LONDON, ENGLAND. Wanasema fanya mazuri 99, lakini kosa moja tu linakushusha chini. Ndiyo imemtokea bondia Muingereza Anthony Joshua ambaye hivi karibuni alipoteza pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa dunia wa IBF la uzito wa juu mbele ya Daniel Dubois.
Pambano hilo ambalo mahudhurio yake yalivunja rekodi rasmi ya zaidi ya watazamaji 98,000, ilishuhudiwa raundi ya tano Joshua akipigwa na shughuli ikaishia hapo.
Joshua alikuwa anafukuzia ubingwa wa tatu wa dunia uzito wa juu IBF, ambapo licha ya kupoteza vibaya kwa KO huku watu wakisema enzi zake zinaelekea mwisho, mwenyewe amesisitiza kwamba: “Bado sijamaliza kucheza ngumi, nitaendelea kupambana.”
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 34, alilamba sakafu mara nne kutokana na kipigo kikali kutoka kwa Dubois huku watu wengi wakisema lazima Joshua atastaafu siku si nyingi kwani ameonekana amechoka.
Ngumi ya Dubois iliyotua kwenye kidevu cha Joshua, ndiyo ilikuwa ya mwisho katika pambano hilo kwani liliishia hapohapo baada ya Joshua kuanguka chini na kushindwa kuendelea.
Licha ya wengi kusema Joshua anapaswa kufikiria kukaa pembeni kutokana na kushuhudiwa siku hiyo akipigwa kama anajifunza ngumi, lakini bingwa huyo wa zamani wa Olimpiki alisema safari yake katika ndondi bado haijafika mwisho na siku zijazo kuna uwezekano wa mechi ya marudiano dhidi ya Dubois, pia dhidi ya Muingereza mwenzake, Tyson Fury.
HUYU NI NANI?
Anthony Oluwafemi Olaseni Joshua, alizaliwa Oktoba 15, 1989, Watford, England. Mama yake ni Mnigeria wakati baba yake akiwa na uraia wa Nigeria na Ireland.
Joshua ni bondia maarufu wa uzito wa juu, anayejulikana kwa matumizi makubwa ya nguvu na mbinu madhubuti anapokuwa ulingoni.

Bondia Anthony Joshua akijaribu kunyanyuka baada ya kulambishwa sakafu na mpinzani wake Daniel Dubois hivi karibuni wakati wa pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa dunia wa IBF. Picha na Mtandao
Alianza kujihusisha na mchezo wa ngumi akiwa na umri wa miaka 18, baada ya kugundua kipaji chake katika mchezo huo. Alianzia katika ngumi za ridhaa na haraka akapata mafanikio. Mwaka 2011, alishinda medali ya shaba kwenye mashindano ya dunia ya vijana na mwaka 2012 alishinda medali ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya London.
Baada ya mafanikio hayo, Joshua aliamua kuhamia kwenye ngumi za kulipwa mwaka 2013 ambapo alicheza pambano lake la kwanza la kulipwa Oktoba, akashinda.
Ushindi huo ukamfanya ajijengee jina na kuwa mmoja wa mabondia maarufu zaidi ulimwenguni.
Mwaka 2016, alishinda taji la IBF baada ya kumchapa Charles Martin, kisha aliongeza mataji mengine kama WBA (Super) na WBO.
Miongoni mwa mapambano yake maarufu ni dhidi ya Wladimir Klitschko mwaka 2017, ambapo alishinda kwa KO katika raundi ya kumi, mchezo uliovutia watazamaji wengi na kuimarisha hadhi yake.
Ingawa Joshua amepata mafanikio makubwa, lakini amekumbana na changamoto kadhaa, ikiwemo kupoteza pambano lake la kwanza dhidi ya Andy Ruiz Jr, mwaka 2019. Hata hivyo, alifanikiwa kurekebisha makosa yake na kupata ushindi katika pambano la marudiano dhidi ya Ruiz baadaye mwaka huo. Hali hiyo ilionyesha uwezo wake wa kutokubali kushindwa.
Mwaka 2021, Joshua alikabiliana na Oleksandr Usyk, bondia wa kizazi kipya mwenye mbinu za hali ya juu. Alipoteza pambano hilo sambamba na lile la marudiano lililofanyika mwaka 2022, jambo lililosababisha watu wengi kuhoji kuhusu mustakabali wake.

Hata hivyo, Joshua aliendelea kuwa na matumaini na kusema kwamba atarudi kwenye ubora wake na kushinda kama zamani, kweli ikawa hivyo ambapo mapambano manne yaliyofuatia akashinda yote kabla ya hivi karibuni kupigwa tena kwa KO.
MAPAMBANO 32, VIPIGO 4
Mkali huyo kupigwa kwake na Dubois ilikuwa ni mara ya nne kati ya 32 alizopanda ulingoni tangu Oktoba 5, 2013 alipoanza kazi hiyo. Katika mapambano manne aliyopoteza, mawili ni kwa KO na mengine uamuzi wa majaji.
Joshua si mnyonge kwani akiwa amepoteza mapambano manne, ameshinda 28 huku 25 yakiwa kwa KO na matatu pekee ni uamuzi wa majaji.
WABABE WAKE
Daniel Dubois ndiye bondia wa mwisho kumchakaza Joshua katika pambano lililofanyika Septemba 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Wembley uliopo London, England.
Pambano hilo la kuwania ubingwa wa dunia uzito wa juu IBF, Joshua alipigwa KO raundi ya tano wakati pambano likipangwa kuchezwa kwa raundi 12.
Kabla ya kichapo hicho, Joshua alipigwa mapambano mawili mfululizo na Oleksandr Usyk, Septemba 20, 2022 kuwania ubingwa wa WBA (Super), IBF, WBO, IBO, huko King Abdullah Sports City, Jeddah, Saudi Arabia.
Hilo lilikuwa pambano la marudiano baada ya lile la kwanza dhidi ya Oleksandr Usyk Septemba 25, 2021 kuchapwa kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur nchini England walipokuwa wakiwania ubingwa wa WBA (Super), IBF, WBO na IBO kwa uzito wa juu.
Mtu wa kwanza kumkalisha Joshua alikuwa Andy Ruiz Jr ambaye alifanya kazi kubwa baada ya bondia huyo kucheza mapambano 22 mfululizo bila ya kupoteza.
TKO aliyopigwa raundi ya 7 kati ya raundi 12 za pambano lao lililofanyika Juni Mosi 2019 kwenye Ukumbi wa Madison Square Garden, New York, Marekani, ilitosha kwake kupoteza ubingwa wa WBA (Super), IBF, WBO, na IBO uzito wa juu.