Droo ya CAF kumkutanisha Ahmed Ally na mastaa

Dar es Salaam. Staa wa zamani wa soka barani Afrika na Algeria, Rabah Madjer atakuwa miongoni mwa watu maarufu watakaokuwa pamoja na Meneja Habari wa Simba, Ahmed Ally huko Doha Qatar, Alhamisi Februari 20, 2025.

Wawili hao ni miongoni mwa watu ambao wamealikwa kushiriki matukio mawili makubwa yatakayofanywa na Shirikisho la Mpira wa miguu Afrika (CAF) siku hiyo.

Droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na droo ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ni matukio mawili ambayo yatamkutanisha Ahmed Ally na Madjer ambaye amewahi kushinda mara moja taji la Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) akiwa na timu ya taifa ya Algeria.

Droo hiyo itafanyika katika makao makuu ya kituo kikubwa cha runinga cha Bein Sports kuanzia saa 11 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki.

Madjer atashiriki tukio hilo akiwa ni miongoni mwa wachezesha droo wakati Ahmed Ally yeye atakuwa ni mmoja wa wawakilishi wa Simba ambayo ni miongoni mwa timu shiriki katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Taarifa iliyotolewa na Simba leo, Jumanne, Februari 18, 2025 imethibitisha kuwa Ahmed Ally atahudhuria droo hiyo akiwa pamoja na mtendaji mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru.

“Mtendaji Mkuu wa klabu, Zubeda Sakuru na Meneja Habari, Ahmed Ally watahudhuria droo ya kupanga ratiba ya robo fainali ya michuano ya vilabu barani Afrika itakayofanyika Februari 20, 2025 jijini Doha, Qatar.

“Ikumbukwe kuwa Simba SC ni timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambayo imetinga robo fainali ya michuano hiyo ya CAF,” imesema taarifa ya Simba.

Katika uchezeshaji wa droo hiyo, Madjer atashirikiana na staa wa zamani wa Zambia na TP Mazembe, Rainford Kalaba.

Kalaba ana historia kubwa na mashindano yote hayo mawili kwani amewahi kuyatwaa kwa nyakati tofauti akiwa na TP Mazembe.

Katika droo hiyo, Simba itakuwa kwenye chungu cha kwanza na timu za USM Alger, Zamalek na RS Berkane.

Chungu cha pili kitakuwa na timu za ASEC Mimosas, Al Masry, Stellenbosch na CS Constantine.