Dube ashtua Yanga, ataka rekodi

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube anakimbiza mwizi kimya kimya kwa kufukuzia rekodi yake mwenyewe licha ya kuwa na msimu bora zaidi ndani ya kikosi cha timu hiyo.

Dube alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Azam ambapo msimu wake wa kwanza Ligi Kuu Bara ule wa 2020/21 alifunga mabao 14 hivyo amebakiza mabao matatu kuvunja rekodi yake mwenyewe lakini msimu wa 2022/23 alifunga mabao 12 amebakiza bao moja pekee kuivunja rekodi hiyo akiwa na mechi sita mkononi ukiondoa ile ya dabi ambayo hatima yake haijulikani.

Dube msimu huu akiwa ndani ya kikosi cha Yanga amefunga mabao 11 na kutoa asisti saba, hivyo amehusika kwenye mabao 18 kati ya 61 yaliyofungwa na timu hiyo hadi sasa kwenye mechi 23 ambazo kikosi chake kimecheza. 

Licha ya kubakiza mabao matatu kufikia rekodi yake mwenyewe tayari amevuka rekodi hiyo kwa kuisaidia Yanga kuhusika kwenye mabao 18 hadi sasa na kuweka rekodi ya kuwa na msimu bora ndani ya kikosi hicho cha wababe wa Jangwani.

Akiwa na Azam alicheza misimu mitatu na nusu akifunga mabao 34 kwenye mechi 54. Msimu wa 2020-2021 alifunga mabao 14, ilhali ule wa 2021-21 aliingia kambani mara moja kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyokuwa yanamuweka nje kwa muda, huku ule wa 2022-23 alifunga 12 na ule wa wa mwisho kuitumikia Azam FC (2023-24) alicheza miezi sita na kufanikiwa kufunga mabao saba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dube alisema kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza ndani ya Yanga ndiko kutakakompa nafasi ya kufanya mambo makubwa zaidi na anafanya kwa kushindana na ‘kivuli chake’ hakuna anayemtazama.

“Nashukuru Mungu napata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi chenye mafanikio na wachezaji wengi bora ambao wana uchu wa mafanikio, hivyo wananiongeza nguvu ya mimi kupambana zaidi. Kuhusu kushindana sishindani na mtu nashindana na kivuli changu mwenyewe,” alisema na kuongeza:

“Ni msimu wangu wa kwanza Yanga na nimeweza kucheza na kufunga mabao hayo 11. Nitafunga kila nitakapopata nafasi, lakini pia nitatoa nafasi ya mchezaji mwingine kufunga kama nitakuwa sipo eneo sahihi la kutumbukiza mpira nyavuni.”

Dube alisema anafurahia maisha ndani ya Yanga kutokana na namna wanavyoishi nje na ndani ya uwanja, wakicheza kwa kushirikiana huku akiweka wazi kuwa wanacheza kwa kuipambania nembo ya timu hiyo na kujipambania wao binafsi wakiwa na malengo ya kuifanya timu hiyo kuwa bora ndani na nje.

Akizungumzia kuhusiana na rekodi yake, Dube alisema ni msimu wa tatu sasa anapambana kufikia rekodi yake ya msimu wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara, lakini anaamini ndani ya Yanga atafanya hivyo na ikiwezekana ataivuka na kuandika rekodi mpya kutokana na aina ya wachezaji waliomzunguka na namna wanavyompa ushirikiano.

“Hakuna mchezaji ambaye anacheza bila malengo. Napambana ili niweze kufikia ni msimu wa tatu sasa naamini ndio utakaoweza kuwa bora kwangu. Nina timu ambayo ina wachezaji wengi bora.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *