
IKIWA ni kati ya timu zinazokabiliwa na hatari ya kushuka daraja, Coastal Union ya Tanga ina kazi kubwa mbele ya Yanga wakati timu hizo zitakapokutana Jumatatu hii kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.
Yanga itawakaribisha Coastal Union katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara huku washambuliaji wake, Clement Mzize na Prince Dube wakitarajiwa kuingia uwanjani wakiwa na akili mbili wakati wapinzani wao wakiwaza jambo moja pekee.
Kwa sasa Yanga inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 61, imefunga mabao 61, karibu nusu ya mabao hayo ni mchango wa washambuliaji wake hatari, Mzize na Dube ambao kila mmoja akifunga 11 na wana jumla ya asisti 9.
Akili za washambuliaji hao kwanza ni kuwaza kushinda ili kuiwezesha timu kujitanua zaidi kileleni mwa msimamo, pia wao wenyewe kuongeza mabao ili kumfikia kinara, Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye 12.
Chini ya kocha Miloud Hamdi, Yanga imekuwa na mwendelezo mzuri wa ushindi. Tangu kuwasili kwake, Hamdi ameiongoza timu hiyo kushinda mechi tano mfululizo baada ya kuanza na suluhu dhidi ya JKT Tanzania. Baada ya hapo, Yanga iliwachapa KMC (6-1), Singida Black Stars (2-1), Mashujaa (5-0), Pamba Jiji (3-0), na Tabora United (3-0).
Hali hiyo imeifanya Yanga kuwa timu tishio zaidi kwa sasa, wakifunga wastani wa mabao matatu kwenye kila mchezo chini ya Hamdi. Kocha huyo raia wa Algeria alisema: “Kile ambacho tumeanza kukijenga sasa ni mwendelezo wa utamaduni wa kushinda. Kila mechi ni fursa mpya ya kujifunza na kuboresha.”
Kwa upande wa Coastal Union, hali si shwari. Timu hiyo haijashinda mchezo wowote kati ya saba iliyopita, ikipata sare nne na kupoteza tatu, wakifunga bao moja tu na kuruhusu mabao saba.
Takwimu hizi zinadhihirisha pengo la ubora baina yao na mabingwa watetezi Yanga.
Ukuta wa Coastal Union unaoongozwa na Fales Gama kwenye lango, wakati Miraji Abdallah na Ali Abubakar wakicheza beki za pembeni, huku Ally Msangi na Lameck Lawi wakisimama mabeki wa kati, umeruhusu mabao 25 katika michezo 24, wana wastani wa kufungwa bao moja kwenye kila mchezo.
Kwa sasa, Coastal Union ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 25. Ikiwa haitapata matokeo mazuri, inaweza kujikuta ikizama zaidi kwenye vita ya kuwania kubaki Ligi Kuu, jambo ambalo linaongeza uzito wa mechi hii kwa upande wao.
Kihistoria, Yanga imekuwa na ubabe mkubwa dhidi ya Coastal Union katika misimu ya hivi karibuni. Katika mechi tisa zilizopita kati ya timu hizo kuanzia Oktoba 2020, Yanga imeshinda mara nane, huku Coastal wakipata ushindi mara moja tu.
Kwa msimu huu, kwenye mzunguko wa kwanza Oktoba 26, 2024, Yanga ikiwa ugenini ilishinda kwa bao 1-0. Msimu uliopita Aprili 27, 2024, Yanga ilishinda tena 1-0, huku mechi ya mzunguko wa kwanza Novemba 08, 2023 ikimalizika pia kwa Yanga kushinda 1-0.
Mwaka 2022, Yanga ilishinda kwa mabao 3-0 na 2-0. Mwaka huo huo, ilishinda tena 3-0 na 2-0. Ushindi pekee wa Coastal Union ulitokea Machi 04, 2021 walipoibuka na ushindi wa 2-1, kabla ya Yanga kujibu mapigo kwa ushindi wa 3-0, Oktoba 03, 2020.
Rekodi hiyo inazidi kuiweka Yanga juu kiakili na kihistoria, huku pia ikiongeza presha kwa Coastal ambayo inapaswa kujipanga kimbinu na kisaikolojia ili kuvunja ubabe huo uliodumu kwa takribani misimu minne mfululizo.
Msimu huu, Yanga imekuwa na uwiano mzuri kati ya safu ya ulinzi na ushambuliaji. Wameruhusu mabao tisa pekee katika michezo 23, ikiwa ni wastani wa bao moja kila mechi mbili.
Mechi hii inatarajiwa kuwa kipimo kingine cha mbinu za Hamdi, ambaye sasa anatamani kuipa Yanga alama tatu nyingine ili kupanua mwanya wa pointi dhidi ya Simba SC kutoka nne hadi saba.
Kwa upande mwingine, Coastal wanahitaji alama yoyote, hata sare, ili kujiweka vizuri zaidi dhidi ya timu zinazopambana kubaki kwenye ligi. Nafasi yao ya kujinusuru ipo, lakini inategemea ufanisi wa mechi kama hii dhidi ya vinara wa ligi.