hiphop.
“Kitu ambacho watu hawajui mimi ndio msanii wa singeli sipendwi na waimba singeli wenzangu. Mimi niko sawa na ndugu zangu kina Madee, Kusah, Chege, Kontawa Jay Melody ndiyo watu wanaonisapoti mimi. Waimba singeli wenzangu hawanikubali nalijua hilo.
Wanafanya hivyo kwa sababu nimepiga hatua.Hakuna anayenifata kuanzia maisha yangu, gari ninazotembele, nyumba ninayoishi, akaunti yangu inavyosoma, simu ninazopigiwa na watu wazito ni tofauti na wao,” amesema Makabila
Kufanya shoo ya ‘Asante Singeli’ kwa Dulla Makabila ilikuwa moja ya ndoto kubwa aliyokuwa akiiota siku nyingi.
“Singeli imenibadilishia maisha yangu. Sikuwahi kuwaza kama Singeli ingekuja kunibadilishia maisha yangu nilikuwa siwazi. Kuna siku mimi nitakuwa na laki moja ya pamoja lakini leo kwenye akaunti yangu kuna zaidi ya Sh 100 milioni.
“Kwa hiyo hicho ni kitu kikubwa sana muziki wa singeli umenifanyia ndio maana nikasema Asante Singeli, kila kilicho kuwa kwenye maisha yangu kimetokana na singeli,” amesema

Dulla Makabila alitoa wimbo wake wa kwanza mwaka 2016 na kwa miaka yote, kwenye tasnia ya muziki wa singeli amekuwa miongoni mwa wasanii wanaowakilisha vyema.
Utunzi wake wa nyimbo unagusa jamii na utumbuzaji wake wenye vibe ya kutosha. 2022 alifanikiwa kutwaa Tuzo mbili ambazo ni Mwandishi Bora wa muziki wa singeli na Mtumbuizaji Bora. Pia 2024 alishinda tuzo ya Msanii Bora wa kiume wa Singeli Tanzania